Jecha ndio chanzo cha unyonge wetu

Mzee akionekana akiburura samaki kutoka kwenye fukwe za kuvutia Zanzibar
Mzee akionekana akiburura samaki kutoka kwenye fukwe za kuvutia Zanzibar

NCHI hii – Zanzibar inayoundwa na visiwa viwili vikubwa vya Unguja na Pemba, na vingine kadhaa vidogo – ipo kwenye unyonge mkubwa. Ni unyonge ulio ndani ya nyoyo za watu wake – Wazanzibari.

Unyonge huu unatokana na uharibifu wa msingi muhimu wa ustawishaji demokrasia uliofanywa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, tuseme, zaidi kidogo ya mwezi mmoja sasa.

Wananchi wamekuwa wakiambiwa wanayo fursa ya haki iliyobainishwa ndani ya katiba kwamba kila baada ya miaka mitano, wanachagua viongozi wanaowataka kwa njia ya kidemokrasia.

Kweli, ukiiangalia sehemu ya mwisho ya utangulizi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inaeleza: Kwa hivyo basi, Katiba hii imetungwa na Baraza la Wawakilishi katika kikao chake cha Oktoba 9, 1984, kwa niaba ya wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Zanzibar inaongozwa na serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ya kijamaa.

Katika Sura ya Kwanza ya Katiba hii, Ibara ya 4, inaelezwa kuwa Katiba hii itakuwa ndio yenye nguvu za kisheria nchini kote; na Ibara ya 5, inaelezwa Zanzibar itafuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa wenye kuheshimu Utawala wa Sheria; Haki za Binaadamu, Usawa, Amani, Haki na Uadilifu.

Ibara hiyohiyo fungu A(1), inaelezwa Zanzibar itafuata mfumo wa mgawanyiko wa madaraka kati ya mamlaka tatu – Mamlaka ya Utendaji (Serikali); Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma (Baraza la Wawakilishi); na Mamlaka ya Kutekeleza utoaji haki (Mahkama).

Upatikanaji wa mamlaka ya utendaji hutokana na kuwepo uchaguzi. Wananchi watashiriki uchaguzi kwa utaratibu uliowekwa na sheria ya uchaguzi iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi, kuchagua viongozi wa kuwawakilisha.

Sasa wananchi wameshiriki uchaguzi, hatua ya kutekeleza maamuru ya Katiba ya Zanzibar; hatua ambayo ni ya kuwezesha wananchi kuipata serikali waliyoichagua wenyewe ambao ndani ya Katiba, yamebainishwa mamlaka yao kuwa huyagawa kwa viongozi wanaowachagua wawaongoze.

Kwa bahati mbaya, wanatokea watu wanaoitwa wanasiasa wanapokonya wananchi haki yao hii ya kuchagua viongozi ili kuwapa kwa mujibu wa katiba, mamlaka ya kuongoza serikali yao, ikawa kweli serikali ya watu, kwa ajili ya watu na kwa niaba ya watu hao.

Wanasiasa hao wanajipa mamlaka yasiyokuwa yao, yasiyoelezwa popote pale kwenye Katiba ya Zanzibar, na kuyakandamiza maamuzi halali ya wananchi ambayo waliyafanya kupitia visanduku vya kura. Haya ndiyo matakwa ya kikatiba, si matakwa ya watu binafsi.

Wanasiasa wanavuruga utaratibu wa kikatiba. Hii maana yake ni kwamba wanavunja misingi ya katiba. Kwa maana nyingine wanasiasa hao wanataka kuweka uongozi usiochaguliwa na wananchi; na huo utakuwa ni uongozi usiotambuliwa na katiba. Utakuwa ni uongozi haramu.

Zanzibar imo ndani ya hilaki hii – kwamba Oktoba 25 watu wake walipiga kura, wakiamini wanachagua uongozi wanaotaka uongoze serikali yao. Lakini wanasiasa wachafuzi walipoona maamuzi ya wananchi waliopiga kura hayakuendana na matakwa yao binafsi, wakatumia nguvu kukandamiza haki ya wananchi.

Wameshajisahaulisha kuwa Katiba imetoa haki kwa wananchi kuchagua viongozi watakaowapa dhamana ya kuongoza serikali yao, ile ambayo imetajwa na katiba kuwa ndio (Ibara 5(A) Mamlaka ya Utendaji na Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia utekelezaji wa Shughuli za Umma (Baraza la Wawakilishi).

Mamlaka ya Utendaji huongozwa na Rais, lakini viongozi wa kushirikiana nao kuendesha shughuli za umma hupatikana kupitia Baraza la Wawakilishi. Wananchi wanapoambiwa wanashiriki uchaguzi mkuu, huwa wanamchagua Rais wamtakae awaongoze, na wanachagua Wajumbe watakaounda baraza hilo.

Baraza la Wawakilishi ndimo hupatikana wateuliwa kuwa mawaziri ambao wakishateuliwa na yule Rais aliyeshinda uchaguzi, rais aliyechaguliwa na wananchi kwa njia ya uchaguzi unaoleta kura zilizo halali, wanaunda Baraza la Mapinduzi (au Baraza la Mawaziri).

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha alipoteuliwa kuongoza tume, alikabidhiwa mamlaka ya kusimamia utaratibu wa kupatikana kwa Mamlaka ya Utendaji pamoja na Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia utekelezaji wa Shughuli za Umma.

Kwa kile alichokifanya – kutangaza kwa ubinafsi wake kufuta uchaguzi uliokuwa njia halali ya wananchi kutafuta mamlaka hizo mbili kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, amefanya uhalifu wa kukandamiza haki ya wananchi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Jecha amesaliti dhamana aliyopewa na Rais kupitia nguvu ya Katiba ya Zanzibar. Kwa hakika bwana huyu amesaliti wananchi wa Zanzibar ambao ndio wenye mamlaka ya nchi yao kupitia Katiba yao.

Ukitaka kujua uzito wa uhalifu wa uwajibikaji na usaliti wa kikatiba alioufanya Jecha, angalia viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tangu Jecha atoe tamko haramu (kama isemwavyo na wataalamu wabobezi wa sheria na katiba) la kufuta uchaguzi.

Nyendo zao zimekuwa zilizojaa ulaghai, uongo na ubabaishaji; wanatembea huku wakijiapiza na hapo hapo wakiwa wanajifariji. Katika kudhani wanatibu mazonge waliyonayo, viongozi wa CCM wameamua kuongeza kazi na utashi wa kudanganya umma na ulimwengu.

Baada ya kujitahidi bila ya mafanikio kuaminisha watu kuwa uchaguzi uliharibika, ikiwemo eti kura zao kuibwa na mawakala wa Chama cha Wananchi (CUF) na watumishi wa ZEC, wanapita kwenye matawi yao wakidai kutakuwa na uchaguzi mpya.

Huku akijua jambo hilo halipo, hata kiongozi mkubwa kama Makamu wa Pili wa Rais naye anajiingiza katika mkumbo. Loo, Halbadir ya mbayana ikamkumba. Baada ya kusema asiloliamini katika mahojiano Jumatano, akalikana Alhamisi mchana aliposema, hakuna uchaguzi utaorejewa bali huo ni msimamo wa wa CCM, chama chao.

Yeye na wenzake wanajua hoja hiyo imeshindwa kwa sababu haina hoja. Si kisheria wala kimaadili. Ni hoja muflisi.

Wananchi wa Zanzibar wanasubiri akili zao CCM zirudi, waheshimu maamuzi ya wananchi. Waitoe tume ilikofichwa itangaze matokeo ya majimbo 23 na imtangaze rais mshindi.

Hakuna jingine, hakika CCM wanajifurahisha tu.

Chanzo: Mwanahalisi

 

One Reply to “Jecha ndio chanzo cha unyonge wetu”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s