Balozi Seif Ali Iddi ala matapishi yake

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya Habari kuhusu kurejewa kwa uchaguzi  Mkuu wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kurejewa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar

BALOZI Seif Ali Iddi, anayeng’an’ania kuwa bado ni Makamu wa Pili wa Rais, katika serikali ambayo uhalali wake kikatiba unatiliwa shaka, ametengua kauli yake mwenyewe aliyoitoa jana kwamba kuna makubaliano ya kurejewa uchaguzi Zanzibar.

Balozi Seif leo ameitisha timu ya waandishi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ofisini kwake Vuga, na kutamka kuwa hakuna makubaliano hayo katika majadiliano yanayofanywa na viongozi wa kisiasa kuhusu utatuzi wa mgogoro wa kisiasa.

“Sikupata kutoa taarifa ya majadiliano kwa chombo chochote cha habari… utaratibu wa kutoa taarifa za vikao vinavyofanyika utaandaliwa baada ya mazungumzo kukamilika,” amesikika akisema kupitia taarifa iliyosambazwa mitandaoni tangu mchana leo.

Katika taarifa hiyo ya picha na sauti pia, Balozi Seif anasema badala yake kwamba ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotamka kuwa kimeazimia kushiriki uchaguzi utakaorejewa kama ilivyotangaza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya kuufuta uchaguzi Oktoba 28.

Balozi Seif amesihi wananchi watulie na kusubiri mazungumzo yakamilike ambako muafaka utakuwa umefikiwa kuhusu masuala yanayojadiliwa ndipo taarifa ya makubaliano itatolewa kwa umma.

Majadiliano yamekuwa yakifanywa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Maalim Seif Shariff Hamad, na marais wastaafu Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi na Amani Abeid Karume, na hufanyikia Ikulu.

Hatua hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani kiongozi huyo asivyokuwa muadilifu hasa kwa kuwa amesikika waziwazi akisema kuna makubaliano yameshafikiwa ya kurejewa kwa uchaguzi isipokuwa tatizo linalobishaniwa ni tume ipi itasimamia uchaguzi huo utakapofanyika.

Isitoshe, katika mahojiano yake na muandishi wa Radio France International (RFI) aliyemfuata ofisini kwake, Balozi alijinasibu serikali ina uwezo wa kugharamia uchaguzi huo yenyewe, huku akisema ni yenyewe iligharamia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Inafahamika wazi kwamba sehemu kubwa ya fedha zilizogharamia uchaguzi mkuu Zanzibar zinazofikia Sh. Bilioni 8, zimetokana na msaada wa wafadhili, ufadhili uliosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Balozi Seif amedai katika mahojiano hayo kwamba uchaguzi utarudiwa kwa sababu uliharibika na kulaumu waangalizi wa uchaguzi kuwa hawakushughulika sana kufuatilia uchaguzi ulivyokwenda kisiwani Pemba, ambako yeye na wenzake katika CCM wanadai kulifanyika vitendo vingi vya udanganyifu.

Baada ya mahojiano aliyoyafanya na RFI – yaliyorushwa yakiwa ya muda wa dakika saba hivi – alihakikisha yanasambazwa kwenye vyombo vya habari na waandishi binafsi wa taasisi nyingi zilizoko jijini Dar es Salaam.

Mahojiano hayo yalipoenea Zanzibar, yalizusha fadhaa na kulazimisha uongozi wa juu wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoa taarifa maalum ya kumpinga kwa upotoshaji alioufanya.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa Ladhu amesema Balozi Seif amekuwa kiongozi mpotoshaji na asiyeaminika kwa namna yoyote ile hasa kwa kuwa amehusika katika kuifikisha Zanzibar ilipo.

Zanzibar imeingia kwenye mgogoro wa kisiasa kufuatia uamuzi wa kinyemela wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutangaza Oktoba 28, kuufuta uchaguzi kwa madai kuwa ulikumbwa na matatizo mengi.

Wakati huo Jecha mwenyewe alikuwa ameshatangaza matokeo ya urais zaidi ya asilimia 70 ambayo ni majimbo 31 kati ya 54 yote ya Zanzibar. Kadhalika Tume ilisharidhika uchaguzi ulikwenda vizuri kama zilivyobainisha ripoti za awali za asasi za waangalizi wa ndani na kimataifa.

Mazingira yanaonesha CCM baada ya kubaini imeshindwa uchaguzi na CUF, ilishinikiza kufutwa kwa uchaguzi wote.

Chanzo : Mwanahalisi

2 Replies to “Balozi Seif Ali Iddi ala matapishi yake”

  1. Bado kuna mvutano mkubwa huko Tanzania Bara ambapo ndipo MAAMUZI yote yanapotokea, ieleweke kwamba huko Zbar hawana serikali yyte ya kuweza kujiamulia mambo yao…Amri na Maamuzi yote hutoka Dodoma ..na hao viongozi waliopo huko zanzibar kawaida hufanywa ni mkokoteni wa kubebeshwa mzigo….Ikumbukwe kwamba Rais Kikwete ndiye alietoa maamuzi ya kufutwa uchaguzi zbar na yeye ndiye alietuma kikosi cha wanajeshi kama vile kuna hali ya hatari …..Kikwete amebaki nje ya “ring” lakini anajaribu kumtumilia Magufuli ili akamilishe yale mapendekezo yake..jambo ambalo halitakuwa rahisi kwa kiongozi huyo wa awamu ya 5 ambaye anaonesha hapendi tabia za ” mizengwe mizengwe” kama walivyozoea hao waliomtangulia .

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s