Marekani yamtikisa Magufuli

MCCSerikali ya Marekani imekunjua makucha kwa Tanzania kwa kuitaka kumaliza haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4), za awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la nchi hiyo.

Hatua hiyo inaonekana kuwa ni mtihani wa kwanza kwa Rais wa serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, ambaye tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka huu, anachapa kazi na matunda yake yanaonekana kwa umma wa Watanzania.

Kadhalika, Marekani imetaka kupata ufafanuzi wa watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Chanzo kimoja kimeieleza Nipashe hivi karibuni, kuwa kuna maelekezo ya kutoka MCC, ambayo huenda yakasababisha kufutwa kwa msaada huo, iwapo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hautatatuliwa kutotolewa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya mtandaoni kabla ya kikao cha Bodi ya MCC Disemba, mwaka huu.

“MCC inafuatilia kwa karibu hatua zitakazichukuliwa na serikali ya  Magufuli katika suala la utawala bora, katika kipindi hiki tunapokaribia kufanya kikao cha bodi ya MCC Disemba. Utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa kuridhisha pande zote zinazohusika,” kilieleza chanzo hicho.

Pia, MCC iliitaka serikali kutoa ufafanuzi juu ya sheria ya makosa ya mtandaoni (cyber –crime law) katika kipengele cha kuchapisha kanuni za utekelezaji zinazozingatia mchango wa wadau na kuendelea kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kulinda uhuru wa kujieleza.

Chanzo hicho kilieleza kuwa MCC imetaka ufafanuzi wa kina juu ya watu kadhaa walioshikiliwa na vyombo vya dola hivi karibuni kwa sheria ya makosa ya mtandaoni iliyoanza kutumika Septemba Mosi, mwaka huu.

“Kama mjuavyo, nchi zote zilizojiunga na MCC zinatarajiwa kuendeleza dhamira ya kuendeleza utawala bora, ambayo ni sehemu muhimu ya kanuni za demokrasia na kulinda uhuru wa kujieleza. Matukio ya hivi karibuni yameisababisha MCC na wadau wengine kujiuliza juu ya dhamira hiyo,” sehemu ya maelekezo hayo ilieleza.

MCC imeeleza kuwa mambo hayo mawili yataiwezesha MCC kuipima Tanzania katika sifa za kupata fedha hizo.

KAULI YA KATIBU MKUU HAZINA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alipoulizwa na Nipashe juu ya maelekezo hayo na kama wameanza kufanyia kazi, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa hajayaona.

“Hadi niione hiyo barua kutoka MCC ndipo nitaweza kuzungumza lolote, tunawasiliana nao kwa masuala mengi, hivyo ni vigumu kueleza kama kuna barua iliyoeleza masuala hayo au la,” alisema Dk. Likwelile.

Maelekezo hayo ya MCC yalisainiwa na Naibu Makamu wa Rais, Idara ya Operesheni Afrika, Jonathan Bloom, na Naibu Makamu wa Rais, Idara ya Sera na Tathmini, Thomas Kelly, kwenda kwa Dk. Likwelile.

Nakala ya maelekezo hayo yameelekezwa kwa Mratibu wa Kanda wa MCC, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, balozi za Tanzania nchini Marekani na wa Marekani nchini.

Fedha za MCC awamu ya pili ni kwa ajili ya kuiwezesha Tanzania kusambaza umeme na kuwaunganisha wananchi wengi katika Gridi ya Taifa na uimarishaji wa taasisi zinazohusika na na sekta ya nishati.

Septemba 26 mwaka huu, Tanzania ilitajwa kama nchi mojawapo iliyotimiza masharti yote ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka MCC, ambazo zilitolewa baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha chini ya mpango huo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, jijini Dar es Salaam, Septemba 26, mwaka huu, ilieleza kuwa Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana Hyde, alimueleza Rais Jakaya Kikwete, katika mkutano uliofanyika New York, Marekani, baada ya MCC kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa kukabiliana na rushwa.

Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.

MCC -1 Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (Sh. trilioni 1.46), Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka nchi hiyo katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani.

Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa  kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya mpango huo na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo imepata kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.

Mgogoro wa kisiasa uliibuka Zanzibar baada ya Oktoba 28, mwaka huu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kutangaza ghafla kufuta uchaguzi mkuu wa Rais na Wawakilishi uliofanyika Oktoba 25.

Jecha ambaye alitangaza uamuzi huo peke yake, alidai kuwa kulikuwapo na kasoro kadhaa katika majimbo ya Pemba, kinyume cha ripoti ya awali ya waangalizi wa kimataifa na wa ndani, ambao walisema ulikuwa mzuri kuliko wa mwaka 2010.

Tangazo la Jecha lilikosolewa na waangalizi hao na baadhi ya mataifa yakiwamo Ireland, Uingereza na Marekani, ambazo na kushauri mchakato wa utangazaji wa matokeo uendelee.

Maamuzi hayo yamesababisha mgawanyiko baina ya vyama vikuu vya siasa vya CCM na CUF. CCM inaunga mkono maamuzi ya Jecha ya kurudia uchaguzi huku CUF ikipinga, kwa maelezo kuwa mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, aniye aliyeshinda na kwamba atangazwe mshindi na kuapishwa.

Wakati Zec ikiendelea kutangaza matokeo oktoba 26, Maalim Seif aliibuka na kutangaza kwa alikuwa anaongoza kwa kupata kura zaidi ya asilimia 52 kisha kupeleka Zec fomu za matokeo kutoka vituoni kama ushahidi.

Kumekuwapo na jihihada binafsi za marais wastaafu kuwakutanisha Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Maalim Seif, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yaliyopatikana huku mazungumzo hayo yakifanyika kwa usiri mkubwa.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

One Reply to “Marekani yamtikisa Magufuli”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s