SMZ: Dk. Shein atahudhuria Bunge leo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema Rais Dk. Ali Mohammed Shein, ni Rais halali wa Zanzibar na atahudhuria ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma leo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, mjini hapa jana.

Alitoa kauli hiyo kufuatia msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuhoji uhalali wa Dk. Shein kuingia Bungeni wakati uchaguzi wa Zanzibar haujakamilika na kupatikana Rais wake.

Waziri Aboud alisema uchaguzi wa Zanzibar umefutwa na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu cha 28(1) Dk. Shein anaendelea kuwa Rais mpaka hapo Rais anayefuata atakapokula kiapo.

“Dk. Shein bado Rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba na atahudhuria uzinduzi wa Bunge kwa sababu Serikali ya Zanzibar ipo na inaendelea na shughuli zake,” alisisitiza Waziri Aboud, ambaye pia ni Msemaji  Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka huu, matokeo yote yamefutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) na kutangazwa katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu.

Waziri Aboud alisema taarifa zilizotolewa na Ukawa zimejaa upotoshaji hasa kwa kuzingatia hakuna uchaguzi uliyofanyika Zanzibar na kutangazwa mshindi na Zec.

Alisema SMZ imesikitishwa na kitendo cha Wabunge wa  Chama cha Wananchi (CUF) kumpinga Rais wa Zanzibar wakati wao ni sehemu ya Serikali ya pamoja kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

“Kitendo walichofanya kinaweza kurudisha matatizo ya nyuma ya kisiasa ya Zanzibar kinyume na malengo ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Waziri Aboud.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo baada ya kuwapo hali ya amani na utulivu mkubwa wa kisiasa kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Waziri Aboud alisema hakuna Rais Mteule Zanzibar baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kufutwa na Zec na kitendo cha Ukawa kumhusisha Maalim Seif na Urais, ni uvunjaji wa sheria za nchi.

Katika hatua nyingine, Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimesema  kitendo cha CUF kupinga Rais wa Zanzibar kuingia katika uzinduzi wa Bunge, hakileti mwelekeo mzuri katika mazungumzo ya kusaka muafaka wa ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ,Vuai Ali Vuai, alisema wabunge wa CUF wameshindwa kuheshimu na kuenzi malengo ya kuundwa kwa Serikali ya pamoja kutokana na kitendo hicho.

Alisema marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yalifanyika ili kumaliza siasa za chuki na uhasama na kufanikiwa kurudisha amani na Umoja wa Kitaifa.

Hata hivyo, alisema kitendo kilichofanywa dhidi ya Rais Dk. Shein na viongozi wa Ukawa, hakina manufaa kwa wananchi wa Zanzibar wakati huu Zanzibar ikiwa katika kutafuta muafaka wa uchaguzi.

Aidha, alisema Rais wa Zanzibar ni Rais halali kwa mujibu wa Katiba hadi Rais mpya atakapochaguliwa na wananchi na kuapishwa kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) cha Katiba ya Zanzibar.

Alisema hakuna mwananchi wa Zanzibar asiyefahamu kama uchaguzi unarudiwa baada ya Zec kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

chanzo: Nipashe

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s