Zitto: Mshindi wa urais Z’bar atangazwe bila kujali chama

Zitto KabweKiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amemtaka Rais, Dk. John Magufuli, kuhakikisha anamaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), inamtangaza mara moja mshindi katika uchaguzi huo bila kujali anatoka chama gani.

Zitto alitoa kauli hiyo alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema endapo wataona haiwezekani kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo, ni vema Rais akatangaza hali ya hatari na aunde serikali ya mpito ikiwamo kusitisha Katiba ya Zanzibar na kuunda nyingine.

“Katiba ya Zanzibar haina kipengele chochote kinachoiruhusu Zec kufuta uchaguzi wala Mwenyekiti wake, na wakati haya yote yanaendelea, hakuna minutes zozote ambazo zinaonyesha wapi walikaa kikao na kujadili kufuta uchaguzi huo, isipokuwa Mwenyekiti aliamua mwenyewe kufuta uchaguzi huo. Ni vema kura hizo zijumulishwe na mshindi atangazwe,” alisisitiza Zitto na kuongeza: –

“Suala hili lingekuwa la kwanza kuwekwa katika meza ya Rais Dk. Magufuli, kwa kuanza kulishughulikia kabla ya kufanya mambo mengine. Itakuwa kosa kubwa kufurahia rais kufanya ziara za kushtukiza katika maeneo mbalimbali wakati mgogoro wa Zanzibar bado haujapatiwa ufumbuzi, bila Zanzibar hakuna Tanzania.”

Zitto alisema kama Zec ilibaini kwamba tatizo lilifanyika katika majimbo, ilitakiwa kurejea katika majimbo husika kutatua tatizo hilo na si kufuta kabisa uchaguzi kama ilivyofanya.

“Mpaka sasa Zanzibar haina Rais, wala Serikali na hata huyo aliyopo, yupo kinyume cha Katiba na kuvunja Katiba ni kosa la kihaini ambalo anatakiwa kushtakiwa,” alisisitiza Zitto.

Hata hivyo, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa juhudi alizozichukua kuanza kushughulikia baadhi ya matatizo likiwamo kufuta safari za nje ambalo alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac), alilisimamia.

Zitto alisema pamoja na juhudi zake hizo za kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi za serikali, haziwezi kuzaa matunda pasipo kuweka mifumo mizuri ya kisheria ya kusimamia hayo.

Kwa msingi huo alimsahauri kuzifanya juhudi hizo  zitambulike kisheria ili hata Rais mwingine atakayefuata azitekeleze.

Kuhusu gharama za safari za nje, alisema Pac ilifanya ukaguzi maalum ambao ulishakamilika na muda mwafaka Watanzania watafahamu.

Zitto ambaye pia ni Mbunge Mteule wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), alisema akiingia Bungeni, atahakikisha analisimamia ili  taarifa inayohusu safari hizo, isomwe wazi na gharama halisi ya namna ambavyo safari hizo zimeigharimu serikali kwa kipindi chote cha uongozi wa awamu ya nne, ijulikane.

Kwa upande wake aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Anna Mghwira, alisema anaamini serikali ya Dk. Magufuli itazifanyia kazi sera za chama hicho ambazo alikabidhiwa ilani ya chama huku akipongeza kwa kuanza vizuri na  kutekeleza baadhi yake.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s