Uchaguzi wa Zanzibar sasa rasmi kurudiwa

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha akiwa na wajumbe wa tume hiyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha akiwa na wajumbe wa tume hiyo.

Wakati mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar yakiwa yamepamba moto, uamuzi wa kufutwa matokeo ya uchaguzi umetangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu, hivyo kumaanisha uchaguzi huo sasa ni rasmi utarudiwa.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, uamuzi huo umechapwa chini ya kifungu 119 (10) na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya Mwaka 1984.

Gazeti hilo pia limetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 3(1) na 5(a) vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Aidha gazeti hilo la serikali limeeleza kuwa, matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu yamefutwa kuanzia Oktoba 25, mwaka huu.

Kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Uchaguzi kinasema:  “Kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa, itajaaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria kama yametiwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi.”

“Mimi Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa vifungu vya 391) na 5 (a) vya Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, natangaza uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25, Oktoba,” gazeti hilo la serikali lilieleza.

Tangazo hilo kwenye Gazeti la Serikali  limetiwa saini na Mwenyekiti wa Zec Oktoba 28 mwaka huu na kwa msingi huo wananchi wa Zanzibar watatakiwa kuingia tena katika uchaguzi ndani ya siku 90.

Kabla ya kuchapwa kwa gazeti hilo, wajumbe saba wa Zec walikutana na kujadili kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu lakini kulitokea mvutano mkubwa kabla ya kuamuliwa kwa kutumia akidi ya wajumbe wengi waliounga mkono.

Katika kikao hicho, wajumbe wanne waliunga mkono uchaguzi kufutwa na wajumbe watatu walipinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, akiwamo Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Abdularhakim Issa Ameir.

Wajumbe wengine waliopinga matokeo kufutwa ni, Ayub Bakar (CUF) na Nassor Khamis (CUF) na wajumbe waliounga mkono walikua ni, Omar Ramadhan Mapuri (CCM), Salmin Senga (CCM) na Haji Ramadhan (SAU).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema baada ya tume kuchapa Gazeti la Serikali juu ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu, kinachosubiriwa ni tume kutangaza tarehe ya uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humo.

Alisema serikali itahakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa wakati kwa kuzingatia sheria na katiba ili wananchi wapate haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao kwa haki na utaratibu wa kidemokrasia.

Alisema serikali imeanza kujipanga katika matayarisho ya gharama za uchaguzi huo, ikiwamo utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi kabla ya kufanyika.

Hata hivyo, Kiongozi Mwandamizi wa Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Janeti Fussi, alisema umoja huo haukubaliani na uamuzi wa kurudiwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

“Tunamtaka Mwenyekiti wa Zec arudi kazini akamilishe uchaguzi wa Oktoba 25 na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo,” alisema Fussi ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kampeni wa Cuf, Ismail Jussa, alisema Mwenyekiti wa Zec katika Gazeti la Serikali ameshindwa kuonyesha kifungu cha katiba au sheria kinachompa uwezo wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu.

Alisema kifungu cha katiba namba 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar alichokitumia kinazungumzia kiwango cha mikutano ya tume na kila uamuzi lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi na siyo kufuta matokeo ya uchaguzi.

Alisema msimamo wa Cuf upo palepale Zec itengue uamuzi wa mwenyekiti wake warudi kazini kukamilisha utaratibu wa kuhakiki na kutangaza matokeo ya majimbo yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.

Gazeti la Serikali la kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu limetoka wakati viongozi wakuu wa Zanzibar wakiendelea na mazungumzo ya kusaka ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi huo, akiwamo Rais Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) na mgombea mwenzake kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anadai yeye ndiyo mshindi kabla ya matokeo kufutwa.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

5 Replies to “Uchaguzi wa Zanzibar sasa rasmi kurudiwa”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s