Mawaziri wa CUF wamsusia Dk. Shein

Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi CUF Taifa Bw. Twaha Taslima, akisoma maazimio ya baraza kuu kwa waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho Vuga mjini Zanzibar Picha: OMKR
Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi CUF Taifa Bw. Twaha Taslima, akisoma maazimio ya baraza kuu kwa waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho Vuga mjini Zanzibar
Picha: OMKR

Sakata la kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar limeendelea kuibua mtafaruku, baada ya mawaziri saba na manaibu wao wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kujiweka kando kutokana na kile wanachodai kuwa ni kuheshimu katiba.

Wanasema kuwa wamechukua hatua hiyo kutokana na muda wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kubaki madarakani kumalizika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Said Ali Mbarouk, ndiye aliyetoa taarifa hiyo wakati akitangaza msimamo wake na wa mawaziri wenzake kutoka CUF wa kujiondoa katika SUK kwa maelezo kuwa haina uhalali wa kikatiba kuendelea kuwapo kwani ilimaliza muda wake tangu Novemba 2, mwaka huu.

Alisema hawakubaliani na uamuzi wa kubaki madarakani kwa Dk. Shein na serikali yake yote, wakiwamo wao, na ndiyo maana wameamua kujiondoa, lengo likiwa ni kulinda Katiba ya Zanzibar inayotamka wazi kuwa muda wa rais kubaki madarakani ni miaka mitano sambamba na ilivyo kwa kipindi cha kuwapo madarakani kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao miongoni mwao huunda Baraza la Mawaziri.

“Siwezi kuvunja katiba kwa kutetea maslahi binafsi…  kwa mujibu wa katiba, mie si Waziri tena,” alisema Mbarouk.

Alisema mbali na yeye, mawaziri wenzake wote waliotokana na CUF kuunda SUK, walishaachia ngazi na kukabidhi ofisi na magari ya umma tangu Novemba 2, siku ambayo kikatiba ilikuwa ukomo wa serikali yao.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Aboubakar Khamis Bakari, alisema sababu ya yeye na mawaziri wenzake kutoka CUF kuachia ngazi kutokana na katiba kutowapa nafasi ya kubaki madarakani baada ya muda wao kumalizika kwa mujibu wa Katiba.

Bakari aliyeongoza timu ya wataalamu iliyoandika Katiba ya Zanzibar mwaka 1984, alisema muda wa uongozi wa Dk. Shein ulikoma Novemba 2, hivyo yeye na mawaziri wengine wote wa SUK hawastahili tena kuwapo madarakani.

Kama ilivyokuwa kwa Mbarouk, naye alitoa msimamo huo mbele ya waandishi wa habari wakati akitoa maelezo kuhusu maamuzi ya kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF mjini Zanzibar.

Abubakar alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 28(2) Serikali ya Dk. Shein imefikisha ukomo wa kuwapo madarakani.

Akieleza kuhusu wadhifa wake wa uwaziri, Bakari alisema yeye si waziri tena wa Katiba na Sheria na tayari amekabidhi ofisi na gari kwa sababu hayuko tayari kuvunja Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

“Rais kamaliza muda wake wa kubakia madarakani, na mie siyo Waziri tena wa Katiba na Sheria… gari na ofisi tayari nimekabidhi,” alisema Bakari.

Alisema hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi imeibua mgogoro mkubwa wa kikatiba Zanzibar.

Alisema wanaotafasiri kifungu cha 28(1) kuwa kinampa rais mamlaka ya kubakia madarakani, wajue wanapotosha kwa sababu Rais muda wake unamalizika ndani ya miaka mitano tangu tarehe ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

“Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa rais,” alisema, akinukuu kifungu cha 28(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar.

Bakari alisema kifungu cha 92(1)(2) cha katiba hiyo kinasema kuwa maisha ya Baraza la Wawakilishi yataendelea kwa miaka mitano tangu tarehe ile ulipoitishwa mkutano wake wa kwanza, baada ya kuundwa au limevunjwa mapema kabla ya muda wake.

Bakari ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza baada ya Zanzibar kupata katiba yake mpya tangu mwaka 1964, alisema wakati wowote ambao Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa iko kwenye vita, Baraza la Wawakilishi linaweza kuongezewa muda kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 92(1) kuhusu uhai wa Baraza hilo.

Alisema Baraza la Wawakilishi lilivunjwa Agosti 13, mwaka huu baada ya kumaliza muda wake na kwa mujibu wa Katiba, linatakiwa kuitishwa ndani ya siku 90 na kikao chake cha kwanza kitapaswa kuitishwa Novemba 12, mwaka huu.

Hata hivyo, alisema kutokana na Mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani, Baraza la Wawakilishi halitakuwapo Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Zanzibar.

KUHUSU MAALIM SEIF
Kuhusu Maalim Seif Sharif Hamad kuendelea kubakia na wadhifa wake wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima, alisema kama Rais Dk. Shein bado mgumu kuondoka, ndiyo maana na walio chini yake inakuwa vigumu vile vile kuondoka.

Alisema CUF wameamua kuitisha kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi ili kujadili hatua ya Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi cha Katiba na Sheria.

MAAMUZI YA BARAZA KUU
Taslima ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, alisema baada ya kujadili kwa kina suala hilo, Baraza Kuu la Uongozi limetoa mapendekezo, saba ikiwamo kuitaka Zec itengue uamuzi wa Jecha na kurudi kazini kukamilisha kazi ya kuhakiki matokeo ya uchaguzi ya majimbo 23 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar.

“Baraza kuu linasisitiza kwamba halitakubaliana kwa namna yoyote ile na hatua ya kufanya uchaguzi wa marudio ikizingatiwa uchaguzi ulishafanyika na kazi ya kuhesabu kura kumalizika,” alisema.

Maazimio mengine ni kuwa baada ya Zece kutangaza mshindi wa uchaguzi wa rais wa Zanzibar, Maalim Seif akutane na viongozi wa CCM na CUF vilivyopata wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujadiliana uundaji mpya wa SUK.

“Wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kuchukua hatua za kuona suala hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa haki unaozingatia matakwa ya katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984,” alisema Taslima, akinukuu mojawapo ya maazimio.

Pia, alisema Baraza Kuu linavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha nchi inadumu katika amani na utulivu kwa kuepuka kujiingiza katika vitendo vinavyoashiria vitisho na kuvunja haki za binadamu Zanzibar.

“Baraza kuu linamuomba Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za kuondoa vikosi na vifaa vizito vya kijeshi mitaani ili kuwajengea imani wananchi kuhusu usalama wao wakati wanasubiri suluhisho la amani la hali iliyojitokeza Zanzibar.

Aidha, alisema Baraza Kuu limewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu huku juhudi za kutafuta muafaka zikiendelea huku akisema mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni ya kutatua mgogoro huo hayajazaa matunda.

MAALIM SEIF
Akizungumza na watendaji na waliokuwa wagombea wakiwamo Wawakilishi, Madiwani na Wabunge wateule, mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif, alisema kama kuna watu wanasema amevunja sheria kwa kujitangaza waende mahakamani na yeye yupo tayari kujitetea.

Alisema alichotangaza yeye ni tathmini ya mwelekeo wa uchaguzi na kuwataka Zec kutangaza matokeo kama yalivyokuwa yakitokea baada ya kazi ya kuhesabu na kubandikwa katika majimbo kufanyika Unguja na Pemba.

Alisema msimamo wa CUF upo palepale, kwamba hakuna kurejewa uchaguzi na wamtaka Mwenyekiti wa Zec arudi kumalizia kazi ya kuhakiki matokeo ya majimbo yaliyobakia na kumtangaza mshindi.

MSEMAJI SERIKALI AKANA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alisema Ofisi yake bado haijapokea taarifa yoyote kuhusu mawaziri wa CUF kujiondoa SUK na kukabidhi ofisi na magari ya Serikali.

Alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ndiyo inayosimamia na kuratibu shughuli za serikali chini ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi  wa Zanzibar, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Alisema Serikali ya Awamu ya Saba bado haijamaliza ukomo wa kubakia madarakani na kwamba Rais Dk. Shein bado ni Rais kwa mujibu wa kifungu cha 28 (1) mpaka rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.

Alisema Serikali bado inamtambua Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kama ilivyo kwa Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamu wa Pili wa Rais.

“Kama wameamua kutoka katika serikali ya pamoja na watoke, lakini serikali ya Dk. Shein bado ipo hai na itaendelea kuwapo hadi atakapoapishwa rais mpya wa Zanzibar baada ya uchaguzi Mkuu,” alisema Waziri Aboud.

Alisema suala la kushiriki CUF uchaguzi wa marejeo ni hiyari yao kwani lililo muhimu ni kwa wananchi kupata haki yao ya kuchagua viongozi wa kuwaongoza kwa njia ya kidemokrasia baada ya uchaguzi wa awali kufutwa.

Alisema SMZ imeanza kujipanga kufanya matayarisho ya uchaguzi mkuu ikiwamo gharama na kinachosubiriwa sasa ni Zec kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Baraza la Mawaziri Zanzibar (BLM) lina Mawaziri 19 na Naibu Waziri saba, huku CUF ikiwa na mawaziri saba na manaibu wake watatu baada ya Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji, kujiuzulu wadhifa wake, baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 na ulifutwa na Jecha Oktoba 28 kwa maelezo ya kuwapo kwa kasoro kadhaa.

Hata hivyo, uamuzi wa Zec umekuwa ukipingwa na waangalizi mbalimbali wa uchaguzi wa kitaifa, kimataifa pamoja na mataifa kadhaa.

Chanzo: Nipashe

One Reply to “Mawaziri wa CUF wamsusia Dk. Shein”

  1. SMZ isifanye maigizo ktk jambo hili, kama wanataka aman ya kudumu wamtangaze mshindi, kama wanataka ubaguzi na uhasama wa kudumu wafanye uchaguzi mwingine. kama wanataka serikal isiyoheshimiwa na raia wafanye uchaguzi tena. kama wanataka wapate aibu wafanye uchaguzi. kama wanataka waichafue tanzania ktk mataifa mengine wafanye uchaguzi.kama wanataka rais asiekubalika na watu wafanye uchaguz mwingine. wanainchi wanasoma na kumjua mtetez wao kupitia kadhia hii. mnaweza kufanya uchaguzi na kupigiwa na watu 900 kati ya 100000. wakumbuke baada ya hapo kuna aibu kubwa sana. wazanzibar si wajinga kiasi hiko. si mfuasi wa cuf wala ccm sasa ukwel wameuona uko wapi. wafanye maigizo yao bila ya tafakuri ya kina. nchi hiz zinazoendelea ambazo hata gharama ya uchaguz zinahtaj kusaidiwa bado zinataka kurudia uchaguzi. lubuva aliwapotosha wa2 wasojua kiswahil na kuwambia kwamba tumeshawahi kufanya kitu kama hicho.jaman hivi hatuijui tofauti ya postpone na cancell? HASARA ZAKE NI KUBWA SANA ENDAPO WATAFANYA UCHAGUZI MWINGINE

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s