Wanasheria Zanzibar wataka Jecha achunguzwe

Viongozi wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, wakizungumza na waandishi wa habari
Viongozi wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, wakili Omar Said na Wakili Awadh; wakizungumza na waandishi wa habari

Sisi, Kama Chama Cha Wanasheria Zanzibar tumefadhaishwa na uamuzi huo hasa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Mwenyekiti huyo kisheria katika kufikia Uamuzi kama huo. Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama Mwenyekiti anao uwezo wa Kufuta matokeo ya Uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwakwaUchaguzi Nchi nzima.

Salma Said, Mwananchi

Zanzibar: Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimetaka kuundwe tume huru ya kumchunguza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Salim Jecha Salum na akithibitika kuwa ameshindikizwa afukuzwe kazi.

Wakizungumza na waandishi wa habari Rais wa chama hicho, Wakili Awadh Ali Said na Katibu Mkuu wake Omar Said Shaaban katika ukumbi wa watu wenye Ulemavu Kikwajuni wamesema tamko la Mwenyekiti halina nguvu kisheria na linaweza kuhatarisha Amani ya nchi.

“Rais aone haja ya kuunda Tume ya kumchunguza Mwenyekiti dhidi ya madai ya kushindwa kufanya kazi zake na ikiwa madai hayo yakithibitika, basi amuondoe mara moja”. Amesema katibu wa chama hicho, Omar Said Shaaban.

Oktoba 28, 2015 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jecha Salim Jecha kupitia vyombo vya Habari vya serikali alitoa tamko la kufutwa kwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Octoba 25 mwaka huu.

Pia wametaka zoezi hilo la uchaguzi kuendelea kutoka pale ilipoishia katika kazi ya kufanya majumuisho ya Kura za Urais ili mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 apatikane na kutangazwa kuwa Rais.

Aidha Chama hicho kimevitaka vyombo vya Dola kuchunguza na kuwakamata na hatimae kuwafikisha Mahakamani watu wote waliohusika kumshinikiza Mwenyekiti kutoa tamko la kufuta uchaguzi na matokeo yake.

Mbali ya hayo chama hicho kimetoa wito kwa Viongozi wote wa vyama vya siasa kujitathmini wajibu wao katika kuheshimu maamuzi ya wananchi yanayofanywa kwa njia ya demokrasia ili kujenga misingi mizuri ya utawala bora.

“Chama cha Wanasheria Zanzibar tunaamini kwamba Rais wetu wa Zanzibar atang’amua mtego huu unaokusudia kumuweka katika Historia ya Rais wa Zanzibar aliewahi kuvunja Katiba ya Nchi na kumuondolea rekodi nzuri aliyonayo ya kuheshimu sheria na Katiba ya Nchi na Utawala Bora” alisema Shaaban.

Kwa upande wake Rais wa chama hicho Awadh Ali Said alisema Chama Cha Wanasheria Zanzibar kimefadhaishwa na uamuzi huo hasa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Mwenyekiti huyo kisheria katika kufikia Uamuzi kama huo.

Alisema Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama Mwenyekiti anao uwezo wa Kufuta matokeo ya Uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwakwa Uchaguzi Nchi nzima.

Akitaja vifungu vya sheria Rais huyo alisema kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Tume ni Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wengine Sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume lazima yaungwe Mkono na wajumbe walio wengi lakini wajumbe wawili kutoka walitoka hadharani mbele ya waandishi na kusema hawajashirikishwa.

“Taarifa iliyotolewa na wajumbe wawili wa Tume Ndugu Nassor Khamis na Ndugu Ayoub Bakari kwa Waandishi wa Habari kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichokaa na kufikia maamuzi ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar kauli ambayo haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume, kinaleta taswira ya wazi kuwa Maamuzi hayo hayakuwa ya Tume bali ni ya Mtu mmoja ambaye ni Mwenyekiti, Hivyo kuyafanya kuwa ni Batili mbele ya macho ya Sheria” alisema Said.

Hata hivyo alisema katika kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyengine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya Uchaguzi au Uchaguzi wenyewe.

“Ni kwa bahati mbaya sana Mwenyekiti katika Tamko lake hakueleza kama utaratibu umefatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria” aliongeza Rais wa chama hicho.

“Kwa Mujibu wa Sheria Tume haina uwezo wala Mamlaka ya kufuta matokeo yaliyokwisha tangazwa na ambapo mgombea ameshapewa shahada ya kuchaguliwa”.

Rais huyo ambae ni wakili anasema wajibu wa Tume ni kuchapisha matokeo hayo kwenye gazeti la serikali kama kanuni ya 59 (4) na kifungu cha 88 (c) cha Sheria ya Uchaguzi vinavyoeleza na kama kuna Mgombea ambae hajaridhika na matokeo au maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi basi anatakiwa kwenda Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Uchaguzi na Ibara ya 72 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo ndio yenye Mamlaka ya kufuta uchaguzi na matokeo yake.

Akitaja athari ya tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar yanaweza kuiingiza Nchi katika mgogoro wa Mkubwa wa Kikatiba katika maeneo kadhaa kadhaa ambapo aliyataja kuwa ni muda wa kushika madaraka ya Urais kikatiba ambapo Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza wazi kuwa Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais.

Alisema tafsiri yake yake nikuwa tangu Rais wa Zanzibar alipokula kiapo cha uaminifu na Kiapo cha kuwa Rais siku ya Tarehe 3 Novemba, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano siku ya Tarehe 3 Novemba, 2015.

“Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya Urais zaidi ya Tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya Nchi. Upo mjadala katika jamii kuwa Rais anao uhalali wa kuendelea kuwa Rais chini ya Ibara ya 28 (1) (a). Maoni ya Chama cha Wanasheria Zanzibar ni kuwa maudhui ya Ibara hiyo ni kumpa uwezo wa Kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais mpya (anaefuata) tu na sio kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa Uchaguzi au kwa sababu ya Uchaguzi kufutwa”. Alisema Said.

Hata hivyo alisema nchi kuendeshwa bila ya Baraza la Wawakilishi ambapo katika mazingira yaliyopo ni wazi kuwa Nchi itaendeshwa muda mrefu bila ya kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa Serikali.

Alisema Katiba ya Zanzibar imeruhusu hali ya kuendesha Nchi bila ya Baraza la Wawakilishi kwa muda usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa.

“Kwa mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba zinaishia tarehe 12 Novemba, 2015 kwa kuwa Baraza la Wawakilishi lilivunjwa tarehe 13 Agosti, 2015. 3”. Alisema.

Akionesha khofu juu ya suala hilo alisema hatari ya kuwa na Rais ambaye yuko juu ya Sheria na Katiba ya Nchi,  Ibara ya 37 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaipa Mamlaka Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba.

Alisema katika mazingira yaliyopo hivi sasa ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015,  Baraza la Wawakilishi halitakuwepo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya Nchi na kukiuka Kiapo chake, hakutakuwa na Mamlaka nyengine yoyote yenye uwezo wa kuhoji matendo ya Rais.

Alisema hii inatoa fursa na inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na Dikteta.

soma tamk kamili hapa: –

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s