Anayoyasema Dk. Shein hamaanishi

Sheikh Mselem Bin Ali akiwa kwenye mahakamani ya Kisutu na wenzake hawapo pichani ambao wameshitakiwa kwa kosa la ugaidi
Sheikh Mselem Bin Ali akiwa kwenye mahakamani ya Kisutu na wenzake hawapo pichani ambao wameshitakiwa kwa kosa la ugaidi

 

UNAPOMSIKIA Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, anasihi wananchi waondoe hofu siku chache hizi za kuifikia Oktoba 25 watakapopiga kura ya kuchagua viongozi wao, harakaharaka utasema “Wazanzibari wanaye kiongozi makini.”

Anawapa uhakikisho wananchi wa Unguja na Pemba, maeneo ya mamlaka yake ya utawala kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwamba “uchaguzi ulio mbele yetu utakuwa huru na wa haki na hakutakuwa na fujo yoyote.”

Tena, anayasema hayo mbele ya viongozi wawili wakubwa; mmoja wa wasaidizi wake wakuu, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais, na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Kwa nafasi yake Dk. Shein, kawaida akihutubia popote pale, hata mkutano wa kisiasa, huwa anazungukwa na viongozi wakubwa wakiwemo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama – Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na Jeshi la Ulinzi.

Nasema usipojua kilichoko ndani ya fikra zake kiongozi huyu, kama ilivyo kwa viongozi wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), utajiridhisha kabisa kusema “Rais Shein anamaanisha.”

Nakwambia wala hamaanishi maana halisi ya anachokisema. Anatoa matamshi ya kuwaondoa hofu wananchi pale jukwaani, lakini kwingineko majukwaani, msaidizi wake huyo anayetoka naye CCM, anatishia amani ya mgombea mshindani wa Dk. Shein.

Balozi Iddi ameamua kuuthibitisha uongozi wa mkono wa chuma anavyoupenda, kwa kauli kali zinazoogofya kila anayezisikia. Anatisha khasa anaowalenga na hata wale wanaosikiliza ayasemayo.

Ofisini kwetu MwanaHALISI, mtaa wa Kasaba, Kinondoni, Dar es Salaam, mwandishi mmoja hata juzi wakati naandika makala hii, alinieleza kwa mara nyingine “sijakaa sawa tangu niliposikia yale maneno mazito ya kukirihisha ya Balozi.”

Ililetwa kanda kupitia mtandao wa kijamii ambayo Balozi anasikika akisema, “Uamsho waliobakia kama wanaweza wajaribu kuleta vurugu, watakiona cha mtema kuni… ona wenzao Uamsho wananyea ndooni kule Tanzania Bara.”

Msaidizi wa rais huyu haiwezekani msimamo huu ameubuni yeye binafsi. Siamini dhana hii. Ninaridhika kuamini ndio msimamo anaojua khasa kuwa ni wa Rais Dk. Shein – anauamini ni sahihi, anauchekelea na kuukumbatia.

Ijumaa kwenye viwanja vya Mnazimmoja, wakati alipopewa nafasi ya kuhutubia mkutano wa kampeni alioandaliwa Dk. John Magufuli kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kupata urais wa Jamhuri ya Muungano, Balozi Iddi alimuita majina mabaya Maalim Seif Shariff Hamad.

Huyu ni msaidizi mwenzake ambaye anagombea kwa mara nyingine kiti cha urais wa Zanzibar. Mafiga matatu hawa wamekuwa wakiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mtindo wa kuviziana kama paka na panya.

Kule kuongoza kwa staili hiyo kunazidi kuthibitisha kuwa mfumo wa serikali ya ushirikiano uliotarajiwa Dk. Shein auzamishe ngazi za chini, umeshindwa. Na hii itakuwa ni matokeo ya Dk. Shein mwenyewe, kukubalia wahafidhina wa chama chao CCM waliohakikisha haufanyi kazi kwa kuwa hauendani na maslahi yao.

Huku wakitamka wenyewe viongozi wa CCM kuwa waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi walioko Zanzibar walikuwepo mkutanoni wanashuhudia, Balozi akamuita Maalim “kichaa, mpumbavu, mwanamke asiyejielewa, fisadi, muongo, mnafiki.”

Haya yamesikika akiyapaisha huku mitambo ya vituo vya televisheni na radio ikiyarusha hewani moja kwa moja kutokea viwanjani. Maalim Seif labda ameyasikia kama nilivyoyasikia mimi kupitia mitambo.

Sijawahi hata mara moja kumsikia Maalim Seif akimuita majina mabaya ya aina hii msaidizi mwenzake huyo. Machi 29, mwaka huu, nilipata kumshuhudia Maalim Seif kwenye jukwaa la mkutano wa hadhara wa Makunduchi, Wilaya ya Kusini akimgusa Balozi Iddi kwa kusema, “mwambieni mimi nampenda sana.”

Sema labda Maalim Seif alimaanisha kinyume cha maneno hayo, lakini hata ingekuwa hivyo, bado alionesha kumheshimu kama kiongozi mwenzake. Hakuthubutu kumuita majina ya kumdhalilisha, ikiwemo kumtukana matusi ya nguoni, kwa sababu alitaka kuendelea kudhihirishia umma wa Wazanzibari kuwa yeye hiyo si hadhi yake kutukana au kudhalilisha watu. Hakuzoea.

Balozi yeye amejifunza na sasa ni championi wa hutuba zilizojaa maneno ya chuki, matusi, vitisho na kashfa nyepesi.

Sauti ya Balozi ni sauti khasa ya kuunyatia urais, mwanasiasa ambaye huo uwakilishi wa kiti cha Mahonda anaouwania akipita, makada wenyewe wa CCM wanasema, alishatanguliza hila.

Angalia mfungamano wa Balozi Iddi na Dk. Shein. Wiki iliyopita, akiwa kisiwani Pemba kwa mikutano ya kampeni, Dk. Shein alitoa kauli ya kumshangaa Maalim Seif, japo hakumtaja kwa jina, kwa alichosema, “kukamatwa kwa Masheikh wa Zanzibar na kupelekwa Tanzania Bara kushitakiwa.”

Anasema alikaa naye na viongozi wengine wa serikali, wakakubaliana njia ya kudhibiti fujo ambazo viongozi wa CCM wameaminisha dunia zimefanywa na Uamsho, ingawa kesi waliyowafungulia inawashinda kutoa ushahidi, iwe ni kuwakamata na kuwasafirisha Dar es Salaam, na kuwashitaki jinai ya ugaidi.

Hapa nathubutu kusema Dk. Shein hakusema ukweli kwa sababu hata kama walikutana, hakuna azimio hilo. Ninajua halipo popote.

Alichokifanya Dk. Shein ni kutafuta huruma ya wananchi ambao wana hasira za ajabu dhidi yake kwa kuruhusu Masheikh wa Zanzibar wakamatwe na kutungiwa kesi nzito, lakini ambayo haina ushahidi.

Dk. Shein amelewa madaraka. Anajiona hakuna wa kumgusa wala kumshughulisha, si kwa hili wala lile. Hwenda ameshajua atarudi kitini hata iweje. Ameakisi utawala mbaya sasa unamuandama kwa kulazimika kulaghai ili apate kuaminika.

Ni kweli hajali kitu kulaghai wananchi. Wakati anajua suala hili la masheikh kuendelea kusota gerezani pasina kuhukumiwa, linahojiwa kila aendako Mkoa wa Kaskazini Unguja na ndilo lililomfedhehesha msaidizi wake Balozi Iddi, alipokwenda kutaka radhi ya kugombea uwakilishi Mahonda, waliko vipenzi wa Sheikh Mselem Khamis Mselem, anayeheshimika na kuaminika kama mmoja wa masheikh waadilifu na weledi.

Dk. Shein anajua ameshindwa wajibu kuhusu suala hilo. Anajua amejitimba haaminiki tena. Na anajua atazikosa kura nyingi kwa hilo tu, achilia mbali yale yaliyozoeleka kuinyima kura CCM – Muungano unaoinyonga Zanzibar, uchumi duni, imani na ufisadi serikalini.

Chanzo: Mawio

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s