Viongozi wa CCM walipotiana Makonde

Wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar wakiwa katika kikao hapo Afisi Kuu ya chama hicho hapo Kisiwandui
Wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar wakiwa katika kikao hapo Afisi Kuu ya chama hicho hapo Kisiwandui

Ahmed Rajab
SINA dhamiri ya kutisha wala kuwatia watu hofu lakini kuna ile iitwayo “Kanuni” ya Murphy (Murphy’s Law) ambayo inanitisha. Kanuni hiyo, kwa hakika, si sheria wala si utaratibu. Ni methali au fumbo lisemalo kwamba kila kinachoweza kwenda kombo, kitakwenda kombo. Nachelea utabiri huo usije ukawa wa kweli katika huu Uchaguzi Mkuu unaotukabili.

Nalichelea hilo kwa sababu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo kuna mambo kadhaa yanayoweza kwenda kombo. Lililo kubwa miongoni mwayo ni amani. Ndio maana wenye kuona mbali haweshi kuwahimiza wadau wote wahakikishe kwamba amani na hali ya usalama itaendelea kudumu baada ya kumalizika mchakato wa uchaguzi.

Miongoni mwa wadau wakubwa wa uchaguzi huu ni vyombo vya usalama (jeshi na polisi), Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZE) pamoja na vyombo vya habari vya umma vya Shirika la Utangazaji la Tanzania (TB) na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC).
Taasisi zote hizo, pamoja na Mahakama, zinatakiwa ziendeshe shughuli zao zinazohusika na uchaguzi kwa njia za haki, bila ya upendeleo na bila ya serikali kuwatisha au kuwatia hofu wapigakura na wananchi, kwa jumla. Zisipofanya hivyo uchaguzi huu utakuwa na dosari na hali hiyo inaweza ikavunja amani.

Amani ni moja ya sababu kubwa zinazoufanya uchaguzi huu uwe si muhimu kwa Tanzania tu, ambako wengi wanautegemea kwa mengi, lakini uwe muhimu pia kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hata nje ya mipaka ya eneo hilo.

Kwa muda mrefu, taifa hili limekuwa likijinata kwamba ni la aina ya pekee katika sehemu hii ya Afrika kwa kuwa limeepukana na majanga mengi yaliyovunja amani katika takriban nchi zote zilizo jirani nalo.
Hadi sasa Tanzania imekuwa mfano wa kisiwa cha amani katika bahari iliyochafuka, licha ya ghasia na mauaji yaliyotokea Zanzibar wakati wa Mapinduzi ya Januari 1964 na katika chaguzi zilizopita. Hofu iliyopo ni kwamba safari hii ghasia na machafuko yanaweza yakaikumba na Bara.
Dalili ziko wazi. Siku mbili hizi wakazi wa Bara nao wamekuwa wakiionja shubiri ya vyombo vya dola kama walivyozoea wenzao wa Zanzibar.

Wananchi wameingiwa na woga kuwaona wanajeshi waliovaa sare wakiwa wanafanya mazoezi karibu na makazi yao.

Kwa Zanzibar hayo si mageni. Licha ya kutahadharishwa, mara kwa mara, kwamba wayafanyayo hayaashirii mema na huenda yakachangia katika uvunjwaji wa amani katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi, bado wakuu wa jeshi na polisi wanaendelea kujifanya kama wana masikio mafu.
Kwa mintarafu ya hayo, tamko lililotolewa Jumamosi iliyopita na Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia (AZAKI) limetolewa wakati ndio. Tamko hilo limevitaka vyombo vya dola viache kutumia vitisho, nguvu na silaha za kivita katika kipindi hiki kinachokaribia siku ya uchaguzi.
Kwa upande wa Zanzibar kuna hofu kubwa ya kuzuka fujo. Aidha, kuna tetesi kwamba njama zinaandaliwa za kuhesabu kura za urais wa Zanzibar kisiri siri. Tetesi hizi zimevuja kutoka vikao vya ndani vya Chama Cha Mapinduzi (CCM-Zanzibar) ingawa mawakala wa chama hicho wameambiwa katika mikutano yao kwamba kura zote zitahesabiwa pamoja katika kila kituo cha kupigia kura.

Wasiwasi uliopo unatokana na yanayosemwa faraghani na baadhi ya viongozi wa CCM-Zanzibar kwamba wataingia wenyewe kuhesabu kura za urais na, kwa hivyo, watahakikisha kwamba angalau ushindi wa urais utakuwa wao.
Inawezekana kwamba hao wakuu wa CCM-Zanzibar wanajaribu kutiana moyo kwa vile wanaona mambo yamewakalia vibaya. Si siri tena kwamba hawaaminiani na wanatuhumiana kwa usaliti.
Kwa mujibu wa habari tunazopashwa na wanaohudhuria vikao vya ndani vya CCM-Zanzibar, woga umewavaa. Kila mmoja anaogopa asije akatuhumiwa kuwa ni msaliti.

Matokeo ni kwamba siku hizi baadhi yao wanaogopa kuhudhuria vikao hivyo wasije wakarushiwa shutuma hizo.
Shutuma zenyewe ni kwamba baadhi ya wakereketwa wanajiita CCM mchana lakini usiku wanageuka na wanakuwa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) au wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kwa muda mrefu, lawama hizi zilikuwa zikifichwa na zikitolewa chini kwa chini lakini zilichomoza hadharani mwanzoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano uliofanywa Mwera na uliohudhuriwa na wahusika wa kampeni ya uchaguzi ya Wilaya ya Mjini Magharibi.
Mmoja wa viongozi waliohudhuria mkutano huo alikuwa Waziri wa Fedha, Omar Yusuf Mzee.
Yaliyojiri hayasemeki. Yaliporomoka matusi na halafu wajumbe wakaanza kutiana makonde. Sokomoko lilianza baadhi ya wajumbe walipowatuhumu wenzao ambao hawakuhudhuria mkutano kuwa ni wasaliti. Waliotiana ngumi walikuwa makatibu wawili wa majimboni. Mmoja akiwafichua “wasaliti” na mwengine akiwahami.

Katibu Amour Idi, anayesifika kwa upole na ustaarabu wake, aliwahami walioshutumiwa akisema kwamba yeye haziamini shutuma hizo.

Kuna waliomhamakia kwa matamshi yake na mmoja wao akamvamia na kumpiga ngumi. Isitoshe, wakaanza kumtuhumu kuwa naye pia ni msaliti na kwamba yeye na hao aliowatetea “wamenunuliwa” na kina Mansour Yusuf Himidi, aliyefukuzwa  CCM na ambaye sasa ni mgombea wa uwakilishi kwa niaba ya CUF.
Kadhalika, wajumbe wa mkutano huo wa Mwera walilaumiana kuhusu uchapakazi. Kwa hakika, katika mikutano yao ya siri viongozi wa CCM-Zanzibar wamekuwa wakilaumiana sana kuhusu suala hilo na wakiwalaumu zaidi wale wagombea wao wa uchaguzi ambao ama hawayapitii majimbo yao au wakiyapitia basi huwa wanawatukana wapigakura.

Hali hiyo inaashiria kuwa ama wagombea hao wanajiamini bila ya kiasi kwamba watashinda au wamekwishasalim amri kwamba watashindwa.

Wenye busara miongoni mwao wanawalaumu wenzao wenye kupita wakiwatukana na kuwatisha watu pamoja na kuwakashifu wapinzani.
Hivyo vitisho vinawafanya wakazi wa Zanzibar waamini kwamba pana njama zinazopikwa na wanaoshikilia mpini za kuanzisha fujo ili waweze kudhibiti mambo ambayo kwa sasa yanawaendea kombo.

Baadhi ya wakazi hao wameingiwa na hofu kiasi cha kuwafanya waanze kuweka akiba ya chakula, mafuta ya taa na kila wakiwezacho kukiweka akiba.
Hii hofu ya kuzushwa fujo kwa kusudi iligusiwa kwa hasira na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, alipouhutubia mkutano wa kampeni yake ya kuwania urais wa Zanzibar huko Fumba, Unguja.

Alidai kwamba masanduku yaliyokuwa na sare za CCM yalionekana gatini Pemba. Kwa bahati, moja lilianguka na zikatokeza sare za CUF. Tuhuma zake ni kuwa CCM inajiandaa kuanzisha fujo, lawama watupiwe CUF ili uchaguzi uahirishwe.

Jumapili asubuhi wakereketwa wa CCM wenye kuaminika waliitwa kuonana na Rais Ali Mohamed Shein katika mkutano wa dharura uliofanywa katika tawi la Amani.

Kwa mujibu wa mpashaji habari wetu, Shein alizungumzia historia ya Zanzibar, kwa mtizamo wake, na namna chama cha zamani cha Afro-Shirazi Party (ASP) kilivyokuwa kikionewa katika chaguzi za kabla ya Mapinduzi.

Inavyoonesha ni kwamba ama akiwatayarisha wakereketwa wa CCM kwa matokeo ya kura yatavyokuwa au akitaka kuwatia moyo wayasambaze aliyokuwa akiyasema. Bahati mbaya, tunasikia kwamba hakuwa na jipya la kueleza. Badala ya kuwafunza historia sahihi, ikiwa mbaya au nzuri, aliwapoteza na kuwatia punju.

Wote walioalikwa, na tunasikia hawakuwa wengi, walikuwa na umri usoipindukia miaka 50. Kwa hivyo, si ajabu kwamba kuna miongoni mwao walioamini walioambiwa kwa sababu hawaujui ukweli. Swali ni kuwa wanaowadanganya watawadaganya mpaka lini?
Kuna tofauti moja kubwa baina ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na chaguzi zilizopita. Safari hii kila mgombea wa uchaguzi, toka wa urais, hadi wa Bunge, wa Baraza la Wawakilishi (Zanzibar) na wa udiwani amekuwa akiahidi mengi. Kila mmoja anamshinda mwenzake; baadhi ya ahadi zao ni porojo zisizo na msingi; nyingine ni za kuwapumbaza walalahoi.
Lakini zipo ahadi walizozitoa baadhi yao zinazoingia akilini, zikifanyiwa kazi kikweli zinaweza zikatekelezeka. Mfano ni ile ahadi ya Maalim Seif aliyewaahidi Wazanzibari kwamba endapo watamchagua Rais ataigeuza Zanzibar iwe “Singapore” ya Afrika Mashariki. Niliizungumzia ahadi hiyo wiki chache zilizopita (“Maalim Seif na mikoba ya Lee Kuan Yew”, Raia Mwema, Toleo la423).

Jumamosi iliyopita kwa kutumia filamu “Ajenda ya CUF kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore” Maalim Seif aliizindua ajenda hiyo na kutoa maelezo zaidi juu ya hatua gani atazochukuwa kutimiza lengo hilo.
Kuna kuigizana. John Magufuli naye, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akaona si vibaya kumuiga Maalim Seif. Wiki iliyopita aliwaahidi wananchi wa Mwanza kwamba akichaguliwa Rais atalifanya jiji hilo liwe “Geneva ya Afrika”.

Geneva ni mji mkuu wa Uswisi na linatajika kwa biashara hasa za saa za bei ghali, dawa na kampuni zenye kufanya utafiti wa kemikali.

Magufuli alisema kwamba Mwanza ni jiji la uchumi kutokana jiografia yake lakini bado hakutoa maelezo ya hatua gani anazokusudia kuchukua kuligeuza Jiji la Mwanza ili liwe kama lile la Geneva.
ukijaaliwa tukakutana tena tutakuwa tushazijuwa mbivu na mbichi: nani washindi na nani walioshindwa. Tunachokiomba ni kwamba paweko amani na usalama kuanzia sasa, wakati wa upigaji kura na baada ya kutangazwa matokeo.

Chanzo: Rais Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s