Kama mzee Moyo, ameyaona Kingunge

Mzee Kingunge sasa amehama Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa na maana kadi yake ya uanachama ambayo ni Na.08, inabaki ya maonesho tu.
Mzee Kingunge sasa amehama Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa na maana kadi yake ya uanachama ambayo ni Na.08, inabaki ya maonesho tu.

Na Jabir Idrissa

NANI katika CCM waliopo sasa, akiwemo Mwenyekiti wao Jakaya Mrisho Kikwete, makamu Philip Mangula na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, anayekijua kwa ufasaha chama hiki – asili yake, itikadi yake, sera yake, malengo yake – kama ajuavyo huyu mzee Kingunge Ngombale-Mwiru?

Jibu rahisi ni hakuna kama yeye. Kingunge sasa amehama Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwa na maana kadi yake ya uanachama ambayo ni Na.08, inabaki ya maonesho tu.

Kingunge ametanguliwa katika uanachama na mwanasiasa mwingine mkongwe nchini, Hassan Nassor Moyo, ambaye tofauti naye aliyejiondoa mwenyewe, yeye alifukuzwa uanachama kwa tuhuma za usaliti.

Kama mzee Moyo, Kingunge naye amesema hatajiunga na chama kingine baada ya kuhama chama alichoshiriki kukianzisha, kukijenga na kukilea au kukiendeleza.

Wote hawa, mzee Moyo na Kingunge, wameahidi kubaki wananchi wa kutoa mawazo kwa Watanzania kuhusu kuiendeleza nchi katika mwelekeo unaotoa matumaini ya kusonga mbele.

Wanasiasa watu wazima wastaafu hawa ambao binafsi ninawaheshimu isivyo kawaida, wameamua kubakia na amani na kusaidia kuelimisha wanaowaheshimu kuhusu historia ya mapambano ya kuikomboa nchi kiutawala lakini na malengo ya kufanya hivyo.

Mzee Moyo alifukuzwa uanachama na ngazi ya mkoa katika kikao ambacho kilijaa wanasiasa chipukizi baadhi wakiwa hawajui hata chembe ya historia yake kisiasa na kiharakati. Si hasha basi alidharau aliposikia taarifa za kuvuliwa uanachama.

“Hawajui watendalo hao vijana. Hivi yupo anayejua nani alinikabidhi kadi yangu Na.08, hakuna maana hata mwenyekiti wao hajui,” alisema akijenga hoja kuwa yeye si mwanachama wa kuchezewa kwa kuwa anakijua chama nje ndani.

Kauli kama hiyo imetolewa na Kingunge, ambaye ni mmoja wa makada waliokuwa karibu mno na Mwalimu Julius Nyerere wakati CCM ikizaliwa baada ya uamuzi wa kuunganisha vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanganyika, na Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar mwaka 1977 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Wakati Kingunge analalamikia mwenendo mbaya wa chama kwa kuwa viongozi wake wakuu wanakiendesha bila ya kuzingatia katiba na makusudi ya kuanzishwa kwake, Moyo analalamikia ukaidi wa viongozi wa Zanzibar kujali haki ya Zanzibar katika muungano wake na Tanganyika.

Kwamba anakiri wao wakati ule wa kuiunganisha mamlaka ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Tanganyika, walikosea kutosimamia ipasavyo, kasoro iliyochangiwa pia na ubeberu wa kuundwa kwa muungano wenyewe.

Sasa anaiona fursa ya viongozi kurekebisha kasoro ile kwa kusimamia msingi wa kurudisha mamlaka ya Zanzibar yaliyomeng’enywa kutokana na sera zinazosimamiwa na Serikali ya Muungano (SMT).

Anajikuta hana wa kubadilishana naye mawazo hayo, badala yake anashuhudia viongozi waliopo wanahangaikia maslahi binafsi na walio karibu nao; hayo yenyewe yakiwa sio hasa malengo ya mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Tanganyika.

Mzee Moyo amesema wazi kwamba amekosa kuungwa mkono na viongozi wa ngazi ya juu wa CCM Zanzibar katika dhamira yake ya kusimamia msukumo wa kuiwezesha Zanzibar kurudisha mamlaka yake kamili ya kujiendesha pasina kutegemea mkono wa Serikali ya Muungano.

Tatizo alolipata mzee Moyo ni kwamba wenzake katika CCM wana mtazamo kwamba kutekeleza mpango huo wa kurudisha mamlaka ya Zanzibar ni kuunga mkono sera ya chama hasimu wao kisiasa – Chama cha Wananchi (CUF) – ambacho kimekuwa kikishikilia imani hiyo kwa miaka yake yote ya uhai tangu 1992.

Kwa CCM, kufanya jambo au kuchukua hatua yoyote itakayokiweka katika kuonekana kimeridhia yanayotakiwa na CUF, ni kukubali kujimaliza kisiasa hasa kwa kuwa sera zinazoibana Zanzibar ndani ya mfumo wa Muungano wa serikali mbili, ndizo zinazowapandisha nyadhifa viongozi hao.

Na hilo linakuwa uthibitisho wa dhahiri kwamba Muungano upo zaidi kimaslahi ya viongozi wakuu na wasaidizi wao katika CCM badala ya kile kilichodhamiriwa uwanufaishe watu wa nchi mbili zilizounganishwa.

Kwamba ingawa Muungano ulikuwa na malengo ya kisiasa, kupata taifa lenye nguvu zaidi ndani ya Afrika Mashariki, kumbe kwao CCM, muungano huo ni njia ya kupitia kutimiza malengo ya kugawana vyeo ambavyo kwa mfumo uliopo, inahitaji kuimarishwa kwa mfungamano wa mifumo ya kikazi inayolindwa na CCM.

Ama kwa hakika, kukacha kwa viongozi wa chama hicho Zanzibar kuukubali ukweli wa mambo kama anavyouona na kuuamini mzee Moyo, ndiko hasa kumekisababishia chama hicho upinzani usioshindikana kwa hoja jadidi, sio tu unapokaribia uchaguzi mkuu, bali pia katika wakati wote wa maisha ya kisiasa nchini.

Ndio maana wakati suala la mahitaji ya kupatikana mabadiliko ya mfumo uliopo wa Muungano wa serikali mbili, ili kupisha mfumo wa serikali tatu unaotoa fursa kwa Zanzibar kukaa meza moja na Tanganyika wakiwa washirika sawa, likipiganiwa, CCM inajikuta ikizidi kuchukiza kwa umma wa Wazanzibari.

Wazanzibari walio wengi wanaamini kwamba dhamira ya viongozi wa CUF ndio inayowapa matumaini kuwa                                           mfungamano wa kimuungano unaweza kupatiwa ufumbuzi ila ni kwa njia moja tu ya majadiliano ya serikali zilizopo ambayo lazima yafanyike chini ya msingi wa kuheshimiana na kuaminiana.

Mabadiliko yanayofikiriwa na CCM siku zote yamekuwa ya kuiweka Zanzibar kama kaka mdogo anayepaswa kusikiliza na kupokea chochote anachotunukiwa na kaka mkubwa ambaye ndiye Serikali ya Muungano inayohifadhi maslahi makubwa ya Tanganyika.

Viongozi wa CCM kwa kuwa shida yao ni kukamata madaraka kwa namna yoyote ile, wala hawajali kuwa maridhiano katika suala hilo ndio njia inayofaa kwa manufaa ya amani ya kweli na mshikamano wa wananchi. Hawajali na ndio maana wamo kupanga ushindi wa tsunami lije jua au mvua.

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s