‘CCM imechochea Wazanzibari kuchoka’

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali Abdulrahman Omar Kinana
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali Abdulrahman Omar Kinana

Wazanzibari wanachochewa kuchoka

TAYARI Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali Abdulrahman Omar Kinana, amejibiwa kwamba kile anachokisukuma kiaminike na ulimwengu, hakina maana yoyote hasa kwa kuwa hakiendani na uhalisia wa suala lenyewe.

Kanali Kinana ameambiwa alichokisema ni upotoshaji usiokuwa na msingi isipokuwa “siasa za kilaghai” za kutafuta huruma ya Wazungu ili waridhie jitihada hasi za chama chao za kutaka kubakia madarakani hata kwa njia za hila.

Anaposema kuruhusu muungano wa upinzani wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vinne kushika utawala wa dola Tanzania kutatoa mwanya wa kushamiri kwa Waislam wenye itikadi kali na hivyo kukaribisha magaidi, anajidhalilisha tu.

UKAWA unaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) ambavyo vimemteua Edward Lowassa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa wafadhili hasa Marekani na Uingereza masuala hayo wanayajua vilivyo katika msimamo kwamba iwapo CCM na serikali zimeamua kuwachimba mkwara Waislam wa Zanzibar na Tanganyika, ni matunda ya sera ya kuwagawa Waislam kwa ujumla wao wakati Uislam umekuwepo Tanzania, Afrika Mashariki na vitongoji vyake kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi kwa karne kadhaa.

Mtendaji huyu wa CCM anapodai kuwa Uamsho ni kundi linalofungamana na Boko Haram na ndilo lililohusika na kuchomwa makanisa na kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini, anajitahidi tu kujenga msingi wa kuwazuia Waislam kushiriki kikamilifu katika maisha ya siasa.

Anaambiwa Uamsho ni kundi la Wazanzibari halisa wanaotumia haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni na kujenga msimamo katika mwelekeo mpya unaobeba matumaini ya Wazanzibari wanaotaka mamlaka zaidi ya serikali yao.

Anapaswa ukweli kuwa kushamiri kwa harakati za Uamsho ni matokeo ya mfumo wa ukandamizaji wa haki za kisiasa unaokuzwa na serikali ya CCM dhidi ya CUF ambacho pia huitwa Civic United Front.

Tena anaambiwa CUF ni chama imara cha siasa kilichoanzishwa na wasomi pamoja na watetezi wa haki za binadamu kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kwa lengo la kusaidia kuharakisha maendeleo ya taifa.

Kwa hivyo basi, yeye Kanali Kinana na sasa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM) wanajifedhehesha kujenga hoja kwa kutumia propaganda nyepesi.

Kilichopo Zanzibar kwa sasa, anasema Nathalie Arnold Koenings, mama wa Kimarekani aliyebobea fani ya mambo ya kale, mwandishi wa vitabu na mfasiri wa lugha ya Kiswahili, ni Wazanzibari kuchoka kuwekewa vikwazo kwa zaidi ya miaka 20 vya kushiriki demokrasia.

Sasa wakati hiyo ndiyo tathmini ya mtaalamu wa Marekani, anajitokeza Balozi Seif Ali Iddi akitamka kuwa kukamatwa kwa masheikh wa Uamsho na kupelekwa Tanzania Bara ambako anasema “wananyea ndooni,” ni uthibitisho kuwa dola haichezewi bali mtu akitaka achezee ndevu.

Maneno hayo ameyakopa kwa Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma ambaye wanamaskani wa CCM wakimuita Komandoo. Ilikuwa ni kauli ya kuonesha jinsi utawala wake ulivyokuwa wa mkono wa chuma dhidi ya wafuasi wa CUF.

Chini ya uongozi wa Dk. Salmin, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilipora ushindi katika uchaguzi mkuu wa 1995 na hata aliposhauriwa na Mwalimu Julius Nyerere aunde serikali kwa kujumuisha wawakilishi wa CUF, alikataa akisema, “mfumo tulionao ni wa chama kinachoshinda kinaunda serikali peke yake.”

Dk. Salmin alitangazwa mshindi wa asilimia 50.2 dhidi ya 49.8 alizopata Maalim Seif Shariff Hamad, na akatamba kuwa “ushindi ni ushindi tu hata ukiwa wa goli moja.”

Utawala wake ukatengwa na jumuiya ya kimataifa kwani viongozi wa CUF walifanikiwa kujenga ushawishi kuwa waliporwa ushindi na Zanzibar ikanyimwa misaada. Matokeo yake, viongozi wengi wa CUF walikamatwa mwaka 1997 na wakafunguliwa kesi ya uhaini ambayo hata hivyo haikuthibiti na wakaja kuachiwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliyosema hawakuwa na kesi kwa kuwa uhaini hauwezi kutendeka Zanzibar kusikokuwa na dola inayojitegemea.

Viongozi wa CUF wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mstaafu Machano Khamis Ali, walipata manufaa hayo baada ya kukata rufaa wakishikilia kuwa mashitaka yao hayakuwa na uhalali kwa kuwa SMZ haiwezi kutendewa uhaini.

Kwa hatua nyingine, baada ya kukaa gerezani kwa miaka mitatu, serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wake, Idi Pandu Hassan, ambaye sasa ni marehemu, iliondoa shauri hilo kwa kusema haina maslahi nalo tena.

Balozi Seif anapoyarudia maneno yale ya Dk. Salmin tena kwa kauli nzito ya maonyo kama “Ole wao watuletee vurugu, fujo, watuletee uvunjifu wa amani, wasisahau vyomb ovya dola vipo vitawashughulikia.

“Uamsho wako wapi sasa hivi, kama wanaweza wajaribu tena… wenzao sasa wapo Bara wananyea ndooni na wale wengine wakituletea fujo na kutuvunjia amani ya nchi hii watakiona cha mtema kuni,” anathibitisha kuwa serikali haifuati utawala wa sheria.

Balozi Seif anasema akiwahimiza vijana wa CCM kuwa wasilale “bado mapambano” kwamba dola haichezewi bora wachezee ndevu.

Kiongozi huyo anatajwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kueneza hutuba za chuki na vitisho dhidi ya viongozi wa CUF, ambao wenyewe wanalalamika kuhujumiwa kampeni zao kwa kuingiliwa mikutano yao na makada wa CCM wakilindwa na Jeshi la Polisi.

Mwenendo huo ndio unazidi kuthibitisha walichokisema masheikh wenyewe kuwa kesi yao ni ya kisiasa wala haihusu wao kutuhumiwa kutenda ugaidi.

Chanzo: Mawio

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s