Mambo saba ni maangamizi kwa Zanzibar

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
Othman Masoud Othman aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amebainisha mambo saba yaliyopo kwenye Katiba Pendekezwa ambayo anasema yataiangamiza Zanzibar endapo Katiba hiyo itapitishwa.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amebainisha mambo saba yaliyopo kwenye Katiba Pendekezwa ambayo anasema yataiangamiza Zanzibar endapo Katiba hiyo itapitishwa.

Othmani alivuliwa wadhifa wake kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar baada ya kuweka msimamo wake kupinga baadhi ya vifungu vya Rasimu ya Katiba wakati wa upigaji kura uliofanyika mapema mwaka huu.

Akizungumza jana kwenye kongamano lililoandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), mjini Unguja, Othman alisema Katiba iliyopendekeza imechukua mamlaka yote ya Zanzibar kama nchi mshirika wa Muungano na kuufanya kuwa chini ya uangalizi wa Serikali ya muungano.

Alisema Zanzibar kama nchi mshirika wa muungano sharti apewe nguvu ya kikatiba ya kufanya maamuzi katika mambo yote ya muungano. Alisema Zanzibar ilitoa mamlaka yake ili ishirikiane na Tanganyika katika kujenga umoja na siyo kuwa chini ya Tanganyika.

“Tulikwenda kwenye Bunge Maalumu la Katiba tukifahamu matatizo na kilio cha muda mrefu cha Wazanzibar, lakini baadhi ya wenzetu wakaungana na wengine kupitisha katiba ambayo haijazingatia maslahi yetu,” alisema Othman.

Alisisitiza kuwa ibara ya 6 (2) ya Katiba ya Zanzibar imebainisha kuwa kila Mzanzibar ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa watu wa Zanzibar. Alisema Kifungu hicho cha Katiba kimekiukwa na watu wenye dhamana ya kuetetea maslahi ya nchi yao.

Othman alifafanua kwamba ni jambo gumu kuondoa kabisa mamlaka ya nchi iliyokuwa dola kamili na kuifanya kuwa chini ya dola nyingine ambayo ilikuwa na hadhi hiyo. Alisisitiza kuwa Katiba Pendekezwa imeondoa kabisa nguvu ya Zanzibar kama nchi mshirika.

Mambo saba

Othman alibainisha mambo saba ambayo alisema endapo Katiba Pendekezwa itapitishwa basi nchi ya Zanzibar itatoweka kabisa na kubaki kama manispaa. Alianza kwa kutaja mamlaka ya Rais.

Alisema ibara ya 2(2) cha Katiba Pendekezwa imempa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na sehemu nyingine, jambo ambalo anasema linaingilia mamlaka ya Rais wa Zanzibar.

“Katiba hiyo haijamlazimisha Rais wa Muungano kufuata ushauri wa Rais wa Zanzibar. Kwa hiyo, inawezekana Rais wa Serikali ya Muungano akaamua mambo yake bila kumshirikisha Rais wa Zanzibar, sasa ushirika wa Zanzibar uko wapi ndani huo muungano?” alihoji.

Mwanasheria huyo alitaja jambo jingine kuwa ni ukuu wa Katiba. Alisema Katiba inayopendekezwa imeipa nguvu zaidi katiba ya Jamhuri ya Muungano bila kutambua uwepo wa Katiba ya Zanzibar.

Alisema Katiba hiyo inasema sheria yoyote inayokwenda kinyume na katiba hiyo ni batili. Aliongeza kuwa hata baadhi ya vifungu vya katiba ya Zanzibar vinavyokinzana na Katiba Pendekezwa navyo ni batili.

“Nilihoji kama sheria inayokinzana na katiba hiyo ni batili, vipi kwa Katika ya Zanzibar, nikajibiwa nayo ni batili. Nikahoji tena kwani Katiba ya Zanzibar nayo ni sheria kama nyingine! Lazima kuwe na uhusiano kati ya katiba hizi mbili,” alisema.

Mfumo wa Serikali mbili ni jambo jingine lililotajwa na mwanasheria huyo. Alisema mfumo wa Serikali mbili hauwezi kutatua kero za muungano kwa sababu Zanzibar haijapewa nguvu ya kufanya baadhi ya mambo.

Alisema hakuna utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kutenganisha mapato ya muungano na yale yasiyo ya muungano. Aliongeza kuwa mapato yanakusanywa na Serikali ya muungano lakini Serikali ya Zanzibar inapewa mgawo wake kama hisani wakati ni haki yake.

“Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kufanya chochote, ikiamua kutotoa fedha kwa Serikali ya Zanzibar, Serikali inaendeshwa vipi?” alisema Othman na kusisitiza kuwa ingekuwa vema kila upande uwe na mamlaka yake ya kukusanya kodi.

Othman alifafanua pia juu ya uhalali wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Alisema Katiba Pendekezwa inaeleza kuwa Rais wa Serikali ya Muungano atapoatikana kwa kupigiwa kura nyingi.

Alisema Katiba hiyo haijabainisha ni kiasi gani cha kura zitoke Zanzibar na nyingine zitoke Tanzania Bara. Alisisitiza kuwa Zanzibar haiwezi kutoa Rais kwa sababu wao ni wachache, lazima Tanzania Bara itapata kura nyingi kwa sababu wao wako wengi.

Kuhusu mamlaka ya Bunge, Othman alisema katiba hiyo inafafanua kuwa maamuzi ya Bunge yatafanyika kwa kufuata idadi kubwa ya wabunge wanaounga mkono jambo husika. Alisema kama ni muswada, utapitishwa kwa idadi kubwa ya wabunge bila kujali wangapi wanatoka Zanzibar.

Alisema Mambo ya Muungano ambayo kwa sasa yanatajwa kuwa yapo 16, yamekuwa ni changamoto kubwa. Alisema kero kubwa ambayo imekuwa ikipigiwa kelele kwa muda mrefu ni suala la benki kuu na kodi ya mapato.

“Mambo ya muungano wanasema yako 16, lakini ukiyataza kwa karibu yapo 21. Moja wapo ni suala la Benki kuu na ukusanyaji wa kodi ya mapato. Hakuna nchi inayoweza kuendelea kama haikusanyi kodi, sasa hapa Zanzibar imenyimwa fuesa muhmu sana ya kujitanua na kuwa kama Singapore,” alisema.

Othmani alihitimisha kwa kusema lazima kura ya maoni kubadili muundo wa muungano ipigwe ndiyo mabadiliko yaweze kufanyika. Alisema mabadiliko hayawezi kufanyika kama viongozi wenyewe hawajaamua kufanya hivyo.

Jussa ‘awavaa’ CCM

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa Ladhu alisema walipokuwa kwenye Baraza la Wawakilishi walishirikiana kwa pamoja na wawakilishi wa CCM katika kutetea maslahi ya Zanzibar.

Alisema walipofika kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMK), wawakilishi hao waliacha kutetea maslahi ya Wazanzibar na kuungana na Watanganyika kupitisha katiba mbovu kuliko hii ya sasa.

“Tuna nafasi ya kuzuia katiba hii isipitishwe kwa kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuwasemea wananchi. Oktoba 25, siyo siku ya kupiga kura tu bali ni siku ya kufanya maamuzi,” alisema Jussa.

Alisisitiza kuwa Wazanzibar wanakwenda kuamua hatima ya nchi yao kwa kuchagua viongozi wanaoipenda Zanzibar au wanaopenda madaraka. Aliwataka wananchi kuichagua CUF kwa sababu inapigania kuwa na Mamlaka Kamili ya Zanzibar.

4 Replies to “Mambo saba ni maangamizi kwa Zanzibar”

  1. Kuna msemo wa kiswahili unasemwa,anaeshiba hamjui mwenye njaaa hao viongozi smz walipokuwa baraza la wawakilishiii walionyesha msimamo kuitetea zanzibar lakini walikatazwa na bosiwao walipofika dodoma wakaufyata kwa maslahiii yao binafsi badala ya kuwatetea wazanzibar kwa faida ya wanzanzibari na vizazi vijavyoo, wako tayariii ata zanzibar ikifanya kata ya zanzibar ilimradi wao wananufaika

  2. Kimsingi Mh Othamn Masoud amemalizakazi kuuelimisha umma wa wanzizibar lakini kwa bahati mbaya sana walengwa husika hauwafikii ukweli huu. Rais wa Zanzibar hatakiwi kujiuliza eti wazanzibari tumekosa nini kiasi kwamba hatuendelei kama wanavyoendelea wenzetu Tanganyika. Ivi ndio kweli hajui kuwa sababu ni muungano uliochukua nguvu zote za serikali ya Zanzibar pamoja na uwezo wa rais wa kufanya maamuzi mazito kwa ajili ya zanazibar? Rais wa zanzibar asiwatupie lawama wapinzani kuwa ndio wanaozuia maendeleo yanayofanywa na serikali bali awalamu waliochukua mamalaka yake kinyemela kiasi ambacho serikali ikiamua kufanya jambo lolote la maendeleo serikali ya muungano huingilia kati na kusema kuwa jambo hilo halipaswi kufanywa na Zanzibar kwa sababu ni la muungano.Kama sikosea Zanzibar awali ilitaka kuanzisha bandari huru eneo la Fumba Zanzibar ilipigwa stop na Muungano, leo Serikali ya muungano wanaanzisha bandari ya kimataifa Bagamoya pasina kuingiliwa kwa sababu rais anamamlaka ya kuamua na kutenda.
    Rais wa Zanzibar asiilaumu UNECO kwa kuulinda mji mkongwe wa Zanzibar. Kwa wazanzibari hilo sio tatizo kwa vile tija inapatikana na tunaamini inawanufaisha wazanzibari wote.
    Kama kweli tunataka kuimarisha na kujenga mji wenye hadhi ya kileo (modern city ) litumiwe eneo la tunguu ambalo kwa upana wake linakidhi mahitaji ya wakazi ya walio wengi kama serikali ingezingatia hilo mapema kwa kuweka mkakati na mpango maalum wa ujenzi wa eneo lile lakini wapi? kila mmoja anaonesha fesheni ya ujenzi katika eneo la Tunguu, badala ya kupatikan haiba nzuri ya mji wa kileo kinachodhihiri ni uchafu wa majengo yenye miundo ya kichina, kijapani, kirumi nk.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s