Mjue Maalim Seif alipotokea

Mwandishi wa Makala hii Salma Said akizungumza na Mzee Rubea Ammi wa Maalim Seif ambaye pekee aliyebaki hai
Mwandishi wa Makala hii Salma Said akizungumza na Mzee Rubea Hafidh ni Ammi wa Maalim Seif ambaye pekee aliyebaki hai huko Mtambwe Nyali Mkoa wa Wilaya ya Wete Pemba

Salma Said

Nipo Kisiwani Pemba ni saa 12 asubuhi naingia garini kutoka Chake Chake naelekea Mtambwe ni kilomita 34 ni mwendo wa kasi ili nifike mapema, kila upande ninapoangaza macho yangu yanakutana na miti mingi sana njiani yenye rangi ya kijani iliyokoza, kila aina ya miti ikiwemo Mikarafuu na Mibura huku ikitoa harufu kali (siipendi) kwani Mibura harufu yake inakera tofauti na Mikarafuu ambayo ina harufu nzuri na yenye kuvutia.

Nikiwa njiani nakutana na akina mama wazee wakiwa na wamebeba majembe begani na vikapu mikononi wakielekea bondeni, njia ni safi na haina msongamano wa magari lakini maeneo ya Wete njia ni mbaya imechimbaka kwa mvua, gari chache nilizopishana nazo lakini naambiwa njia hiyo ni kongwe na hivyo gari hazipiti sana.

Mikarafuu na Mibura Wete Pemba
Mikarafuu na Mibura Wete Pemba

Nimechukua saa moja na robo kutoka Chakechake hadi Mtambwe Nyali kijiji ambacho amezaliwa Maalim Seif Sharif Hamad na hapo nimekutana na Baba yake mdogo aitwaye Maalim Rubea Hafidh Rubea (75) ambaye ndiye mzee pekee aliyebaki wengine wote wameshafariki dunia.

Familia ya Maalim Seif, ni watoto wa Ammi zake wanaoishi huko Mtambwe
Familia ya Maalim Seif, ni watoto wa Ammi zake wanaoishi huko Mtambwe

Maalim Rubea amenipokea yeye na ndugu zake Maalim Seif ambao (Cousin) ni Bi Maryam na Bi Aisha Haji Seif na kuanza kunipa historia fupi ya familia ya Maalim Seif ambapo ananieleza kwamba Maalim Seif amezaliwa na Bwana Sharif Hamad na Bi Time Seif Haji na hivyo Maalim Seif amepewa jina la babu yake mzaa mama.

Naelezwa kuwa wakati wa ukoloni Baba yake Maalim Seif alikuwa ni Sheha, na umaarufu wake akiitwa Bwana wa Mtambwe najiuliza alaa kumbe hiki cheo cha Sheha kumbe tumerithi kwa wakoloni? Naambiwa ndio. Pia Maalim Seif ni mtoto wa pekee kwa Bi Time hakuwa na mtoto mwengine zaidi yake.

Mama Bi Time Seif Haji na Bw. Haji Seif Haji ambaye ni Mjomba wa Maalim Seif alilelewa na Mjomba na alifariki mwaka 1987 wakati huo Maalim akiwa Waziri Kiongozi wa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ni nyumba ya familia ya Maalim Seif iliyopo Mtambwe
Ni nyumba ya familia ya Maalim Seif iliyopo Mtambwe

Mzee Rubea wakati wa ujana wake alikuwa mwalimu na amesomeshwa kwa miaka 11 katika skuli ya Fundo na Jadida yeye anasema Maalim Seif amekulia katika malezi ya kijijini na na sio masikini kwani wakati huo vijiji vilikuwa na neema kubwa kwani wazee wakijishughulisha na kilimo na uvuvi.

Na ndio sababu hata yeye Maalim Seif ameondokea kujua yote hayo kama anavyobainisha “Yeye kama watoto wengine akijishughulisha na kazi za nyumbani kusaidia wazee wake na akijua kuvua, kulima kuendeshwa mtumbwi baharini yote hayo akiyafanya kwa sababu akiwaona wazee wake wakiyafanya” anasema Mzee Rubea.

Asili ya Maalim ni wapi?

Suali hili linajibiwa na Mzee Rubea kwa kusema “Maalim Seif asili yake ni hapa hapa Mtambwe Nyali hajakhusu kabisa uarabuni na wanaosema kuwa MaalimSeif ni mwarabu hawamjui, lakini  sisi wazee wake ndio tunaojua kuwa hajahusu uwarabu hata chembe basi afadhali hata wangesema amekhusu Tumbatu.”.

Familia inamuonaje Maalim Seif?

Katika harakati zake zote Maalim Seif amekuwa akipata Baraka za wazee wake kwa kila analolifanya khasa yale ambao anayafanya kwa maslahi ya nchi yake na watu wake wa Unguja na Pemba.

Mwalimu Rubae yeye ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakimuunga mkono katika harakati zake akiwemo na wazee wenzake Mzee Mbarouk Nassor, Sharif Chande, Khatib Bakari, Khamis Ali lakini vijana na wenzake waliocheza pamoja na kukutana skuli pamoja ndio hao waliojitokeza kwa wingi kuwa pamoja naye katika harakati za kuipigania Zanzibar.

Ndugu na majirani zake wanasemaje?

Mzee Bakari Makame Shaame (80) ni Baba wa Mwanasiasa Machachari Bi Asha Bakari (CCM) wa kijiji Bwagamoyo huko huko Mtambwe anamuelezea MaalimSeif kuwa ni kijana mwenye mtazamo mzuri wa kisiasa na kiuongozi na sio mtu anayependa majisifu na ndio maana anaungwa mkono na watu wa rika tofauti.

Mzee Bakari Makame nilipomtembea nyumbani kwake Wete
Mzee Bakari Makame nilipomtembea nyumbani kwake Wete

“Sisi wazee tunamuona Maalim Seif ni kiongozi wetu tunamuamini na tunampenda na ndio maana tunamuombea dua kwa sababu na yeye ameonesha uaminifu wake kwetu na tunaamini anaweza kuiongoza Zanzibar”.

Bi Maryam Haji Seif na Bi Aisha Haji Seif kwa pamoja wanasema Maalim Seif ni mtu anayependa watu wa rika zote na hana tabia ya dharau tokea utotoni mwake.

Aliyekuwa kampeni meneja wake mwaka 1995 ambaye sasa ni Rais wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Awadh Ali Said anasema Maalim Seif  ni mwanasiasa mwenye ubunifu wa hali ya juu, na ni mwenye muono na mwelekeo wa kuleta mageuzi ya msingi katika uwanja wa uchumi ambapo maisha yote amepigania kujenga uchumi imara utakaoakisi huduma bora za jamii na hivyo kustawisha maisha ya wananchi.

“Ni muumini wa demokrasi, utawala wa sheria na anaetetea usawa wa wananchi katika kupata haki na fursa bila ubaguzi wa aina yoyote, huyo ndio Maalim Seif” amesema.

Mwanasheria Awadh Ali Said
Mwanasheria Awadh Ali Said

Aidha anasema Maalim Seif ni mwanasiasa anaeamini kuwa siasa si ulumbi wa maneno na ahadi za ulaghai bali siasa ni uwanja wa kutekeleza mambo yamaendeleo na mageuzi yanayojengwa katika jamii inayoendeshwa kwa nidhamu na iliyojiwekea malengo maalum.

Wenye mtazamo hasi

Bakari Mshindo ni mtaalamu wa Kiswahili na mwenyekiti wa bodi za shirika la magazeti ya serikali na aliyewahi kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketiya CCM anasema Maalim amekomaa kisiasa hivi sasa kwani alikuwa akihubiri siasa za vurugu za jino kwa jino lakini sasa anahubiri siasa za kistaarabu na njia za Amani.

“Amekomaa kisiasa alipoanza alikuwa anataka uongozi kwa kutumia vijana wenye jazba na sera ya jino kwa jino lakini sasa amebadilika” alisema.

Said Miraji alikuwa CUF na sasa amejiunga na ADC anasema Maalim Seif ana kawaida ya kumpenda mtu na kumuamini bila ya kiasi, na akimchukia pia humchukia kwa kiasi kikubwa.

Anasema Maalim hatofautishi mamlaka yake ya kichama na alipokua serikalini, serikalini wakubwa huwa hawakosolewi na wadogo moja kwa moja, wadogo wakifanya hivyo huoanekana hawana adabu, ila katika vyama ni jambo la kawaida.

Katika mfumo wa vyama vingi unaweza kuwa na wanachama wenye tabia tofauti, ila bado yeye hutafsiri tofauti ya mawazo ni usaliti hii ni aibu kwa mtu kama yeye kushindwa kuvumilia tofauti ya mawazo ya wengine na kuwaita ni wasaliti.

Miraji anasema Maalim huahidi mambo kwa wafuasi wake “Mfano wakati wa uchaguzi wakati wa migogoro kila alipoahidiwa jambo hasa na wazungu alikuja hadharani kuwaeleza watu na kuwajengea matumaini mwisho maadui zake wanaingilia kati na kuzuia mafanikio yake na hatimae akaonekana yeye ni muongo”.

         Said Miraji
Said Miraji aliyekuwa Mkurugenzi wa Vijana CUF

Miraji anasema Maalim akitaka jambo lake anaweza kutumia gharama zozote hata ikibidi kukigharimu chama kwa kulazimisha watu wote wafate msimamo wake anasema ingawa Maalim ni mwerevu wa kutumia watu wengine na yeye hubaki nyuma ya pazia.

Lakini tabia yake ya kumsulubu mtu kwa maneno mbele ya watu bila ya kujali umri, jinsia, cheo wala mahusiano aliyonayo mtu huyo, na watu waliopo mbele yake.

Kauli hii ya Miraji iliungwa mkono Mzee Machano na Maalim Rubea ambapo amesema hii ni tabia ya Maalim anapokuwa anasimamia jambo anakuwa mkali huku akijitolea mfano yeye mwenyewe.

“Mimi ni Mzee wake Maalim Seif na nilikuwa Mwenyekiti wa Jimbo lakini anapokuja kufuatilia masuala ya kichama anasahau kama mimi ni Mzee wake hataki kabisa kuharibiwa kazi na anakuwa mkali katika kusimamia kazi”.

Harakati na vuguvugu la kisiasa

Tofauti na mawazo ya wengi kwamba harakati za kisiasa na hatimae kuzaliwa kwa chama cha upinzani Zanzibar zimetokana na watu wa kisiwa cha Pemba pekee lakini ukweli ni kwamba washiriki wa harakati hizo ni wazanzibari wenyewe kwa pande zote mbili Unguja.

Waliosaidia harakati hizo pamoja na wengine lakini watu wanne ndio walikuwa mstari wa mbele ambapo kutoka Unguja ni Mzee Mchano Khamis Ali, Ali Haji Pandu, Shaaban Khamis Mloo na Khatib Hassan na kutoka Pemba alikuwa Soud Yussuf Mgeni, Suleiman Seif Hamad Hamad Rashid Mohammed na Maalim Seif.

Mzee Ali Haji Pandu na Dk Maulid Makame
Mzee Ali Haji Pandu na Dk Maulid Makame

Katika kumuunga mkono Dk Maulid Makame alikuwa waziri wa Afya wakati ule Machano Khamis Ali akiwa Kashna Msaidizi wa Polisi ambapo alishawahi kupewa karipio Kamishna wa polisi Tanzania kutokana na mahusiano yake naMaalim Seif wakati huo akitanabahishwa kuhatarisha nafasi yake hiyo.

Wengine waliokuwa katika harakati za kumuuonga mkono Maalim Seif ni pamoja na Juma Othman Juma alikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya CCM, Juma ngwali Kombo alikuwa Mkuu wa Mkoa kusini Pemba na Masoud Omar Said alikuwa Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba.

Lakini pia walikuwepo wengine ambao wakiunga mkono harakati hizo za kudai maslahi ya Zanzibar akiwemo aliyekuwa Naibu Waziri, Bi Asha Bakari Makame (ambaye kwa sasa amekuwa ndio mpingaji mkubwa wa Maalim na anayepambana kwa maneno ya Ismail Jussa), mwengine ni Juma Othman na Dk Maulidi Makame ambao wakidaiwa wanaendesha hujuma dhidi ya chama cha CCM na dhidi ya Muungano

Juma Othman na Fatma Maghimbi walipotoka CUF na kujiunga na CCM
Juma Othman na Fatma Maghimbi walipotoka CUF na kujiunga na CCM

Lakini pia walikuwepo wengine ambao wakiunga mkono harakati hizo za kudai maslahi ya Zanzibar akiwemo aliyekuwa Naibu Waziri, Bi Asha Bakari Makame (ambaye kwa sasa amekuwa ndio mpingaji mkubwa wa Maalim na anayepambana kwa maneno ya Ismail Jussa), mwengine ni Juma Othman na Dk Maulidi Makame ambao wakidaiwa wanaendesha hujuma dhidi ya chama cha CCM na dhidi ya Muungano.

Bi Asha Bakari na Ismail Jussa walipokuwa na lengo moja la kuipigania Zanzibar
Bi Asha Bakari na Ismail Jussa walipokuwa na lengo moja la kuipigania Zanzibar

Mwengine hakufukuzwa chama lakini alisimamishwa uongozi na kupewa karipio kali aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Vuguvugu hilo likaendelea na lilizidi kupamba moto pale mwaka 1989 Maalim Seif alipofanyiwa mahoajino na BBC akasema Muungano huu haujashirikisha wananchi na ifike pahala wananchi washirikishwe na watoe maoni yao ambapo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza hadharani baada ya kufukuzwa na ndio sababu ya kuleta vuguvugu kubwa iliambatana na siku za sherehe za Eid ambapo kwa wakati huo BBC ilikuwa ni chembo pekee kinachosikilizwa na wananchi wengi hapa Zanzibar.

BBC_News_gplus

Waliposikia makundi watu yakawa yanamfuata na kumpongeza kwa kauli yake na kumuunga mkono hatimae 10 May 1988, akamamatwa na kuwekwa kizuizini kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali, lakini baada ya kuonekana kosa hilo dogo na angeweza kupata dhamana na lengo lilikuwa kumdhibiti hivyo akashitakiwa kwa kosa la kupatikana na nyaraka za siri za serikali huku akishitakiwa chini ya sheria za usalama wa taifa.

Vuguvugu hilo la kudai mabadiliko mnamo mwaka

1988-89 Maalim Seif baada yakufukuzwa kwenye CCM na uwaziri kiongozi wazanzibari wengi wakazidi kuunga mkno harakati zake hali ambayo ilipelekea wakati mgumu kwa CCM.

Mwalimu Julius Nyerere
                                   Mwalimu Julius Nyerere

Baada ya hali hiyo Mwalimu Nyerere alifanya ziara maalumu katika mikoa yoteya Zanzibar akielezea sababu za kufukuzwa kwa Maalim Seif na wenzake huku kutoa shutuma kali dhidi yao ambapo nao wakaamua kuandika barua kali iliyosainiwa na watu wanne akiwemo Soud Yussuf, Maalim Seif, Mzee Mloo na Ali Haji Pandu.

Katika hali hiyo hiyo ya joto la kisiasa kupanda kwa kuondoshwa Maalim Seif kwenye uwaziri kiongozi na kuwekwa Dk Omar Ali Juma alikuwa akikumbana na wimbi kali la harakati hizo ambapo wakati mmoja aliitishwa mkutano mkubwa wa wasomi na kutoa hutuba kali na maneno makali ya wasomi hayo na kuzidisha kupandisha joto la kisiasa Zanzibar.

Dk Omar Ali Juma
Dk Omar Ali Juma

Mahakamani

Kesi yake ilikuwa ni sehemu ya vuguvugu la kisiasa na kuonesha upinzani dhidiya serikali na CCM wakati huo mamia wazanzibari wakenda mahakamani kusikiliza kesi na wasiopata nafasi ya kuingia ndani wakisubiri nje, na kawaida yake akitoka mahakamani na kuingizwa katika gari akionesha dole akionesha alama ya mapambano dhidi ya Dola kandamizi na hapo ndipo lilipotoka jina la Mandela wa Zanzibar na Seif Mkombozi. Maalim Seif akatangaza Mahakamani kwamba chama wanachokiunda ni Zanzibar United Front (ZUF).

KAMAHURU, ZUF na hatimae CUF

Wakati huku nje Wanamageuzi mbali mbali wakafanya mkutano wa kitaifa Chuo kikuu Dar es Salaam moja katika maazimio ni kumtangaza Maalim Seif ni mfungwa wa kisiasa na kuitaka serikali imuachie huru na hapo iliundwa kamatiya kupigania mabadiliko ya katiba ikiongozwa na Chief Fundikiza na Mabere Marando ambapo wahaharakati kutoka Zanzibar walishiriki katika mkutano huo na kutakiwa nao waanzishe kamati yao ndipo ikaanzishwa Kamati ya Mageuzi yaVyama Huru (KAMAHURU).

KAMAHURU ikiwa chini ya Mwenyekiti Shaaban Khamis Mloo na Katibu wake Ali Haji Pandu na wajumbe wengine sita, ilipofika Novemba 1991 alipotolewa gerezani Maalim Seif alitangaza kuiunga mkono KAMAHURU na baadae vuguvugu hilo kuendelea hadi ZUF kilikuwa kimeanzishwa Zanzibar pekee lakini kutokana na Nyerere kushituka na akajua hali hiyo ingeweka kuuweka pabaya Muungano ndipo akaweka masharti lazima vyama vya siasa viwe vya kitaifa na mwaka 1992 chini ya sheria ya vyama vya siasa vyama vyote vikatakiwa viwe vya kitaifa na ndipo harakati mpaya za kudai chama cha siasa ili KAMAHURU iwe ni chama cha kitaifa.

Ismail Jussa na Hamad Mmanga wakiwa na Maalim Seif baada ya alipotoka Gerezani chini ya utawala wa Dk salmin
Ismail Jussa na Hamad Mmanga wakiwa na Maalim Seif baada ya alipotoka Gerezani chini ya utawala wa Dk salmin

Katika harakati hizo masharti makubwa matatu moja makao makuu ya chama yawe Zanzibar, pili uongozi ugawiwe kwa usawa, tatu vyombo vyote vya maamuzi wajumbe wawe na idadi ya uwiano baada ya makubaliano hayo chama Civic Movement na KAMAHURU wakakubaliana kuundwa kwa Civic United Front (CUF) Na baada ya Maafikiano hayo kulifikiwa Mwenyekiti wake akawa James Mapalala na  ndipo katibu Mkuu wa kwanza wa chama hicho akawa Maalim Seif na Mzee Shaaban Mloo Makamo Mwenyekiti.

Mzee Shaaban Mloo aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa CUF Zanzibar
Mzee Shaaban Mloo aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa CUF Zanzibar

Na kuanzia May 1992 ikazaliwa CUF na kupata usajili wa muda harakai zikaendelea licha ya vikwazo mbali mbali wakishutumia bkuwa ni chama cha Wapemba, chama cha Kidini, chama cha wazanzibari tu lakini safari ya chama hicho imepita katika mito na mabonde hadi kusimama kwake.

Maalim alikuwa akionesha kupambana wazi wazi na Mwalimu Nyerere katika kutetea maslahi ya Zanzibar jambo ambalo kwa wakati ule ilikuwa ni nadra kwa kijana kama yeye kupambana na kiongozi mkuu wa nchi.

Waliofanyanaye kazi

Mzee Ali Haji Pandu mwenye asili ya Makunduchi, anasema Maalim Seif ni mtu muadilifu na hana tabia ya tamaa katika maisha tofauti na wanasiasa wengine wengi ambao wanapenda madaraka na ulafi.

Mzee Ali Haji Pandu akiongea na Salma Said nyumbani kwake Magomeni
Mzee Ali Haji Pandu akiongea na Salma Said nyumbani kwake Magomeni

Mzee Ali Haji yeye anamlinganisha Maalim Seif na watu kama Mandela kwa kupigania nchi yake na kutokana tamaa kirahisi, “Misukosuko aliyoipata MaalimSeif ingekuwa mtu mwengine angeshakata tamaa akaachana na siasa lakini yeye ni mtu jasiri anayefaa kupigiwa mfano kama akina Mandela”.

Mzee Machano Khamis Ali mwenye asili ya Donge, ambaye kwa sasa ni Makamo Mwenyekiti wa  wa CUF mstaafu (70) yeye ni miongoni mwa watu wachache wa mwanzo kumuunga mkono Maalim Seif wakati wa kuanza harakati za kuipigania Zanzibar kuwa na Mamlaka yake.

Mzee Machano Ali akizungumza na Salma Said nyumbani kwake Mombasa Zanzibar
aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa CUF Zanizbar, Mzee Machano Khamis Ali muda mfupi baada ya mazungumzo yake na Salma Said nyumbani kwake Mombasa Zanzibar

“Kupigania Mamlaka ya Zanzibar hatukuanza sasa ni miaka mingi sana madai yetu yalikuwa ni hayo” amesema Mzee Machano.

Siri ya mafanikio yake

Siri ya mafanikio ya Maalim Seif ni ukweli wake na kufuatilia mambo kwa umakini ndio sababu kubwa ya watu wengi kumuunga mkono hata kwa wale ambao wana mitazamo tofauti ya kisera na kiitikadi.

Maalim Seif na Dk Amani Karume wakizindua kitabu
Maalim Seif na Dk Amani Karume wakizindua kitabu

Inaelezwa kwamba umaarufu wake ameanza kuupata mapema akiwa Waziri wa Elimu Zanzibar na pale alipoteuliwa kushika nafasi ya Mipango na Uchumi kwneye idara za CCM na akamalizia kwenye waziri kiongozi, vuguvugu la kisiasa na harakati zake za kudai maslahi ya Zanzibar ambapo hadi sasa Maalim Seifanaonekana kama kiongozi mkweli na mwenye kutaka mabadiliko makubwa.

Mzee Machano akitaja mambo ambayo aliyoyasimamia Maalim Seif akiwa waziri kiongozi, ni pamoja na ni kurejesha nidhamu na kuheshimu wakati wa kazi ambapo alikuwa akenda mapema kazini na kutaka wafanyakazi wote wa serikali kuanza saa 1.30 kazini na kutoka saa 2.30.

Maalim Seif akimfariji Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai
Maalim Seif akimfariji Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai

Jengine ni kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha za serikali, Gari za serikali zikitumika saa za kazi tu na ni marufuku kutumika kwa shughuli binafsi.

Suala la kuongezwa mishahara wafanyakazi pamoja na aliyekuwa Rais ni Ali Hassan Mwinyi lakini Maalim ilikuwa ni chimbuko la utetezi huo na alilisimamia mwenyewe hadi mwisho.

Mwaka 1984 Maalim alisimamia kuazisha kwa sera ya biashara huria na baadae kuja kutumika kwa Tanzania nzima mwaka 1985 baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuingia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye akataka itumike baada ya kuona ina faida kwnai sera hiyo iliondosha dhidi ya maisha Zanzibar na ndipo vijana kuanza kupata ajira na biashara kuimarika nchini.

Aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi
Aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi

Jengine alisimamia Mpango wa kitaifa wa Kujitoshelewa na Chakula (MTAKULA) ambapo katika kulisimamia hilo akenda mwenyewe mabondeni na kuzungumza na wakulima kuona wakulima wanakumbana na changamoto gani na kuzitatua kwa haraka hivyo suala la mbegu, pembejeo na halikuwa jambo lililokuwa likiwasumbua wakulima kwa wakati huo.

Katika jambo jengine ambalo limemuinua kisiasa Maalim Seif ni pale alipokwenda Baraza la Wawakilishi kama Waziri Kiongozi mwaka 1984 kupitisha katiba mpya ya Zanzibar, Sheria namba 1 ya mwaka 1985 pamoja na wajumbe wa baraza la wawakilishi kupitisha nembo ya taifa ya Zanzibar na Bendera yaZanzibar.

Ahadi yake kuu kwa wazanzibari

Disemba 1987 Maalim Seif alikwenda matibabu Ulaya wakati huo akiwa Waziri Kiongozi zile fununu za kutaka kufukuzwa tayari zilikuwa zimeshaanza kusikika chini kwa chini wakati huo wanaharakati wenzake walimuandalia mapokezi makubwa Unguja na Pemba lakini bahati mbaya mapokezi ya Unguja yaliingiliwa na idara za usalama yakawa ni madogo lakini baadae alikwenda Pemba na huko alipokewa na umati makubwa na alitembea kwa miguu kutoka uwanja wa ndege hadi uwanja wa Tibirinzi Chake Chake ambapo alihutubia na kuwaahidi maneno haya ambayo hadi leo ahadi hiyo anaendelea nayo na ndio kitu ambacho anaona hajatimiza ahadi kwa wazanzibari.

whiter-zanzibar-1

Alisema hivi: “Umoja wetu ndio silaha yetu. Ndugu wananchi wa Unguja na Pemba katu wasikubali kugawiwa. Matokeo ya karibuni yameonesha kwamba kama hakuna umoja, kama tunapigana majungu, nasema aliyepoteza sio Seiflakini iliyopeteza ni Zanzibar, kwa hivyo nasema matokeo ya karibuni ni matokeoya Wazanzibari kujifunza. Nasema sina cha kuwalipa wala sina cha kuonesha shukrani zangu isipokuwa kuahidi tu kuwa mimi nitaendelea kuwatumikieeni nikiwa ndani ya chama, nikiwa nje ya chama; nitaendelea kuwatumikieni nikiwa ndani ya serikali, nikiwa nje ya serikali. Hizo ndio shukrani zangu. Nawashukuru sana sana kwa ushirikiano mlionipa.”

Maalim Seif akihutubia kwenye mkutano wa mwaka 1995
Maalim Seif akihutubia kwenye mkutano wa mwaka 1995

Wasifu wake:

Maalim Seif alizaliwa Oktoba 22, 1943 Nyali, Mtambwe Kisiwani Pemba na kupata mafunzo ya msingi katika Shule ya Uondwe na baadae shule yawavulana ya Wete kati ya mwaka 1950 – 1957) na baadae kujiunga na elimu yaSekondari Kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka mwaka 1958 – 1961

Skuli aliyosoma Maalim Seif
Skuli aliyosoma Maalim Seif

Maalim Seif alijiunga na Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mfalme George Unguja ambayo sasa inaitwa Lumumba na kuendelea hadi kidato cha tano na sita 1962 -1963.

Maalim aliajiriwa kama mwalimu kwa miaka tisa kati yam waka 1964 – 1972 na alifundisha Sekondari Fidel Castro iliyoko Pemba na Chuo cha Ualimu cha Lumumba kilichoko Unguja ambapo mwaka 1972 aliruhusiwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Usimamizi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa na kukhitimu shahada hiyo  mwaka 1975 akiwa mmoja wa wanafunzi waliofaulu vizuri sana na kuweka rekodi nzuri chuoni hapo.

Wadhifa wake serikalini

Maalim Seif aliingia katika masuala ya uongozi wa serikali mwaka 1975, alipoteuliwa kuwa Msaidizi Binafsi wa Rais wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe ambapo aliifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977. Mwaka 1977 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar na akatumika katika nafasi hiyo hadi mwaka 1980.

Mnamo Februari 1984 akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar.Maalim Seif amekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar katika kipindi chote cha uongozi wa Rais Mwinyi kama Rais wa Zanzibar, na mwaka 1985 alipochaguliwa Rais Idris Abdul Wakil (Marehemu) kuongoza Zanzibar, bado Maalim Seifaliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi na alishikilia wadhifa huo hadi Januari 1988 alipoondolewa katika baraza la mawaziri na baadaye kufukuzwa ndani ya CCM. Kwa hivyo, Maalim Seif amekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuanzia mwaka 1977 hadi 1988.

Wadhifa wake kwenye siasa

Kisiasa, Maalim Seif amepitia katika nafasi nyingi sana. Mwaka 1977 – 1988 alikuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM lakini pia mwaka 1977 – 1987 alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM huku mwaka 1982 – 1987 akiteuliwa kuongoza Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi (kitaifa).

Maalim Seif na wenzake kadhaa walifukuzwa kutoka Chama Cha Mapinduzi mwaka 1988 baada ya kushindana kimsimamo na CCM na alikuwa mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la “Kamahuru” la Zanzibar lililoungana na CCW (Chama Cha Wananchi) ya Tanzania Bara na kuunda Chama Cha Wananchi CUF ambapo yeye (Maalim Seif) alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kwanza wa CUF akihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1999 alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CUF wadhifa ambao anao hadi sasa.

Wadhifa wake Kimataifa

Maalim amewahi kushikilia wadhifa mkubwa sana kimataifa kati ya mwaka 1997 – 2001, alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa “The Unrepresented Nations and Peoples Organization (UNPO)” (Nchi zisizowakilishwa na Mashirika ya Watu) – Tafsiri yangu. Hii ni taasisi ambayo makao makuu yake yapo jijini The Hague nchini Uholanzi na inahusisha mataifa zaidi ya 50 duniani na watu ambao siyo wajumbe wa Umoja wa Mataifa, yaani ambao wakienda Umoja wa Mataifa wanakuwa na hadhi ya waangalizi tu (au wageni).

download

Baadhi ya nchi mwanachama wa umoja huu ni pamoja na Taiwan, Tibet na Zanzibar. Lakini pia amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Vyama vya Kiliberali Duniani kati ya mwaka 2002 – 2003.

Maalim Seif na mkewe Bi Awena Sanani wakiporudi Zanzibar wakitokea nchi za Ulaya
Maalim Seif na mkewe Bi Awena Sanani wakiporudi Zanzibar wakitokea nchi za Ulaya

Maalim Seif amemuoa Bi Fourtuna Saleh Mbamba na amezaa mtoto mmoja na kisha kufunga ndoa na Bi Aweina Sinani Masoud tangu mwaka 1977 na wana watoto watatu wote wa kike.

Advertisements

3 Replies to “Mjue Maalim Seif alipotokea”

    1. Na kwa sasa jee bado anaendelea na wadhifa gani katika Chama cha C.U.F? Na jee kwa uoni wako wataingia katika kinyang’anyiro kwa mwaka 2020?

      1. Namiya kwa sasa Maalim bado ni katibu mkuu wa Chama cha Wananchi C U F sina uhakika wa kuwa atagombea mwaka 2020 Ila tunamuombea kwa Mungu amlinde na ampe nguvu Kwani Wazanzibar tunampenda sana na Zanzibar inampenda na Zanzibar anaipenda tunaamini bado anaweza kutusimamia

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s