Wananchi waandaliwe kisaikolojia kupokea matokeo

NEC itoe majibu ya namna wanafunzi wa vyuo vikuu watakavyopiga kura
NEC itoe majibu ya namna wanafunzi wa vyuo vikuu watakavyopiga kura

Njombe. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele ameitaka Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaandaa wananchi kisaikolojia ili wawe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi wasiyotarajia.

Askofu huyo pia ameitaka Serikali kuheshimu uamuzi wa wananchi baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kutangazwa ili kuondoa uwezekano wa kutokea vurugu na amani kutoweka.

Akihutubia kwenye mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Seminari ya Kidugala mkoani Njombe, Askofu Mengele alisema Serikali haina budi kuanza kuwaandaa wananchi kisaikolojia kupokea matokeo.

“Ni vizuri kuwaandaa wananchi kisaikolojia kwa kuwa lolote linaweza kutokea. Kikubwa ni kutopindisha uamuzi wa wananchi,” alisema Askofu Mengele kwenye mahafali hayo ambayo yalihudhuriwa pia na wachungaji na wainjilisti.
“Naiomba Serikali iheshimu uamuzi wa wapigakura kwa sababu ikifanya tofauti, itawagharimu na itagharimu amani ya nchi yetu.”

Askofu Mengele alitoa kauli hiyo zikiwa zimesalia siku chache kabla ya wananchi kupiga kura Oktoba 25 kumchagua Rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi unaoonekana kuwa na ushindani mkubwa kuliko chaguzi nne zilizopita tangu siasa za vyama vingi zirejeshwe.

Wakati NEC ikiwahakikishia wananchi kuwa matokeo ya uchaguzi yatakuwa ya haki, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) – Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi na NLD – vimekuwa vikituhumu kuwapo kwa njama za kuchakachua matokeo.

Askofu Mengele pia aliitaka NEC kutoa majibu ya namna ambavyo wanafunzi wa vyuo vikuu nchini watapiga kura.
Askofu huyo pia amesema KKKT, ambayo inamiliki vyuo vikuu saba, imeunda timu ya maaskofu kwa ajili ya kukutana na viongozi wa NEC kujadiliana juu ya mustakabali wa wanafunzi katika suala la upigaji kura.

Askofu Mengele alisema NEC inapaswa kutoa majibu hayo mapema ili kutowachanganya wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha kupiga kura wakati wakiwa vyuoni na ambao kwa sasa wapo likizo hadi baada ya uchaguzi.
Askofu Mengele alisema awali, wakati wa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, NEC iliwatoa wanafunzi hao wasiwasi kuwa wanaweza kupiga kura ya Rais kwenye kituo chochote tofauti na kauli ya sasa kuwa hakuna atakayeruhusiwa kupiga kura nje ya kituo alichojiandikisha.

Alisema siku ya kupiga kura hakuna chuo ambacho kitakuwa kimefunguliwa na kwamba si rahisi kwa wanafunzi hao kujisafirisha mpaka kwenye vituo walivyojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.

Kuhusu vitambulisho vya kupigia kura, Askofu Mengele aliwataka Watanzania kuvitunza na kutoa taarifa ya watu walioanza kupita mitaani kuvikusanya, akisema ni kinyume cha taratibu.

Alisema maaskofu wamepata taarifa ya kuwapo kwa watu wanaokusanya kadi hizo licha ya kuwa hawajui sababu na akaiomba Serikali kusimamia na kuhakikisha suala hilo haliendelei.

Aliwataka Watanzania kuendelea kumwomba Mungu ili uchaguzi huo uwe wa amani na utulivu na kuwapata viongozi bora watakaoiongoza kwa awamu nyingine.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s