Lowassa, Magufuli waikwepa Mwanza

Wagombea wa urais wadaiwa kuukwepa Mji wa Mwanza
                              Wagombea wa urais wadaiwa kuukwepa Mji wa Mwanza

Dar es Salaam. Wakati kampeni zikiwa zimefikia katikati, vyama vya CCM na Chadema bado hazijajitosa mkoani Mwanza kufanya mikutano yake licha ya kupita mikoa inayouzunguka.

Mgombea wa CCM, John Magufuli jana alikuwa mkoani Geita baada ya kufanya kampeni Mkoa wa Kagera na anatarajiwa kuhamishia harakati zake mkoani Shinyanga.

Mgombea wa Chadema, ambaye pia anaungwa mkoano na vyama vingine vitatu vinavyounda Ukawa-NLD, CUF na NCCR Mageuzi-, jana alikuwa mkoani Lindi baada ya kufanya mikutano yake mkoani Mtwara na Dar es Salaam.

Tayari wagombea hao wawili, wanaochuana vikali wameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa inayopakana na Mwanza, lakini wanaonekana kutegeana au wameuweka kiporo mkoa huo, ambao una wapiga kura takriban milioni 1.4 kwa mujibu wa makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Mkoa wa Mwanza ambao ni kitovu cha shughuli za kiuchumi za mikoa ya Kanda ya Ziwa, unapakana na Kagera, unaokisiwa kuwa na wapigakura 217,390, Geita (808,337), Shinyanga (762,317), Simiyu (714,757) na Mara inayokisiwa kuwa na wapiga kura 834,580. Mkoa huo una majimbo ya Ukerewe, Nyamagana na Ilemela yaliyo chini ya Chadema, na Magu, Nyamagana, Buchosa, Misungwi na Sengerema yaliyo chini ya CCM.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa alifanya mikutano ya kampeni Mkoa wa Kagera, ambao uko Kaskazini Magharibi mwa Mwanza, Mara (Kaskazini Mashariki), Shinyanga, Simiyu na Geita iliyo upande wa Kusini.

Dk Magufuli amefanya mikutano ya kampeni kwenye mikoa hiyo pia akiuruka Mkoa wa Mwanza.

Walipoulizwa sababu za wagombea wao kuuweka kiporo Mkoa wa Mwanza, wasemaji wa vyama hivyo walisema wanafanya hivyo kwa kufuata ratiba na si kutegeana au kuuweka mkoa huo kiporo kwa malengo maalumu.

Mkurugenzi wa mawasiliano ya umma wa CCM, Godfrey Chongolo alisema jana kuwa wanafanya kampeni kulingana na ratiba ya Tume ya Uchaguzi (NEC), ambayo ilibadilika licha ya kuwa walipanga awali kufanya Mkoa wa Mwanza.

“Unajua NEC ndio wanaopanga ratiba. Vyama vyote vimepangiwa ratiba na kila mahali kwa tarehe zake za kampeni, sasa huwezi kwenda nje ya hapo utakuwa unakiuka taratibu,” alisema Chongolo.

Hata hivyo, alisema kuwa watafanya kampeni Geita na leo Alhamisi wataanzia Kahama na baadaye Shinyanga mjini kuhitimisha kampeni za Kanda ya Ziwa.

Alisema baada ya ratiba hiyo, Dk Magufuli na timu yake watarudi Dar es Salaam kabla ya kuendelea na ziara kama hiyo visiwani Zanzibar.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema kuwa Ukawa wanafuata ratiba ya NEC na hawawezi kufanya kampeni nje ya ratiba ya chombo hicho cha uchaguzi

“Hatuwezi kujifanyia kampeni tunavyotaka, NEC wamepanga hivyo. Tulipeleka mapendekezo, lakini NEC wakaja na ratiba nzima ya kampeni, na hata ukiangalia, kila mahali tunaacha baadhi ya maeneo ya kuja kumalizia.

“Huu ni mpango mkakati vilevile, umetusaidia, kwanza mpango wetu ni kuacha kila kanda mkoa mmoja au eneo moja kwa ajili ya kuja kuhitimisha, hatutaki kuondoka moja kwa moja,” alisema.

Alisema kuwa Ukawa imejipanga tangu uzinduzi ndiyo maana baada ya uzinduzi moja kwa moja walikwenda Nyanda za Juu Kusini na kuendelea na ratiba.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, vyama vinatakiwa kupeleka NEC mapendekezo ya ratiba za shughuli zao za kampeni na Tume huangalia ratiba za vyama vyote na kutoa ya mwisho ambayo inaondoa migongano kwa vyama.

Wagombea hao pia wamegusa sehemu ndogo ya mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa, Iringa na Njombe, lakini ukiondoa CCM wameepuka kuingia Jiji la Mbeya, ambalo linakisiwa kuwa na wapigakura wapatao milioni 1.47. Mikoa hiyo inakisiwa kuwa na jumla ya wapiga kura milioni 3.1.

Mbali na mikoa hiyo miwili yenye watu wengi, wagombea hao wawili wamefanya mikutano mkoani Tanga na kuacha kiporo mikoa mingine ya kaskazini, ambayo ni Kilimanjaro, Manyara na Arusha.

Mikoa ya kaskazini ina jumla ya wapigakura milioni 3.8 na vyama hivyo vina mpambano mkali kwenye majimbo.

Mpaka sasa, NEC imekwishaandikisha watu 24,252,927 kwa mujibu wa takwimu za makadirio zilizotolewa na NBS Julai 17, 2015 ikionyesha kukamilika katika mikoa 17

Kati ya hao, mikoa mingi ikiwemo Mwanza na Dar es Salaam ndiyo yenye watu wengi wanaokadiriwa kufikia milioni 4.4. Mkoa wa Mwanza una watu milioni 1.4 na Dar es Salaam ni milioni tatu.

Mgombea wa CCM, Dk Magufuli bado ameweka akiba ya kampeni kwa mikoa hiyo wakati Lowassa ameshagusa sehemu ya Dar es Salaam katika maeneo ya Bunju, Tegeta, Chanika, Kigamboni na Mbagala.

Chanzo: Mwananchi

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s