Hujuma nzito ndani ya kambi ya Dk. Magufuli

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni

Hatimaye mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameibuka hadharani na kuzungumzia tatizo la kuwapo kwa baadhi ya wafuasi wa chama chake kumhujumu kwa kuunga mkono harakati za upinzani.

Akizungumza kwenye viwanja vya Zimbiilo, Wilaya ya Muleba Kusini jana, Magufuli alisema anatambua kuwapo kwa baadhi ya wanaCCM wanaojionyesha kumuunga mkono nyakati za mchana lakini inapofika usiku hubadilika na kuwaunga mkono wapinzani.

“Naomba na nyinyi msiniangushe maana wengine mchana mnakuwa CCM, usiku mnahamia vyama vingine, mimi nina moyo kama nyie jamani msiponichagua nitakwazika sana Wanamuleba,” alisema Magufuli.

Hivi sasa, Magufuli amekuwa akichuana vikali na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anaeywakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF). Wote wawili wamekuwa wakivutia maelfu ya wananchi karibu katika kila mikutano yao ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25.

Kadhalika, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo, alizungumzia pia tatizo hilo la kuwapo kwa wanachama wa CCM  ambao wamekuwa wakisaidia wka kificho kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa.

Bulembo alifichua hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumnadi Dk. Magufuli katika Jimbo la Bukoba Vijijini.

Akieleza zaidi, Bulembo alisema ana ushahidi kwamba ziara ya Lowassa mkoani humo iliratibiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho na hivyo akawataka kuamua moja, ama kuitumikia CCM kwa dhati au kuondoka CCM mara moja na kumfuata Lowassa. “Msidhani hatuwafahamu. Mikakati yote na namna mnavyofadhili Ukawa na Lowassa tunafahamu, tena tunawafahamu kwa majina na nawaambia ole wenu… msipoondoka wenyewe, tutawafukuza baada ya Dk. Magufuli kushinda,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

“Anayempenda Lowassa na Ukawa avue magwanda ya CCM na awafuate huko. Hatutaki watu ambao mchana ni CCM usiku ni Lowassa… hili ni gari kubwa. Wengine wanashuka, wengine wanapanda,” alisema Bulembo.

Alisema yeyote mwenye kinyongo na CCM hafai kubaki ndani ya chama hicho kwa sababu (chama hicho) kina wanachama wengi na hakiangalii uwezo wa mtu kifedha.

“Tunawajua mnaomng’ang’ania Lowassa. Lakini nawahakikishia kuwa mtalia baada ya uchaguzi wa mwaka huu…  mnajifanya CCM lakini mnafadhili upinzani,  mwisho wenu unakuja,” alisema Bulembo.

KUKOMESHA MAFISADI
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alirudia kauli yake kuwa kamwe hatalea mafisadi wanaorudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa manufaa yao binafsi.

Alisema watu wenye tama ya fedha ndiyo wameifikisha nchi pabaya kwani fedha nyingi zimeishia mikononi mwao.
Alisema atahakikisha Tanzania haiendelei kuwa shamba la bibi kwa sababu yeye hakuomba urais kwa majaribio bali kupambana na wezi wote wa mali za umma.

IKULU NJIA NYEUPE
Kuhusiana na safari ya Ikulu baada ya Oktoba 25, Magufuli alisema njia ni nyeupe kwake kwa sababu hakuna mgombea yeyote mwenye sifa zinazofanana naye.

Dk. Magufuli alisema kwa namna wananchi wanavyompokea kwenye mikutano yake, ni dalili ya wazi kwamba hakuna kizingiti cha yeye kushindwa kuingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu.Alisema Ikulu ni ya CCM na wapinzani wamebaki kuwa wasindikizaji wa chama hicho na kwamba, hata wao (wapinzani) wanajua fika kwamba hawataweza kuingia Ikulu.

“Ikulu ni ya Magufuli. Wengine ni kama wale wasindikizaji wa harusi. Wanamuleba msirubuniwe,” alisema Dk. Magufuli huku wananchi hao wakishangilia kwa kiitikio cha “Rais! Rais! Rais!”

RANCHI 52
Akiwa katika viwanja vya Polisi Kamachumu, Wilaya ya Muleba Kaskazini, Dk. Magufuli alielezea kukerwa na namna ranchi 52 zilivyobinafsishwa vibaya na  kuwasababishia wananchi wengi wabaki bila ardhi, huku akimshushia waziri mmoja wa serikali ya Rais Kikwete. Hata hivyo, hakutaja jina la waziri huyo. “Katika vitu vilivyoniumiza nikiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni namna ranchi hizi zilivyogawiwa ovyo ovyo, simtaji waziri huyo maana wote mnamjua. Lakini cha ajabu hao hao ndiyo wanakuja kwenu kuomba kura,” alisema.

Aidha, alisema akiingia madarakani atahakikisha anawezesha kuongezeka bei ya kahawa na kuiongezea thamani ili wakulima wa zao hilo wainuke kiuchumi.

KAGASHEKI: Ufisadi halmashauri ushughulikiwe
Naye mgombea  ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Balozi Hamis Kagasheki, alimuomba Dk. Magufuli kushughulikia ufisadi uliopo katika halmashauri nyingi nchini.

Kaghasheki alitoa ombi hilo katika mkutano huo wa kampeni jana.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s