Vyama vitano taabani

Baadhi ya wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Baadhi ya wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Dar es Salaam. Wakati CCM, Chadema na ACT- Wazalendo vikisema vitajitahidi kubana matumizi ya shughuli za Uchaguzi Mkuu yasivuke kiwango cha Sh17 bilioni kilichowekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, vyama vingine vitano vinalia ukata.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, ofisi hiyo ilitoa waraka kutaka vyama vya siasa visitumie zaidi ya kiwango hicho katika kugharimia shughuli zao za kampeni zao, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Waraka huo uliochapishwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 325, ulipongezwa na vyama vya CCM, Chadema na ACT Wazalendo ambavyo vilisema ni sheria nzuri ambayo itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha na kuepusha tabia ya wagombea kununua demokrasia.

Ukiacha ACT – Wazalendo, vyama vya CCM, Chadema na CUF vinapata ruzuku kutoka serikalini inayotokana na matokeo ya uchaguzi wa Rais na wabunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010. CCM pia inamiliki vitega uchumi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na majengo na viwanja vya michezo. Vyanzo vingine vya fedha vya vyama hivyo ni vyama rafiki kutoka nje ya nchi, wahisani na michango.

UPDP
Wakati vyama hivyo vikitoa kauli hiyo, viongozi wa UPDP, ADC, TLP, NRA na Chaumma wamesema hali ya fedha ni ngumu kiasi cha kufanya kampeni zao kusuasua. “Bado hatujazindua kampeni zetu ila tuko kwenye maandalizi… Chama chetu hakina wafadhili wala hatuna usaidizi kutoka serikalini, kwa hiyo tunategemea nguvu za wanachama,” alisema Mwenyekiti wa UPDP, Fahmy Dovutwa.

Dovutwa, ambaye pia ni mgombea urais, alisema: “Fedha imekuwa changamoto. Katika kipindi hiki huwezi kufanya kampeni kama huna fedha. Kutokana na changamoto hizo tumelazimika kupanga idadi ya mikutano tutakayoweza kufanya kwa kipindi kifupi.”

Hata hivyo, alisema licha ya kushindwa kuzindua kampeni zake kitaifa, baadhi ya wagombea ubunge na udiwani katika majimbo na kata mbalimbali nchini wanaendelea na kampeni.

Dovutwa, ambaye katikati ya uchaguzi wa maka 2010 alitangaza kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, akiwa na vyama vingine visivyo na wabunge, alieleza kuwa uzinduzi wa kampeni za UPDP utafanyika wakati wowote wilayani Kilwa na kufuatiwa na mikutano mingine itakayofanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Njombe, Iringa, Dodoma, Singida, Tabora, Simiyu, Geita, Mwanza, Kigoma, Musoma, Pwani na Dar es Salaam.

“Wakati nikiwa kwenye kampeni katika mikoa hiyo, mgombea mwenza (Ahmed Mohamed Ibrahim), naye atakuwa akifanya kampeni katika mikoa ya Bukoba, Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Zanzibar,” alisema. UPDP imesimamishwa wagombea 60 wa ubunge na madiwani katika kata mbalimbali nchini.

NRA
Ukata huo pia umeelezwa kukikumba Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) ambacho mgombea wake wa urais, Janken Kasambala alisema analazimika kujigharimia kwa kuwa hana mfadhili. “Wanasema tusitumie zaidi ya Sh17 bilioni wakati sisi bajeti ya Sh2 bilioni imekuwa tatizo,” alisema na kuongeza kuwa amekuwa akisaidiwa na ndugu, jamaa na marafiki katika kampeni.

Hata hivyo, mgombea huyo alisema licha ya changamoto hiyo, chama chake kinaendelea na kampeni kwa mtindo tofauti: “Wakati vyama vingine vinafanya kampeni majukwaani, sisi tumeamua kuanza kwa mtindo wa man to man (mtu kwa mtu). Tunaonana na wananchi, tunazungumza nao na kufahamu changamoto zao. Vilevile, tunatumia nafasi hiyo kuomba kura,” alisema.

Alibainisha kuwa aina hiyo ya kampeni inafanyika kwa awamu ya kwanza ya kampeni inayoishia Septemba 25. Alisema awamu ya pili itaanza Septemba 27, wakati chama hicho kitakapofanya kampeni majukwaani hadi siku ya mwisho kabla ya uchaguzi Oktoba 25.

Aliitaja baadhi ya mikoa kitakayofanya kampeni kuwa ni Mbeya, Kigoma, Tabora, Kagera, Mtwara, Tanga na Morogoro. Mgombea huyo wa urais, ambaye hakuwa na mpinzani katika nafasi hiyo ndani ya chama, alisema NRA ina wagombea 35 wa ubunge na madiwani 122.

TLP
Hali kama hiyo ya ukata imekikumba pia Chama cha Tanzania Labour (TLP). “Kama huna wafadhili ni kazi kubwa kufanya kampeni kwa sababu chama chetu kinapata ruzuku ndogo na ukweli ni kwamba zoezi la kampeni lina gharama sana,” alisema Katibu Mkuu, Nancy Mrikazira.

Lakini, licha ya changamoto hiyo, Mrikazira alisema kampeni zinaendelea katika mikoa mbalimbali nchini. Mrikazira, ambaye anagombea ubunge wa Jimbo la Temeke, alisema TLP imesimamisha wagombea 30 na madiwani ambao alisema idadi yake haikumbuki.

ADC
Lakini chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimejifariji kuwa tatizo la fedha ni kwa vyama vyote. “Hata hao (vyama vinavyosema vitajitahidi kupunguza matumizi) wanaosema hivyo, ukiwauliza watakwambia jinsi suala la fedha lilivyo gumu,” alisema Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Uendeshaji na Utawala wa ADC, Jumanne Magafu.

Alisema fedha katika uendeshaji wa kampeni ni changamoto kubwa kutokana na kwamba zinahitajika katika kila kitu. “Hata kufikia hiyo Sh17 bilioni ni kazi kwa sababu hiyo si hela ya mchezo,” alisema.

Hata hivyo, alisema mgombea urais wa ADC, Chief Yemba wagombea ubunge 65 na wagombea udiwani 100 wanaendelea na mchakato wa kuomba kura kwa wananchi.

Chaumma
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) pia kilikuwa na mtazamo tofauti kuhusu ukata wa fedha kwa vyama vinavyoonekana kuwa vidogo.

“Changamoto iliyovikumba vyama vingi vidogo, imekuwa neema kwa vyama vikubwa kwa kuwa vinaendelea na kampeni na kupata watu wengi,” alisema Katibu Mwenezi wa Chaumma, Eugene Kabendera.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s