Maalim aahidi mafuta, gesi ndani ya siku 100 Zanzibar

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika mkutano wa hadhara Kisiwani Pemba
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika mkutano wa hadhara Kisiwani Pemba uliofanyika Tibirinzi Mko wa Kaskazini

Na Salma Said, Pemba
Zanzibar: Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi katika siku mia za mwanzo za uongozi wake atahakikisha anafunga mikataba na makampuni ya mafuta na gesi asilia ili kuweza kuchimbwa katika ardhi ya Zanzibar.

Maalim Seif ameyasema hayo jana katika viwanja vya Tibirinzi Mkoa wa Kusini Pemba alipokuwa akizungumza na wananchi na wafuasi wa wa vyama mbali mbali vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika muendelezo wa uzinduzi wa kampeni ambayo kwa upande wa Unguja ilizinduliwa juzi katika viwanja vya Kibanda Maiti.

Amewaomba wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wampe ridhaa ya kuongoza nchi ili aweze kuwaletea wananchi maendeleo na katika kipindi chake cha uongozi siku zake mia ndizo atakazoweza kuonesha mabadiliko mbali mbali ya uongozi wa nchi.

“Katika siku zangu mia za uongozi wangu nakuhakikishieni wananchi iwapo mtanichagua niwaongoze basi ni kuinua uchumi wa nchi yetu kwa kuitisha makampuni ya gezi na mafuta ili nchi iweze kuwa uwezo tusiwe tunategemea misaada peke yake na mimi naamini hilo linawezekana” alisema Maalim Seif.

Alisema katika uongozi kunahitaji kuchapa kazi na kuwa na dhamira ya kwlei ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kutandika misingi ya utawala bora, haki na demokrasia na yakiwezekana hayo basi hakuna jambo ambalo linashindikana kwani wananchi watakuwa na moyo wa kujitolea katika kuendeleza nchi yao.

“Mimi naamini hakuna linaloweza kushindikana kwa uwezo wa Mwenyeenzi Mungu na tabia ya wananchi wa Visiwa wanakuwa na uchungu na wivu na nchi yao, naamini hakuna Mzanzibari asiyeipenda nchi yake naamini hakuna mzanzibari asiyeumwa na nchi yake, hakuna Mzanzibari asiyekuwa na wivu na nchi yake, na hiyo ndio tabia ya nchi za visiwa wanakuwa na wvu kama mtu mume kwa mkewe ” alisema Maalim huku akishangiriwa kwa kutaja wivu wa mume na mke.

Maalim Seif amesema Chama Cha Mapinduzi wamewasaliti wazanzibari kwa kushindwa kuwatetea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kutengenezwa kwa katiba mpya ambapo alisema walipokwenda Dodoma wamesahau kero na shida zao walizozipta kwa muda wa miaka 50 na badala yake wamenyamaza kimya na kuungana na watu wasioitakiwa mema Zanzibar.

“CCM kwa kweli walitusaliti wazanzibari kwa sababu wamekwenda kutengeneza katiba mpya lakini kufika kule wameufyata kabisaaaa! Sawa sawa…badala ya kuwatetea wazanzibari wamekwenda kusahau yote na wakaungana na wale watu wasioitakia mema Zanzibar wakaupitisha mfumo wa serikali mbili ambayo ni mbaya zaidi jee watu hao wanafaa kurudi jee wanastahiki hawa kurudishwa tena madarakani” alihoji Maalim Seif na kuitikiwa hapata hawapaswi kurudishwa tena.

Aidha Maalim Seif alisema katika utawala wake akipewa nafasi atahakikisha anatandika misingi ya utawala bora, atapambana na rushwa kwa kuwadhibiti na kuwashughulikia wala rushwa, kuinua uchumi kwa kushughulikia suala la bandari huru ili kuinua wafanya biashara wafanye biashara zao kwa uhuru na urahisi zaidi kuliko walivyo sasa.

Alisema hali hiyo watakaoweza kuirejesha Zanzibar katika hali nzuri ya uchumi na mambo mengine yote ni viongozi wa UKAWA peke yao hakuna wengine ambao wana uchungu na nchi yao kwa sababu wameshindwa katika kipindi chote cha uongozi kuoneshwa kwamba wana dhamira ya kweli kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo Mansoor Yussuf Himid ambaye ni mshauri wa Maalim Seif alisema wazanzibari wana hamu ya kupata kiongozi ambaye atajali utu, haki na usawa huku suala la umoja, upendo na mshikamano likiwa ni jambo la laazima kwake.

“Tunampata kiongozi ambaye anajua na kuheshimu utu wa mtu atakayewaunganisha wazanzibari wote bila ya kujali dini, kabila wala rangi ambaye jambo la kuwaunganisha watu hilo ni jambo la lazima kwake na mimi naamini ndani ya nafasi yangu kwamba mtu huyo sio mwengine zaidi ya Maalim Seif kwa hivyo namuombea kura zenu muome ridhaa ili atuongoze katika usawa” alisema Mansoor huku akishangiriwa.

Amesema Zanzibar pamoja na utajiri wake ulipo lakini hakuna ajira na ajira zilizopo ni zile za mahoteli tu na ajira nyengine ni za vikosi vya SMZ ambazo hutolewa kila inapokaribia uchaguzi lakini ukimalizika uchaguzi vijana hao hutupwa.

“Ajira tulonazo ni mahotelini tu sasa vijana wangapi watafanya kazi hoteli kwani tuna hoteli ngapi? Alihoji Mansoor  na kuongeza kwamba ajira zinazotolewa kwa wingi ni zile za vikosi ambazo hutolewa wakati wa uchaguzi na ukimaliza uchaguzi vijana hao hutimuliwa.

Akizungumzia suala la Mapinduzi Mansoor kama kawaida yake amesema malengo ya Mapinduzi yamedharauliwa na watawala na badala yake wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwadhalilisha wananchi jambo ambalo halipaswi kuendelezwa na serikali ijayo.

“Ukimuona Askari unasema Alhamdulillah maana unajua upo katika mikono salama lakini sasa hivi ukimuona Askari unajenga khofu kubwa unaogopa tunauliza tumekosa nini hata polisi muendelee kutudhalilisha? jua umeshaingia katika balaa”.

Ismail Jussa Ladhu ni Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma amesema katika kitu ambacho walichojichanganya na kujiharibia kukosa wafuasi wengi CCM ni tabia yao ya kutapatapa katika kutaka kukata majimbo ambapo amesema wamezidi kujichanganya.

“CCM wamechanganyikiwa walijifungia ndani wakakata mipaka ya majimbo lakini ndio wamejiharibia zaidi maana ndio watakosa kabisa hayo majimbo walioyafikiria na mimi niliwaambia kwamba Kashata wakate mkato watakaoutaka lakini kashata utemu wake upo pale pale”  alisema huku akipongezwa kwa makofi.

Jussa alisema Unguja kuna majimbo 36 lakini aliwaahidi wananchi kwamba majimbo 18 ni majimbo hayo yatakwenda kwa Chama Cha Wananchi (CUF) na majimbo ya Pemba yote 18 yatarudi CUF kama kawaida hivyo amewataka wananchi wahakikishe wanawapa kipigi kikali CCM mwaka huu.

“Nataka niwahakikishie wananchi wa Pemba nyinyi mtatupa majimbo 18 lakini na sisi tutawarudishieni majimbo 18 tunataka tuwatie adabu kubwa hawa CCM mwaka huu maana waone khasa jinsi walivyojichanganya” alisema Jussa.

Kabla ya kumkaribisha Meneja kampeni, Hamad Masoud Hamad alisema watahakikisha ushindi wa Maalim Seif ni wa asilimia 90 hadi 95 kwani kazi kubwa inafanywa na vijana ambao wamepewa kazi ya kumtafutia Maalim kura nyumba hadi nyuma mtaa hadi mtaa.

Alisema vijana hao hivi sasa wameshafika 4700 kwa upande wa Pemba na wanafanya kazi kubwa sana ya kuwachota vijana wenzao na kuwabadilisha ili wajiunge na CUF kwa kuwaelimisha kwani baadhi ya vijana walikuwa hawajajishirikisha bado na siasa hivyo kazi inayofanywa na vijana hao ni kubwa ambao wamekusudia kutaka kuleta mabadiliko ya kweli.

Hamad alisema katika vitu ambavyo ni ghali zaidi ni elimu na wazee huwa wanapoteza fedha nyingi kwa ajili ya kuwasomesha vijana wao ili wamalize masomo waajiriwe lakini matokeo yake wanamaliza kusoma hawapati ajira yoyote.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu katika jambo ambalo hapa kwetu ni ghali na gumu ni elimu mtu anapoteza kila kitu chake katika kumsomesha mwanawe anauza kila alichonacho ili amsomeshe mwanawe lakini matokeo yake unamaliza kusoma licha ya gharama zote ulizolipa lakini hakuna ajira kwa hivyo vijana hawa wanahitaji ajira” aliongeza Hamad.

Akimkaribisha mgeni rasmi wa shughuli hiyo Kampeni Meneja Nassor Ahmed Mazrui alisema Zanzibar ni kitovu cha biashaara lakini kilichokosekana ni mazingira mazuri na kukosekana kwa mipango thabiti ya kuweza kuinua biashara lakini chini ya uongozi wa Maalim Seif atainua uchumi na kuweka mazingira bora ya wawekezaji.

Aliwaambia wananchi kwamba huu ni wakati wa mabadiliko hivyo watambue kwamba kuna jahazi linaondoka na nahodha wake ni Mheshimiwa Edward Lowassa na Maalim Seif na wawahi kuingia katika jahazi hilo la Nuhu atakayechelewa basi ameshindwa kuyaona mabadiliko.

Mkutano huo ulipambwa na shamrashamra za ngoma za utamaduni mbali mbali ambazo ziliwavutia watu wengi na kujikuta wakiingia uwanjani wakicheza.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s