Nchi sasa gizani siku saba

tanesco1Shirika la umeme nchini (Tanesco), limetangaza nchi kuingia ‘gizani’ kwa wiki nzima kuanzia leo kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya gesi inayozalisha umeme kutoka Songosongo na kuanza majaribio ya gesi ya Mtwara.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchism Mramba, aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kutembelea mtambo wa Kinyerezi I, kuwa sasa Watanzania wategemee umeme wa uhakika baada ya kuanza kuzalisha umeme kwa gesi ya Mtwara.

Alisema tayari gesi imeanza kuingia kwenye mtambo wa Kinyerezi I na Ubungo II na kwamba kinachofanyika sasa ni majaribio ya kusukuma mitambo ya Ubungo II na Symbion kwa ajili ya uzalishaji.

“Kwa hiyo kesho (leo), tutazima mitambo yote ya gesi ya Songosongo ili kuanza kazi ya kuunganisha bomba la gesi kutoka Mtwara…wakishaunga, kutakuwa na kazi ya kufanya majaribio ya hapa na pale, kazi ambayo tunategemea itachukua kama wiki moja hivi,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Wananchi wamekuwa wakifuatilia sana umeme, lakini niwaambie tu kuwa tutaendelea kuwa na tatizo hadi Septemba 15 kwa sababu tunataka kuingiza kitu kipya, lakini tunategemea baada ya wiki moja, umeme utaongezeka zaidi.”

Alisema hali ya umeme kwa siku ya leo itakuwa mbaya zaidi kwa kuwa ‘mitambo yote itakuwa imezimwa.’

Alisema kazi ya kuunganisha bomba hilo itaihakikishia nchi kuwa na umeme wa uhakika hata kama mabwawa ya maji yanayotumiwa kuzalisha umeme yatakuwa yamekauka.

Alisema gesi ya Mtwara inategemewa kuendesha mtambo wa Ubungo II wenye uwezo wa kuzalisha MW 105, Symbion (MW 112) na Kinyerezi I (MW 150)

Mramba alisema mtambo wa Ubungo I utaendelea kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya Songosongo na kwamba Ubungo II inatumia gesi ya Mtwara kwa kuwa inatosha kuendesha mitambo hiyo.

Alisema hadi jana, mafundi walikwisha unganisha bomba la gesi kutoka Mtwara na kituo namba 15 Ubungo tayari kwa kuanza uzalishaji

Kwa mujibu wa Mramba, mikoa itakayoathirika ni yote inayopata umeme wa Gridi ya Taifa ukiwamo Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Dk. James Materegeo, alisema mchakato wa kuchukua gesi kutoka mitambo ya Madimba mkoani Mtwara imekamilika juzi na kazi inayofanyika ni ya majaribio.

Alisema juzi, TPDC ilianza kusukuma gesi kutoka Mtwara hadi Kinyerezi I kwa mgandamizo wa 3 (3 bar) na kwamba ili uzalishaji wa umeme ufanyike kwa uhakika, mgandamizo huo unatakiwa kufikia 50.

“Kuanzia leo hadi kama wiki moja hivi tutakuwa tumefikia mgandamizo wa 50 unaotakiwa kitaalam,” alisema.

Alisema uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi ya Mtwara utaisaidia serikali kuokoa takribani Dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka ambazo zilikuwa zinatumiwa kununua mafuta mazito ya kuzalisha umeme.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

2 Replies to “Nchi sasa gizani siku saba”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s