Wasomi wamshukia Mkapa kwa kauli za kuudhi

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akihutubia umati wa wafuasi wa CCM waliohudhuria ufunguzi wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Jangwa, Dar es Salaam
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akihutubia umati wa wafuasi wa CCM waliohudhuria ufunguzi wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Jangwa, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Siku moja baada ya ufunguzi wa kampeni za CCM, wasomi na wananchi wamesema kauli ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa wanaosema wanataka kuikomboa Tanzania ni “wapumbavu na malofa” haikustahili kutolewa na kiongozi huyo.

Katika ufunguzi huo, Mkapa alisema wapinzani wanaodai  vyama vyao ni vya ukombozi ni wapumbavu na malofa kwa  kuwa Watanzania walikwishakombolewa na ASP na Tanu na kwamba chama pekee cha ukombozi kilichobaki sasa ni CCM.

Profesa wa Uchumi katika Kilimo wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), Damian Gabagambi alisema kauli kama hizo zinatokana na mabadiliko yanayoonekana kwenye siasa za Tanzania yanayosababishwa na kutimia kwa unabii wa Mwalimu Julius Nyerere kuwa ‘mpinzani wa kweli atatoka ndani ya CCM.’

Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wakubwa wa CCM hawajiamini, wanalazimika kutumia lugha zisizo na staha kupunguza msongo walionao.

“Kuhama kwa viongozi waandamizi kunawaumiza kichwa na huenda hawajui sababu. Wameanza kampeni na matusi na pia, wamechelewa kumaliza mkutano, kwa hali hii watatoa wapi nguvu ya kuwakemea wengine?” alihoji Profesa Gabagambi.

Alishangazwa na kitendo cha polisi kuendelea kutoa ulinzi bila ya kukemea baada ya ufunguzi huo kupitiliza muda wa saa 12.00 unaoruhusiwa na akaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa kauli juu ya suala hilo.

“Walipoteza muda mwingi kwa burudani za wasanii, nilitarajia wangetumia muda ule kutueleza wamefanya nini kwa muda waliokuwapo madarakani na kufafanua walivyotekeleza ilani iliyopita. Kwa mgeni angeweza kudhani kuwa lilikuwa tamasha la burudani,” alisema.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alipoulizwa alisema: “Suala la muda limeainishwa kwenye kanuni, navikumbusha vyama vyote vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi kwa kipindi chote cha kampeni. Mwisho wa kampeni ni saa 12.00 jioni na hili linapaswa kufuatwa na vyama vyote.”

Jaji Lubuva alisema vyama vyote vinatakiwa kuzingatia maadili waliyosaini na kuzungumza mambo yanayohusu sera na ilani zao badala ya kushambuliana na kutoleana maneno ya kuudhi majukwaani.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa alisema: “Nyie Mwananchi mkoje? Shughuli imeandaliwa na CCM, halafu mnataka CCM watoe maoni, inawezekanaje?

Hata alipofafanuliwa kuwa kauli za viongozi hao zimehojiwa na watu mbalimbali alisema, “basi endeleeni na hao.”

Wakati Nape akisema hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Allan Simba alisema kauli hizo ni za woga na zinataka kuwatisha wananchi ili wasiwachague wapinzani.

Aliwataka viongozi hao kutulia na kutoogopa kinachoendelea ili kuwapa wananchi fursa ya kufanya uamuzi juu ya mtu wanayeridhika naye kuwatumikia.

“Kubezana siyo haki na hatutarajii kinywa cha mzee huyu kitoe maneno makali kama hayo ila isingeshangaza kama angeongea vile kijana yeyote kutoka ndani ya chama. Tungejua kuwa baadaye wazee wangemuita na kumkanya ili awe makini zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa ni vyema ushindani ukaelekezwa kwenye hoja ili kujenga demokrasia makini na siasa zenye weledi kwa kuwaacha wananchi wapembue ilani za kila chama.

“Kama upande wa pili nao watajibu kwa matusi haitashangaza kama siku moja itatokea wakashikana mashati,” alisema.

Profesa Milline Mbonile wa UDSM alisema si jambo jema kuzingatia masuala ambayo hayakuwa lengo la mkutano ule badala yake watu waangalie kiini ili wananchi wawe kwenye nafasi nzuri ya kufanya uamuzi.

“Mgombea mwenyewe alizungumza vitu atakavyovifanya ndani ya muda wake wa uongozi,” alisema.

Profesa huyo alifafanua kuwa kwa watu waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), matusi kwao siyo hoja kwani walishayazoea na kueleza kuwa anayaona kuwa ni masuala mdogo madogo ambayo hayapaswi kuzingatiwa na kuacha hoja kuu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Jesse Angowi alieleza kusikitishwa na maneno hayo ya jazba ambayo hayakustahili kutamkwa na Mkapa.

“Ukawa inao wafuasi wengi tu kama ilivyo CCM. Mheshimiwa Mkapa amesema kwa jazba na kwa kweli kama kanisa ametusikitisha kutoa maneno ya kashfa,” alisema.

Wakili Peter Shayo alisema kauli ya Mkapa ni uvunjaji wa wazi wa kanuni za kampeni zinazowataka wagombea na mawakala wao kutumia lugha ya kistaarabu.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s