Makada wakubwa na anguko lao 2015

Mahadhi Juma Maalim na Mohamed Seif Khatib (juu), Balozi Seif Ali Idd na Yahya Kassim Issa (chini)
Mahadhi Juma Maalim na Mohamed Seif Khatib (juu), Balozi Seif Ali Idd na Yahya Kassim Issa (chini)

TUNAPOULIZANA sababu “hasa” za anguko la makada wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura za maoni za kutafuta uteuzi wa kugombea uwakilishi na ubunge majimboni Zanzibar, muhimu kwanza tukumbushane ukweli kuwa kisiasa, CCM imo ndani ya tanuri la moto.

Hali ya chama hiki ni mbaya. Tena, baada ya hali mbaya hiyo kuzoeleka upande wa Zanzibar, safari hii ugumu umehamia na kuzama katika siasa za Tanganyika, upande ambao upinzani dhidi ya CCM, umekuwa na mitihani mingi.

Tanganyika ni nchi kubwa kieneo na kwa idadi ya watu wake. Haiwezi kwa namna yoyote ile kupimika kwa hayo mawili, na ilivyo Zanzibar. Hata kisiasa, haijapata hasa ushindani wa maana ulioshughulisha serikali iliyopo madarakani kulinganisha na Zanzibar.

Ushindani mkubwa wa kisiasa umezoeleka Zanzibar kwa miaka ya historia ikijumuisha nyakati za harakati za kutafuta uhuru zilipokuwa hai, ndio umedhihirika kipindi tulichopo.

Nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umoja wa vyama vinne vya siasa, kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF) kinachonyima usingizi viongozi wenye mamlaka Zanzibar, haishindiki kirahisi.

Ile nguvu iliyoanzia wakati wa Bunge Maalum la Katiba, hata kulevya CCM kusaka kura za kishetani ili kupitisha Katiba Inayopendekezwa, hakuna namna inaweza kudhoofishwa sasa taifa linapokabiliwa na uchaguzi mkuu.

Sasa katika mwelekeo huohuo, wapo wakubwa waliopigwa dhoruba Zanzibar katika dhamira yao ya kutaka kuendelea kushikilia viti majimboni, kwa nafasi ya ubunge na uwakilishi.

Baada ya kutafuta wajipange vipi kwa kuwa baadhi yao ‘walitengenezewa’ majimbo ili kutarajia ushindi wa ‘tsunami’ dhidi ya CUF-Ukawa, hatua iliyosababisha wengine kulazimika kubanana wenyewe kugombania majimbo waliyorudi baada ya walimokuwa kuvunjwa au kuvurugwa, bado walipigwa kumbo.

Bali hata wale waliotangazwa kushinda kura ya maoni, wanaendelea kubakia hivyo ndani ya shutuma na lawama za kufanya hila washinde.

Ndio kusema kwamba hizo hila, huko kutengenezewa majimbo kifisadi na kishikaji, kunathibitisha wanachokijua wengi – hali ngumu ya mustakbali wa CCM katika siasa za jamhuri yetu.

Wakubwa wanatemwa. Wengine wamekosa kura majimboni walikoota mizizi na kujipa ufalme, wengine wakaoneshwa mlango wa kutokea. Ah, wengine wamenunua kura kwa lazima – rushwa na mipango ya uchafuzi wa taratibu za chama.

Kwa wakubwa waliokosa kura majimboni, khabari ni kubwa kuwahusu. Hawakuwajibika kwa wapigakura na wananchi, hawakutimiza ahadi walizotoa katika kuomba kura, waliendeleza jeuri na kiburi, wengine wakisema wazi, “nimeshinda kwa pesa zangu.”

Kama vile hayo yote ni mzaha, wapo walioshinda kwa nguvu tu ya mamlaka waliyonayo. Baadhi ya hawa, ni viongozi chamani na serikalini, wanasauti na wakaitoa sauti kulazimisha wapigiwe kura. Sio kulazimisha wapigiwe, basi kulazimisha kura zao zitoshe iwe isiwe.

Wakubwa wawili-watatu kwa kujua mapema kuwa hawatopata ridhaa ya wana-CCM, walijenga mazingira ya vitisho vya kila namna. Ndio, yupo aliyeulizwa alfajiri, “unatoka chama gani tusichokijua.”

Alipojibu wananchi ni “chama hichohicho chetu cha enzi CCM,” akaambiwa “basi rudi usirudi hapa mpaka uje na mtoto wetu Sheikh Mselem bin Ali.” Nguvu ya hoja yao wananchi wakaijenga kwa kusema, “mtoto wetu mpendwa ambaye unajua vizuri mmempeleka wapi.”

Viongozi wa mkoa wa Kaskazini, Unguja, wamepata shida isiyo na kifani. Kila walipojitokeza kuomba wakubaliwe waje kugombea, walikutana na hoja zilizohusu kadhia ya kukamatwa na kufungwa gerezani Dar es Salaam kwa mashekhe wa Kizanzibari wakiongozwa na Sheikh Mselem, mzaliwa kindakindaki wa Donge, jimbo ambalo nalo limefumuliwa kwa kumegwa baadhi ya maeneo yake na kupelekwa jimbo la Tumbatu.

Tumbatu ndiko ambako Haji Omar Kheri, waziri katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar (Tawala za Mikoa na Vikosi vya kiaskari vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar), amewekeza kwa vitisho na kupandikiza chuki miongoni mwa wananchi.

Imemegwa kaskazini na kusini: maeneo ya kaskazini yakasogezwa kuimarisha ngome ya kulazimisha ya Kheri jimboni Tumbatu, na yaliyo kusini yakatengeneza jimbo ‘nchekea’ kwa ajili ya Balozi Seif Ali Idi, Makamu wa Pili wa Rais, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM.

Huyu Balozi amemaliza kuwa mbunge wa Kitope, jimbo lililovunjwa na maeneo yake kusogezwa kuunda hilo jipya la Mahonda ambalo wachambuzi wanaamini ametengenezewa, ingawa atakabiliana na ushindani mkubwa wa CUF-Ukawa.

Balozi ameamua safari hii kugombea uwakilishi, baada ya ‘labda’ kuona ni vema akabakia Zanzibar na kuimarisha siasa ndani ya Baraza la Wawakilishi, ambamo kwa mara ya kwanza ameshiriki kwa karibu zaidi alipoteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais.

Alipata wadhifa huo baada ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein kumteua kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM wakati wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ulipomalizika uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Jimboni kwa Balozi kumetokea tafrani ambayo mpaka sasa haijaelezwa fawahisha. Wala hakuna katika wakuu wa chama aliyethubutu kueleza ni nini hasa kimetokea wakati wa kura ya maoni.

Saa kadhaa wakati wananchi wakitarajia matokeo ya kura yawe hewani, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, alinukuliwa akisema, “tunaendelea kufuatilia kilichotokea na hatuna hakika kama itabidi uchaguzi urudiwe.”

Walioko ndani, wanadai ushindi wa Balozi ulitatizika ikihofiwa kulikuwa na ‘rafu’ mchezoni huku jina la mtaka uteuzi wa ubunge, Makame Mshimba Mbarouk, likitajwa kama “damu ya kunguni.”

Hakuna uthabiti kwamba viongozi hawa hawapikiki chungu kimoja siku hizi, lakini pia sina hakika ni nini hasa kilichomsukuma Balozi kugeukia uwakilishi badala ya ubunge.

Mshimba amepigwa kumbo katika kura, kama ilivyotokea kwa makada wakubwa Muhammed Seif Khatibu (Uzini), Yahya Kassim Issa (Chwaka), Mahadhi Juma Maalim (Muyuni), Mohamed Chombo (Magomeni), Waride Abubakar Wakati (Kiembesamaki), Abdalla Sharia Ame (Dimani) na Pereira Ame Silima (Chumbuni).

Kati ya hawa waliopigwa kumbo, wamo waliosaliti wananchi kwa ama kutotimiza ahadi walizotoa wakati wakiomba ridhaa, au kwa kutojishughulisha kamwe na kusaidia mipango ya maendeleo ya watu jimboni. Wengine wanatajwa kama viongozi jeuri na wenye kiburi wakitamba kuwa waliutafuta ushindi kwa pesa zao.

Baadhi yao wanajulikana wamepata mafanikio kimaisha kwa kuwa viongozi wawakilishi wa wananchi, lakini wamewekeza zaidi Tanganyika, na kusahau kwao au angalau kuwakumbuka wananchi waliowachagua Zanzibar.

Ipo kadhia kubwa zaidi iliyohusika katika kukataliwa kwa wakubwa wa CCM Zanzibar – kupitisha Katiba Inayopendekezwa isiyoyatazama maslahi ya kweli ya Zanzibar na hili linaloendelea kuumiza roho za Wazanzibari la kuwakamata na kuwafunga bila ya hukumu masheikhe wapatao 20 wa Zanzibar.

Na mambo hayo mawili ya mwisho, yataendelea kubakia kama “mambo muhimu” yanayotarajiwa kukitupilia mbali Chama Cha Mapinduzi kutoka kilele cha madaraka katika Jamhuri yote.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s