Kikwete: Wapinzani wataisoma namba

Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli na Mgombea wake mwenza, Samia Suluhu Hassan wakiwa kwenye gari wakisindikizwa na wafuasi wa chama hicho walipokuwa wakitoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua fomu, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli na Mgombea wake mwenza, Samia Suluhu Hassan wakiwa kwenye gari wakisindikizwa na wafuasi wa chama hicho walipokuwa wakitoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua fomu, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan jana walichukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku Rais Jakaya Kikwete akisema wapinzani wataisoma namba.

Ofisi ndogo za makao makuu ya CCM zilizoko Lumumba na za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilifurika mashabiki waliovalia nguo za rangi ya njano na kijani, ambazo hutumiwa na chama hicho, huku wakazi wengine wanaofanya kazi au kuishi maeneo jirani na barabara za Morogoro, Bibi Titi na Ohio, wakilazimika kusimamisha shughuli zao kwa muda kushuhudia msafara wa wagombea hao ukipita.

Walinzi  wa ofisi za NEC walilazimika kufanya kazi ya ziada kudhibiti wafuasi wa CCM waliosindikiza wagombea hao kutoka ofisi ndogo za CCM kabla ya msafara huo kuondoka baada ya wawili hao kuchukua fomu, kurejea Lumumba, ambako mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliupokea.

“Wakwere wanasema chihendo na mwene mwana, yaani shughuli na mwenye mtoto,” alisema Rais Kikwete mara baada ya msafara kuwasili akieleza sababu za yeye kuwapo eneo hilo kwa kutumia maneno ya shughuli za kitamaduni za jandoni, unyagoni na mkoleni za kabila la Wakwere.

“Nimekuja hapa kujiridhisha kama kweli fomu zimechukuliwa. Na kweli nimeziona. Baada ya hatua hii wale wanaodhani kuwa CCM ni chama cha mchezo mchezo, wataisoma namba.”

Huku akikatiza hotuba yake kwa kuitaka bendi ya TOT ya chama hicho kuimba wimbo wa “Shangilia Ushindi Unakuja”, Rais Kikwete alisema kwa kuwa yeye ni baba alilazimika kuja kuangalia kama mwanaye ametekeleza alichotuma.

Kikwete, ambaye alitumia mifano iliyovunja mbavu wafuasi hao, alirusha kijembe kwa wanachama walioihama CCM akisema ni tamaa na kuahidi kufanya mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni.

“CCM shangilia ushindi unakuja, tena ushindi wa uhakika na si wa wasiwasi. Baada ya hapa kitakachofuata ni uzinduzi hapo Agosti 22 kwenye mkutano utakaotisha. Hatumwi mtoto siku hiyo, unakuja mwenyewe,” alisema.

“Watu wanasumbuliwa na tamaa na wakati mwingine ni tamaa iliyopitiliza kutaka madaraka.”

Magufuli alitoka ofisi ya CCM Lumumba akiwa amepanda gari aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa wazi juu akiwa na msafara wa magari yapatayo 10 kuelekea ofisi za NEC. Baada ya kufika eneo la makutano ya Barabara ya Ohio na Bibi Titi, alishuka na kupanda gari nyingine iliyokuwa wazi nyuma na kuamsha kelele za shangwe.

Aliwasili ofisi hizo saa 5.22 asubuhi na baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, msafara wa kurejea ofisi za chama hicho zilizoko Lumumba ulianza tena na kufika ofisi hizo ndogo za CCM, ambako ulipokelewa na Rais Kikwete.

“Matatizo ya Watanzania nayajua na  ninaahidi kuwa nitakuwa mtumishi wenu mtiifu,” alisema Dk Magufuli baada ya Rais Kikwete kumuomba aketi ili azungumze na wafuasi wa chama hicho.

“Nafahamu kuwa Watanzania wanahitaji ajira na hawataki usumbufu kwenye biashara zao kama mamantilie, wana kero kwenye huduma mbalimbali. Ninawaahidi kuwa nitazishughulikia.

“Napenda nimhakikishie mwenyekiti na wananchi mliokusanyika hapa kuwa CCM itashinda na wala simuoni mtu wa kutushinda. Nashukuru kwa moyo mliouonyesha wa kunisindikiza mimi pamoja na Samia. Mmetoa jasho na mmepoteza muda wenu. Napenda kuwahakikishia kuwa muda wenu hautapotea bure.”

Alirudia wito wake wa kuwataka wananchi kuendeleza mshikamano uliopo bila kujali itikadi zao wala makabila ili kuliletea Taifa maendeleo kwa kuondoa kero zinazowakabili.

Kama ilivyo kawaida yake tangu apitishwe kuwania urais, Dk Magufuli alisalimia kwa lugha za makabila zaidi ya kumi na kubainisha kuwa lazima wenyewe watakuwapo, hivyo ni vyema wakaendelea kuishi kwa mfumo huo uliojengwa kwa muda mrefu. Wakati akieleza hayo, mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwenye harakati za kujikomboa kiuchumi. “Kwa umati huu uliopo hapa kwanini tusipate ushindi wa kishindo?

Niwaambie wanawake wenzangu mliopo hapa, nimepata ujumbe kutoka kwa wanawake wasio wana-CCM na wamenieleza kuwa wanatuunga mkono,” alisema Samia, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba.

Alisema anawasikitikia makada kadhaa  wa  chama hicho wanaoendelea kutangaza kujiunga na upinzani huku, akisema wanachokifanya ni sawa na kupoteza malengo kwani wamechagua fungu la kukosa.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s