Mauzauza kura za maoni CCM

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa kura za Moniwa Kta ya Kisukulu B,Christopher Masinde akionyesha kadi ya mpigakura halali kwa wajumbe wa mkutano huo jana wakati wa kuhakiki majina kabla ya kupiga kura kuchagua wagombea udiwani na ubunge kwenye jimbo la Segerea ,Dar es Salaam
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa kura za Moniwa Kta ya Kisukulu B,Christopher Masinde akionyesha kadi ya mpigakura halali kwa wajumbe wa mkutano huo jana wakati wa kuhakiki majina kabla ya kupiga kura kuchagua wagombea udiwani na ubunge kwenye jimbo la Segerea Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mauzauza jana yalitawala mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM kutokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa, vurugu, kura kuchomwa moto, makada kukamatwa, wanachama kutoruhusiwa kupiga kura na kugundulika kwa karatsi zilizokwishapigwa kura.

Kwenye baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na vifaa kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo zimeshapigwa kura zikiwa ndani ya maboksi.

Lakini matukio yaliyotawala kura za maoni ni makada kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura.

Dar es Salaam

Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Takukuru inawashikilia wagombea sita kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye kura za maoni.

Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Denis Manumbu aliwataja waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba, Denisi Kalela, katibu wa itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu wa Goba, Rehema Luhanja,

Wengine ni mwenyekiti kata ya Goba, Pili Mustafa, mgombea udiwani, Msigani Mwasha na Eliasi Nawera ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe.

Alisema kuwa Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00 usiku maeneo ya Kibamba CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba Kati na Kawe.

“Walikamatwa wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa wakiwa na kiasi cha pesa ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine wakiwashawishi wajumbe kupokea rushwa,” alieleza Manumbu.

Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24 ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa.

Kondoa

Lakini hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika kuchoma moto makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa baadhi ya wanachama walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha kupigia kura.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu, mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya, Nyantora walikubaliana kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo.

Hatua hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa vitambulisho vya kura havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi ya wanachama 200 walikuwa wamepiga kura hizo.

Maboksi hayo yalichomwa mbele ya kituo cha kupigia kura cha Ubembeni na kushuhudiwa na wananchi, wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa CCM.

Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo.

Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote kutawanyika eneo hilo hadi leo.

Awali kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua sanduku lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura

Mbeya

Kashfa ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya ambako mgombea udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi wampigie kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja.

Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia alikwenda kwenye kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura ili awanunulie kinywaji.

Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na Aziza Mbika wa eneo la Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo akitoa fedha na pombe kwa vijana mbalimbali .

Msimamizi wa uchaguzi wa Kituo cha Meta, Ndoni Mwakalukwa alikiri kupokea malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha hizo na kwamba atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura.

Vituo vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda na Sinde, vilikosa wanachama wa kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja kila baada ya saa kupita.

Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na kazi ngumu ya kuwaita watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura kama ni wanachama wa CCM.

“Tatizo ni kwamba vituo vya kupigia kura havijawekewa alama yoyote, hivyo wanachama wengi hawajui,’’ alisema msimamizi wa kituo cha Soweto, Ambakisye Kitunga.

Lindi

Rushwa pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako mbunge wa viti maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za hongo.

Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga.

Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.”

Alipoulizwa kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema: “sijui hawa wanasingizia singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru wa mkoa wa Lindi, Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku Kata ya Mchinga akigawa fedha kwa wanachama.

Chami alisema akiwa ofisi za Takukuru baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alitoa tena Sh780,000 kwa ajili ya kuwahonga maofisa hao ili wasiendelee na suala hilo.

Alisema kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha mahakamani muda wowote baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma zake.

Wakati huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano na Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya Mbanja.

Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.

Shinyanga

Mjini Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga, Ramadhani Majani amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini.

Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari jana kwamba Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya watu waliotilia shaka nyendo zake kwa kitendo chake cha kuongozana na mmoja wa wagombea nyakati za usiku kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna jambo lisilokuwa la kawaida walilopanga kufanya.

Walisema waliamua kuwapigia simu wagombea wengine waliokwenda ofisi hizo na kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa anaongea naye, hata hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM wakijongea ofisini hapo.

“Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na baadhi ya watu wanaoishi jirani na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona katibu kata wetu akiwa na mgombea udiwani pamoja na wapambe wake. Walidai inavyoelekea walikuwa wakipanga mikakati mibovu ya kutaka kuiba kura,” alisema Rashidi Abdalah.

“Taarifa hizo zilitushangaza sana. tuliamua kuchukua gari na kwenda katika eneo la ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea (anamtaja jina) wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani, ghafla walipotuona mgombea na wapambe wake walikimbia na katibu kata aliingia ofisini na kuufunga mlango,” alieleza aliongeza.

Abdalah alidai kitendo cha Majani kukimbilia ofisini kilisababisha baadhi ya watu kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili kumtoa nje na kumshushia kipigo, lakini mgombea

mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza ghasia.

Majani alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba ni kweli muda huo wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri kwenye karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku.

“Nilikuwa naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa watu wanakuja na fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini kwangu,” alisema Majani.

Handeni

Hali ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya Vibaoni wakati zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani kwa maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na badala yake kuamua kupiga kura ya wagombea ubunge.

Wakizungumza jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama hao walisema kuwa walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri, lakini hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau.

Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa walikubaliana kukutana na madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya wanachama haikutimia ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha ajabu wagombea hao hawakutokea hadi jioni.

Arusha

Sakata la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka mkoani Arusha, ambako viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo. Waliokamatwa ni katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa wa Bondeni, Yakub Shaban.

Katibu wa Wilaya ya Arusha, Feruz Bano alisema: “Ni kweli wamekamatwa, lakini tunafuatilia kujua kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo walikuwa wanapeleka karatasi hizo kwenye chumba cha kupigia kura kidogo kidogo,” alisema.

Dodoma

Rafu iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama walikamatwa na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa.

Waliokamatwa na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni katibu wa vijana Tawi la Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia kura, 20 za udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle.

Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia.

Aidha, baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa na makosa. Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni Tambukareli na Kilimani mjini Dodoma.

Katibu wa CCM wa mkoa, Albert Mgumba alisema kata ambazo hazijafanya uchaguzi, kazi hiyo itafanyika leo kabla ya saa 4:00 asubuhi. Kuhusu makada waliokamatwa, katibu huyo alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa wilaya kwa kuwa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, vurugu zimetokea katika tawi la Mji Mpya lililoko Kata ya Uhuru kutokana na baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki wameingia kupiga kura.

“Asubuhi walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna mamluki wanataka kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema msimamizi wa kituo hicho, Mariam Jumbe.

Bukoba

Hali ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya wanachama waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo.

Hali hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata hivyo, katibu wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana kwa majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo.

Pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya watu waliofika kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba waliolalamikia kutoorodheshwa.

Mtwara

Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani.

Wakiongea na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima Nassoro wa Tawi la Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM kuwapa kadi za chama bila kuweka majina yao katika daftari la wapigakura.

“Sisi tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa au la. Nyingine tumezilipia na majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za mwaka 2000 hadi mwaka 1950 zipo na majina yao yapo na sisi majina yetu hayapo kuna nini hapa?” alihoji Aisha

Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga alikiri kuwapo na tatizo hilo, akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi.

Njombe

Pia mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana na kadi zao za uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku ambayo CCM ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya.

Msimamizi wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa alisema licha ya uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama waliokuwa na kazi walizopata baada ya Julai 15.

“Ni kweli kuna baadhi ya watu wanakuja na kadi zao zilizochukuliwa baada ya Julai 18, lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha wameridhika,” alisema Nyadoa.

Pwani

Mchakato kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa baada ya baadhi ya wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya wanachama wa chama hicho.

Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia baadhi ya wanachama walikutwa wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya malipo ya wanachama maarufu badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM.

Kasoro hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura mjini Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro.

Bundala alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya uchaguzi ni Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha. Uchaguzi huo utarudiwa leo.

Alipoulizwa sababu za kuwepo tofauti ya idadi ya majina yaliyomo kwenye daftari la uanachama na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo, alisema wamebaini kasoro hiyo imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili kwenye daftari la chama la wapigakura.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama waliokuwa wakipiga kura Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu katika mchakato wa upigaji kura wakisema baadhi ya matawi yaliweka orodha kubwa ya wanachama wanaoruhusiwa kupiga kura ikilinganishwa na idadi ya awali iliyobandikwa kwenye kuta za ofisi za matawi yao.

Tarime

Mjini Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa hadi leo baada ya kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa zimeshawekewa alama ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na Tarime Mjini.

habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo zinazoendelea kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya, Bernard Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi.

Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni.

Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi.

Alisema kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika vijiji vya Nyamwaga, Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini zimekamatwa Mtaa wa Bomani, Magena na Romori.

Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo, uchaguzi umeahirishwa.

Kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia alithibitisha kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa. Alisema Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya wagombea wawili wa majimbo hayo.

Mwananchi ilipomtafuta Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge wa Tarime, na Waziri Gaudensia Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika na kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao.

Makada wengine wanaowania ubunge wa Tarime ni Christopher Kangoye ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles Machage.

Kwa jimbo jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango, Ditu Manko na Brito Burure.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s