Hii rushwa hatari CCM

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Ali Shein, akizungumza na Wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Ali Shein, akizungumza na Wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar

NIMEKAA nje nyumbani kwangu Zanzibar, jirani yangu akapaisha, “babaake Asma, natoka kupokea pesa mwenzio.”

Huyu bibi hana kawaida ya kuniambia kila kitu. Ingawa sina ugomvi naye, kwa hulka yake, huchagua jambo gani aniambie.

Tu jirani lakini tunaotofautiana mitizamo ya mambo, bila ya shaka kutokana na kila mmoja anavyotumia akili yake. Mimi mambo ya habari chakula changu, anajua; ila kwake habari ni nadra kuzifuatilia.

Lakini labda anajua mambo ya ovyo akiniambia ninayafuatilia. Ndio akaona anieleze yanayotendwa na makada wa Sisiem wanaosubiri matokeo ya kura za maoni kuomba uwakilishi na ubunge Zanzibar.

Anasema watia nia wa chama hicho anachokishabikia kwa roho safi, wanagawa pesa kwa wanachama wao. Ile tu kutafuta kura za kupitishwa na wanachama kugombea, Sisiem wanagawa pesa.

Jirani anafichua siri, “kila mtu anapewa shilingi elfu kumi.”

Nini maana yake? Kama nafasi ya uwakilishi inawaniwa na wana-CCM kumi, kila mgaiwa rushwa, atapata Sh. 100,000. Hili chumo bomba!

Sisiem kimeruhusu wanachama wake watoe rushwa kusaka kura za wanachama wenzao watakaoshiriki kuamua kada gani agombee. Kura hizi zinapigwa Agosti mosi.

Wala nisiambiwe chama hakikuruhusu uchafu huu. Nisiambiwe maana ugawaji unafanywa asubuhi, mchana na jioni, kabla ya kiza kuingia. Hadharani dhahiri shahiri.

Nikamuambia safi jirani. Umezichukua sio? “Ah nisichukue mie masikini ivo unajua. Sikuziomba tumeitwa tukapewa, niziwache?”

Hakuona au aliona ni vibaya kupeana pesa, hakujua kama mtindo ule ni rushwa.

Sawa kama jirani yangu hakujua, je waliotoa pesa zile nao hawakujua? Baadhi yao wana elimu kubwa ya mambo, wanajua wametoa rushwa.

Kwa mfano tuseme mtu kama Shamsi Vuai Nahodha hajui kufanya vile ni kutoa rushwa? Amewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, Waziri Kiongozi Zanzibar kwa miaka kumi. Hajui rushwa huyu?

Wanachama wa kawaida kama jirani yangu wakipewa elfu kumi. Walio viongozi wakiwemo masheha na kamati zao, itakuwa wamepewa malaki kuwakusanya wanachama. Usiulize viongozi wa majimbo, wilaya na mikoa.

Ally Abdalla Saleh, mwandishi mkongwe na mwanasheria aliyejiunga na siasa, amepata sifa kwa kuteuliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kugombea ubunge jimbo la Mji Mkongwe, bila ya kutoa rushwa.

Kikao cha juu cha chama kilipata taarifa alikataa kuhonga wajumbe wa kupiga kura katika jimbo kuamua nani awe mgombea.

Mwenyewe alipata kuniambia hatatoa hata senti kutafuta kuteuliwa. Ametoa msimamo huo kwa timu yake iliyoratibu kampeni, na hata kwa wanajimbo. Kweli hakutoa.

Kura ilipopigwa alikuwa mtu wa tatu. Lakini Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipoketi kufanya maamuzi, liliwatema waliomshinda, akateuliwa yeye.

Kumbe rushwa inaweza kupigwa vita na chama chenyewe hata kama tume za kudhibiti rushwa zimelala. Ipo Takukuru na Zanzibar ipo Tume ya Kudhibiti Rushwa na Kuhujumu Uchumi.

Bali hiyo haiwezekani kwa Sisiem. Ni chama kinachokua kwa rushwa na Edward Lowassa anasema wazi majungu, uongo na fitina ndio mpango mzima. Acha kifilie mbali, chama gani kibaki hai kwa nguvu ya rushwa na uongo?

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s