CCM kitanzini mpangilio wa majimbo

Jecha Salim Jecha, akitangaza Mabadiliko ya Idadi, Mipaka na Majina ya Majimbo ya Uchaguzi kwa mwaka huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015
Jecha Salim Jecha, akitangaza Mabadiliko ya Idadi, Mipaka na Majina ya Majimbo ya Uchaguzi kwa mwaka huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015

BAADA ya kuisoma makala ya wiki iliyopita, msomaji wa mkoani Tanga alinitumia ujumbe mfupi wa simu akisema, “Mwandishi kwa kweli leo umenitia wazimu.”

Sikupata undani wa alichokusudia kunieleza. Nilipompigia simu kwa lengo la kupata ufafanuzi wa kauli yake hii, Hamad Ali Mbae akafunguka.

Akasema sio kwamba amepata ugonjwa wa wazimu, isipokuwa yaliyomo kwenye makala ile, yamemuelimisha kitu muhimu asichowahi kukijua kabla. Amegubuka kutoka usingizini alikokuwa.

Mbae anasema haijapata hata mara moja kumpitikia akilini mwake kuwa mwananchi wa kawaida kama yeye, kumbe anapaswa kufuatilia na kujishirikisha katika hatua zote zinazotangulia ile hatua ya kupiga kura.

Amepata elimu kwamba hatua za uchaguzi zinazoishia na kutangazwa kwa matokeo, zisipotekelezwa kwa mujibu wa sheria na katiba, huweza kuufanya uchaguzi ukose vigezo vya kutangazwa kuwa ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.

Kilichomfurahisha zaidi Mbae, ni kule kuelezwa kwamba hatua mbili zilizokwishapita Zanzibar – mpangilio mpya wa majimbo ya uchaguzi na uandikishaji wa wapigakura – tayari zimeutia dosari uchaguzi unaokuja.

Ndio ukweli uliopo katika suala hili. Tume ya Uchaguzi inapofanya uchambuzi wa majimbo ya uchaguzi na kuyagawa upya – hatua inayotambuliwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 – na ikaonekana imetekeleza kwa utashi wa kisiasa, basi itabakia kuwa ilitekeleza hayo kwa nia ya kukibeba chama kilichopo madarakani.

Ukiyaona majimbo yalivyokatwa yakiwemo manne yaliyoongezwa, utathibitisha kile kilichotarajiwa wakati matokeo ya kazi ya uchambuzi yalipokuwa yakisubiriwa.

Kwanza kazi hiyo ilichelewa sana kutolewa taarifa yake pamoja na wakuu wa ZEC inayoongozwa na mwenyekiti Jecha Salim Jecha kutetea kuwa palikuwa na muda wa kutosha na kwamba walishirikisha wadau wote.

Tena, niseme mapema Jecha ambaye ni mtumishi wa serikali mstaafu aliyefikia ngazi ya katibu mkuu katika wizara, anasaidiwa na Omar Ramadhani Mapuri, kada wa CCM aliyetoka kuwa balozi wa Tanzania nchini China.

Mapuri aliwahi kuwa waziri wa elimu Zanzibar mpaka mwaka 2005 alipoitwa kwenye chama hicho na kupangiwa kazi ofisi ndogo ya Lumumba akipewa dhamana ya kuwa msemaji mkuu wa kampeni ya CCM katika uchaguzi ule wa 2005.

Aliondolewa baada ya waandishi wa habari kumgomea kwa kutoripoti taarifa alizozitoa kichama, kutokana na kauli mbaya aliyoitoa pale wapigapicha walipopigwa na askari magereza kwa kuwa waliwapiga picha wafungwa. Mapuri alisema kipigo hicho walikitafuta.

Taarifa ya uamuzi wa kuyaongeza majimbo ya uchaguzi kufikia 54, badala ya 50 yaliyotumika katika uchaguzi wa 2010, ilitolewa wakati kulishakuwa na habari kuwa majimbo yataongezwa na itakuwa ni kwa maeneo ambayo yatakinufaisha Chama Cha Mapinduzi.

Inawezekana wala CCM isipate manufaa yale iliyoyatarajia au inayoyatarajia. Na hii ni mahsusi kwa sababu uchaguzi safari hii unafanyika wakati umma umehamasika zaidi kwa kiu ya kupatikana mabadiliko ya uongozi Zanzibar na jamhuri kwa jumla, kuliko ilivyokuwa uchaguzi uliopita.

Mpaka sasa, wapo wananchi hawajui hasa watapiga kura kituo gani kwa kuwa vituo walivyozoea, vimo ndani ya majimbo mapya. Mfano ni wakazi wa Kwarara, ambao wamekuwa wakipiga kura skuli ya Kijitoupele, ambako sasa ni sehemu ya jimbo jipya la Pangawe.

Tume imechomeka jimbo katikati ya majimbo ya Fuoni, Mwanakwerekwe na Koani huku ikilivunja jimbo la Magogoni ambalo katika uchaguzi wa 2010, lilitwaliwa na wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kitu cha ajabu, Tume imefuta jimbo la Rahaleo, likitwaliwa siku zote na CCM, na kulazimisha wanasiasa waliokuwa wawakilishi hapo, kuingia katika ushindani katika jimbo la Kikwajuni, ambako kwenyewe kuna msuguano mkali.

Tume ilifanya hivyo kwa sababu tayari serikali ilishapangua shehia mbalimbali na kuzichomeka kwenye majimbo ambako imeamini yatasaidia kuinufaisha CCM. Serikali ilifanya hivi kwa nguvu ya sheria inayompa mamlaka Waziri anayehusika na tawala za mikoa kubadilisha miundo ya wilaya.

Hilo lenyewe halina utetezi kwamba lilifanywa kwa lengo la kutimiza matakwa ya CCM. Tangazo la Waziri wa Tawala za Mikoa, Haji Omar Kheri, ambaye ni kiongozi ndani ya CCM, lilipotoka ikiwa ni wiki kadhaa kabla ya Tume ya Uchaguzi, lilikuwa ni sharti la kuzingatiwa na tume hiyo katika kupanga upya majimbo ya uchaguzi.

Haikushangaza basi kuiona Tume ikiunda majimbo yenye sura ya rasi kwa jimbo kuingia kwenye shehia ambako kiasili zimekuwa katika majimbo mengine.

Mfano ni jimbo la Muyuni ambalo limefumuliwa kwa kunyang’anywa shehia zilizopelekwa jimbo la Makunduchi; Mji Mkongwe lililovunjwa na kuitwa jimbo la Malindi baada ya kuongezwa shehia zilizokuwa katika jimbo la Rahaleo lililofutwa kwa shehia zake kupelekwa jimbo la Kikwajuni.

Jimbo la Kikwajuni lenyewe sasa limejengwa kufurahisha wakubwa wa CCM ambao wamekuwa na shauku ya muda mrefu kutaka Ikulu ya Zanzibar iondolewe ndani ya jimbo la Mji Mkongwe kwa kuwa tu linashikwa na CUF.

Sasa Ikulu hii itakuwa ndani ya jimbo la Kikwajuni ambalo uzoefu unaonesha CCM imekuwa ikitangazwa wagombea wake kushinda uchaguzi chini ya malalamiko kuwa uchaguzi umevurugwa. Kwa mpangilio mpya, wakubwa hao wanaamini Kikwajuni linachukulika kirahisi.

Tume ya Uchaguzi imepangua pia jimbo la Tumbatu, Donge na Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Jimbo la Tumbatu ambalo ushindi wake kwa CCM umekuwa ukilalamikiwa kuwa ni wa kupangwa, sasa limeongezewa maeneo yaliyokuwa ndani ya jimbo la Donge ambalo kwa asili ni ngome ya CCM.

Bali kutokana na muamko mzuri wa wananchi wa Donge, hasa maeneo ya Muwanda, ambako CUF imefanikiwa kupenya kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ulioingiza zaidi ya wanachama wapya 1,000 miaka miwili iliyopita, pamoja na Mbiji na Vijibweni, badala yake, CCM imejiongezea mzigo kulichukua jimbo la Tumbatu, ambako waziri Kheri ndiko amejijenga kisiasa kiasi cha kujitokeza kama mfalme wa jimbo.

Tume imetoa jimbo la Kijini ambalo limeongezewa shehia ya Shangani, inayojulikana kuwa ni ngome ya kihistoria isiyopasuka ya CUF. Tayari kuna malalamiko kuwa CCM imejipunguzia nguvu ya kulitwaa kirahisi jimbo la Mkwajuni lililopewa jina jipya la Kijini.

Mpangilio mpya wa majimbo pia umelikumba jimbo la Kiembesamaki ambalo limemegwa na baadhi ya maeneo yake kuundiwa jimbo jipya la Chukwani. Kiembesamaki linagombewa na Mansour Yussuf Himid, mwanasiasa kijana aliyeihama CCM na kujiunga na CUF ambaye alilitwaa 2010 akiwa CCM.

Jimbo la Kiembesamaki limepewa maeneo yaliyokuwa ndani ya jimbo la Dimani, ngome ya asili ya CCM ambako CUF imempitisha naibu waziri wa zamani katika serikali ya CCM, Mohamed Hashim Ismail, kugombea. Mohamed amekimbia CCM mwaka huu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s