Kwa kukosa kutoa mgombea Urais: Zanzibar yadhihirisha mshindikizaji tu Muungano

Aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Balozi Amina Salum Ali
Aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Balozi Amina Salum Ali

Na Mwadini Ali

USHAHIDI mwengine umejiandika wenyewe kuhusu nafasi ya Zanzibar ndani ya muungano wake na iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika, katika tukio la kihistoria lisiloweza kusahaulika miongoni mwa Wazanzibari halisia, lililoasisiwa tarehe 26 Aprili, 1964.

Kumekuwa na malalamiko upande wa Zanzibar ya namna nchi hii katika ukanda wa Afrika Mashariki, unaoandamana na mwambao wa Bahari ya Hindi, inavyozidi kukandamizwa ili ibakie tu mshindikizaji kuliko kuwa mshiriki wa kwelikweli ndani ya muungano huo.

Ingawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa baada ya yenyewe kuwa sehemu muhimu kati ya zile mbili, Zanzibar inazidi kutumbukizwa shimoni ambako lengo, kwa mujibu wa Civic United Front (CUF) -Chama cha Wananchi- na hasa kiongozi wake mkuu Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, ni kuimeza isisikike kabisa.

Uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mgombea wake wa wadhifa wa urais wa Jamhuri ya Muungano uliofanywa wiki iliyopita katika vikao vya juu mjini Dodoma, umethibitisha kila kinachohofiwa.

Chama hicho kupitia Mkutano Mkuu wake kwenye ukumbi wake mpya na wa kisasa, uliopo njia kuu ya kwenda Chuo Kikuu cha Taifa Dodoma (UDOM), kilimchagua Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais atakayeshindana na mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), muungano wa vyama vinne ulioundwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba, Machi mwaka uliopita.

Muungano wa UKAWA ambao viongozi wake wakuu na kamati za kitaalamu wamekuwa katika vikao vya ngazi ya juu vya majadiliano, jijini Dar es Salaam, unatarajiwa kutangaza mgombea wake siku mbili-tatu hizi.

Dk. Magufuli ni daktari wa kemia aliyesomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na ambaye amekuwa katika Baraza la Mawaziri tangu 1995 alipoteuliwa naibu waziri wa ujenzi akiwa chini ya Anna Abdallah, aliyekuwa waziri.

Mara baada ya kuidhinishwa na CCM, na baada ya kufanya mashauriano na Kamati Kuu ya chama hicho, Dk. Magufuli alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake mwenza katika mbio za kusaka urais kwa uchaguzi wa Oktoba 25.

Samia ni mwanamke wa Kizanzibari, mwenye asili ya kijiji cha Muungoni, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, na elimu ya shahada ya uzamili kuhusu masuala ya utawala na biashara. Aliingia medani ya siasa mwaka 2000 alipoteuliwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuteuliwa waziri.

Kwa kuteuliwa yeye kuwa mgombea mwenza wa Dk. Magufuli, ina maana tayari Zanzibar imenyimwa nafasi ya haki ya kutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania safari hii.

Itakuwa mara ya tatu Zanzibar inaikosa nafasi hiyo muhimu katika kufanya maamuzi ya mwenendo na muelekeo wa jamhuri. Itakumbukwa Muungano ulipoasisiwa Aprili 26, 1964 Mwalimu Julius Nyerere ndiye alishika urais, mzee Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964, akiwa Makamu wa Rais.

Hata mzee Karume alipouawa kwa risasi Februari 7, 1972 kwenye jengo la makao makuu ya Afro-Shirazi Party (ASP) la Kisiwandui, sasa zikiwa ndio Ofisi Kuu za CCM, maalim Aboud Jumbe Mwinyi alirithi nyadhifa zote mbili – Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania – mpaka alipolazimishwa kwa nguvu kujiuzulu mwaka 1984.

Hapo Mwalimu Nyerere, mwanasiasa aliyejitokeza kama mtawala mkuu wa jamhuri badala ya kiongozi, alisukuma uteuzi wa mzee Ali Hassan Mwinyi, mzaliwa wa wilayani Rufiji aliyefika Zanzibar kwa ajili ya kupata elimu ya dini ya Kiislam akikalia kijiji cha Mangapwani, awe rais.

Mzee Mwinyi alishika urais Zanzibar kwa mwaka mmoja tu, kwani mwaka 1985, Mwalimu Nyerere alimtaka kuachia ngazi ili ajipange kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, wakati yeye akiwa ameamua rasmi kung’atuka uongozi wa taifa.

Mzee Mwinyi alikuwa ameipeleka Zanzibar kwenye mwanzo wa mafanikio ya sekta za kiuchumi. Zanzibar ilianza tena kuwa na harakati nyingi za uzalishaji mali ikiwemo kujitokeza kwa viwanda vidogo huku bandari yake ikitumika kupokelea bidhaa mchanganyiko – nguo, vipodozi, viatu na vifaa vya ujenzi, achilia mbali vyakula vya aina kwa aina kutoka nchi za ng’ambo, tena vilivyokuwa na ubora wa kimataifa.

Biashara ilianza kushamiri kwa wageni kutoka nchi za kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini, kufika kwa nia ya kununua bidhaa mbalimbali. Sekta hii ilichochea ukuaji wa pato la taifa kutokana na mapato yatokanayo na ushuru wa forodha.

Ni wakati huu wafanyabiashara wadogo wa Kizanzibari walipoibuka na kusafirisha bidhaa Tanzania Bara na nchi jirani. Vipato vya wananchi vikaongezeka na ajira zikaendelea kuzalishwa kila mwaka.

Baada ya mzee Mwinyi kuchaguliwa rais mwaka 1985, na sasa kukiwa tayari na ukomo wa uongozi wa Jamhuri, hajaingia Mzanzibari mwengine kwenye wadhifa huo.

Alipostaafu urais baada ya miaka kumi, kufikia Oktoba 1995, mzee Mwinyi, ambaye makamu wake alikuwa Jaji Joseph Warioba, akishika pia wadhifa wa uwaziri mkuu (alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais), alirithiwa na Benjamin Mkapa, mwanadiplomasia kutoka Nanyumbu, kulikokuwa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, aliyekuwa Waziri wa Habari na Utangazaji na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje.

Mkapa ambaye pia aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Tanganyika Standard Newspapers Ltd (TSN) miaka ya 1980, na mwanasiasa ambaye alipandishwa hadhi kwenye urais kwa kampeni kabambe iliyosimamiwa na Mwalimu Nyerere alipomuita Mr. Clean, alichaguliwa Dk. Omar Ali Juma, Mzanzibari mzaliwa wa Wawi, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, kuwa makamu wake.

Dk. Omar ambaye alikuwa daktari wa wanyama (vetenari) aliyesomea Urusi, alitoka kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, chini ya Mzee Idris Abdulwakil, mara baada ya kufukuzwa CCM kwa Maalim Seif Shariff Hamad na wenzake kadhaa kutoka Zanzibar, waliokuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Daktari huyo alifariki dunia ghafla mwaka Julai 2002, akiwa nyumbani kwake alikowasili muda mfupi akitokea kufungua Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) viwanja vya Sabasaba, Mtoni, Dar es Salaam.

CCM ilimteua Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa Waziri katika Serikali ya Amani Abeid Karume mwaka 2002, na kuvikwa wadhifa huo wa Makamu wa Rais wa Tanzania, hadi ulipofanyika uchaguzi ambapo Mkapa alistaafu Oktoba 2005.

CCM ikamteua Jakaya Kikwete, mzaliwa wa Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kugombea wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2005. Uteuzi wake ulikuja baada ya mbinu nzito zilizohusisha matumizi makubwa ya fedha, chini ya ufadhili mkuu wa Rostam Aziz, mfanyabiashara bilionea anayemiliki kampuni mbalimbali ikiwemo inayokodisha mitambo mizito ya miradi ya ujenzi kama barabara na migodi.

Kikwete ambaye sasa ni daktari wa falsafa (heshima), alishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kuiongoza jamhuri kwa matatizo makubwa kutokana na kushamiri kwa rushwa na ufisadi miongoni mwa mawaziri wake na rafiki zake wafanyabiashara, anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba utakapofanyika uchaguzi mkuu.

Kwa hali inayojionesha dhahiri sasa, ina maana hatakuwepo kwa miaka mingine mingi Mzanzibari kushika wadhifa huo, labda tu kama kutakuwa na mabadiliko ya uongozi wa jamhuri, au angalau mabadiliko ya uongozi Zanzibar.

“Kama CCM itaendelea kutawala Tanzania, Zanzibar itaendelea kuwa mshindikizaji tu katika wadhifa huu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hakuna huruma wala busara hiyo upande wa viongozi wa Tanganyika kuipisha Zanzibar itoe kiongozi wa taifa,” anasema mchambuzi ambaye pia ni mwanasheria na wakili wa Mahkama Kuu Zanzibar.

Mchambuzi huyo haioni njia karibuni hasa akizingatia ukweli kwamba iwapo CCM itashinda uchaguzi ujao, inatarajia itasimamia kupigiwa kura kwa Katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum ambalo lilikuwa na zaidi ya asilimia 80 ya makada wake pamoja na waliobaki wengi kusimamia matakwa yake.

Katiba mpya iliyopitishwa, imeondoa msingi wote wa mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa utawala wa jamhuri yaliyojumuishwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Miongoni mwa mapendekezo ya msingi ni kuundwa kwa mfumo wa muungano wa serikali tatu badala ya serikali mbili ambao umekuwa uking’ang’anizwa na CCM. Chini ya mapendekezo mapya ya Rasimu, kungekuwa na serikali ya Tanganyika itakayoshughulikia masuala ya Tanganyika tu, Serikali ya Zanzibar itakayosimamia masuala yasiyokuwa ya Muungano yanayoihusu Zanzibar, na Serikali ndogo ya Shirikisho itakayosimamia masuala ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka zaidi ya 30 yaliyopo.

CUF iliungana na vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) kuunda muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupigania katiba mpya itakayotokana na mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya Tume ya Jaji Warioba.

Wajumbe wote wa UKAWA walisusia mjadala wa rasimu kwa kuwa CCM ilifanikiwa kuivuruga msingi wake kwa kutumia faida ya wingi wa kupitiliza wa wajumbe ndani ya Bunge Maalum. Walitoka wakati majadiliano ya Sura ya Kwanza na ya Sita yalipokamilika, lakini kura zikawa hazijapigwa bado kupitisha sura hizo zilizojadiliwa.

Advertisements

2 Replies to “Kwa kukosa kutoa mgombea Urais: Zanzibar yadhihirisha mshindikizaji tu Muungano”

 1. zanzibar siokukostu kutowa nafasi ya raisi wa jamuhuri pia imekosa hata kuchaguwa makamo wa raisi inasikitisha hata makamo wa raisi ccm zanzibar wanachaguliwa na makufuli inatia huruma

 2. Ukweli ni kwamba tarehe 26 aprili ya 1964 “Nchi 2 ,ziliungana kuwa ni Nchi 1,Dola 1,
  Taifa 1,Uraia 1 ,Serikali 2,kwa shabaha ya kuwepo na serikali 1.

  Suala la Zanzizibar kukosa Urais linazukajee ? Muandishi angesema alao “Mzanzibari
  Amina Salim ,mwanachama wa CCM ,amekosa Urais kwa sababu mwenzake Magufuli ,
  ameshinda hapo ingheeleweka .Ikiwa siyo hivyo ,wengine wa Mtwara na Monduli na
  kwengineko huenda wakafanya ubishi kwa Upotoshi wa kuzusha hisiya finyu za Ukanda,
  Ukabila ,Uvisiwa na hata kimajimbo .

  Inajulikana wazi kwamba ,CCM ni chama cha kitaifa Visiwani na Bara .Wagombea Urais
  huwa wanafuata utaratibu wa chama chao na kila mwanachama anayo haki ya kikatiba
  kugombea nafasi zote za ndani ya chama na za kitaifa – Amina na wengine wote 38
  wamefanya hivyo na .hitimaye Dr..Magufuli ,ameshinda na umetangazwa Ushindi kwa
  wote walio shindania ikiwa pamoja na Samia Suluhu ,kuteuliwa ni mgombea mwenza .

  Mzee Ali Hassan Mwinyi ,Mkapa na Kikwete walichaguliwa kwa utaratibu huo huo .
  Hoja ya kulazimisha kinyume na KATIBA kuwepo Urais wa Mpokezano ni utashi wa
  Upinzani ,ambao kimsingi ni siasa ya “kugawa maziwa ya sumu ” ,inayofanywa na
  wapinga Mapinduzi na Muungano.Shabaha yao ni kujadisha hisiya Ujananchi wa
  Uzanzibari Dhidi Ya Utanganyika au Utanganyika dhidi ya Uzanzibari.
  Wanasambaza sumu hiyo badala ya kuujenga undugu wa kijadi na Ujananchi wa Utanzania ,ambao ndio lengo halisi la Waasisi wa Muungano Marehemu Karume na
  Mwalimu Nyerere.

  Muunganisho wa Vyama Vya ASP na TANU 1977 na kuwepo chama cha Mapinduzi
  CCM ilikuwa ni ushahidi thabiti wa lengo la kutoka 2 kuelekea 1 ,huo ndio ukweli wa
  mambo .

  Hata hivyo,bila ya Shaka kuna Wazanzibari CUF-Zanzibar na hata Watanganyika kwa
  mfano CHADEMA ambao pia hawataki Muungano na hawakubaliani na Itikadi hiyo ya
  chama cha CCM,lakini hawawezi kulazimishwa na wao Wapinzani hawawezi kamwe
  kulazimisha CCM Kuzikubali Itikadi za Upinzani.

  Mpangilio wa hoja za muandishi wa makala ya hapo juu ,hajaweka lolote jipya ila tu
  ni marudio ya ushabiki na kupachika-pachika Itikadi za CUF za kuhalalisha yale ya Warioba,ambayo walitaka kuyalazimisha kinyamala kinyume na sheria na utaratibu
  wa kidemokrasia na kanuni za Bunge .Dai lao batilifu na kwamba wingi wa Wabunge
  wa CCM hawajaitendea haki Ushauri wa Tume ya Warioba,ni Sawa na kusema “Rasimu
  ya Warioba ilikuwa ni msahafu au bibliya isiyopaswa kurekibishwa “,kauli kama hilo
  ni la Upotoshi kwa sababu hata Warioba mwenyewe baada ya kuiwakilisha Rasimu
  alisema ” Wabunge wanahaki ya kuiboresha na hata kuikataa ,kwa mujibu wa sheria “.

  Bunge limeamuwa kuirekibisha na ni Wananchi ,ni wananchi wenyewe ndio wenye
  kauli la Uamuzi la kuikubali au kuikataa Katiba Pendekezwa kwa zao za “Ndiyo au
  Hapana na sio Ushabiki na kelele-kelele za Vyama Vya Siasa hasa Za Wapinga
  Mapinduzi Na Muungano. UKAWA walitoroka kazi za Bunge kwa sababu walishindwa
  na waliishiwa na hoja – Wabunge Wengi Waliendlea Na Kazi ,Wamependekeza Na
  Wananchi watatowa Uammuzi .

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s