Taqabbala Allaahu Minnaa Wa Minkum – ‘Iydul-Fitwr Al-Mubaarak

Eid-mubarak-2015Assalaamu ‘Alaykum wa RahmatuLLaah wa Barakaatuh,

Tunapenda kuchukua fursa hii kuwasilisha salaam zetu za siku hii na du’aa njema kwenu wote, tukimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Atutaqabalie ‘amali zetu na zenu ‘TAQABBALA ALLAAHU MINNAA WA MINKUM’ (Hivi ndivyo Maswahaba watukufu walivyokuwa wakiambiana pindi wanapokutana katika siku ya ‘Iyd). Na tunamuomba Yeye Aliyetukuka na Mweza, Awajaalie furaha, amani, mapenzi, siha, iymaan, taqwa, ikhlaasw pamoja na karama na utukufu katika masiku yote ya uhai wetu.

Mwisho, bila kuwasahau kwa du’aa zetu Waislam wote waliopo kwenye dhiki, vita, ukandamizwaji, njaa, maradhi na wanaodhulumiwa pote duniani. Tukimuomba Allaah (Subhaanahu wa ‘Ta’alaa) Awakwamue na kuwapa faraja na nusra. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Atutakabalie du’aa zetu na za Waislam wote duniani, Aamiyn

Zakaatul-Fitwr, ‘Iydul-Fitwr Na Swawm Ya Sittatush Shawwaal

1- ZAKAATUL-FITWR  

Inaitwa Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana na kumalizika Swawm ya Ramadhwaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika mwezi wa Ramadhwaan.

Hikmah Yake

Ni kutwaharisha Swawm ya Muislamu kutokana na maneno machafu, ya upuuzi wakati alipokuwa amefunga kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya ‘Iyd. Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:

عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . ” رواه أبو داود  بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .

Kutoka Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni twahaara ya mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalah basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalah basi hiyo ni miongoni mwa sadaka” [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].

Na ndio kusudio ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)

((قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى))   ((وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّى))

((Hakika amekwishafanikiwa aliyejitakasa)) ((Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akaswali)) [Al-A’laa: 14-15]

‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz alikuwa akiamrisha watu kutoa Zakatul-Fitwr na huku akisoma Aayah hizo tukufu.

Wakati Unaowajibika Kutoa

Kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhwaan hadi asubuhi kabla ya Swalah ya ‘Iydul-Fitwr. Inaweza pia kutolewa siku mbili tatu kabla. Mtoto atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama jua imewajibika kutolewa Zakaatul-Fitwr.

Anayewajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr Na Kitu Gani Cha Kutoa

 عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَال فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأُنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ وَأَمَرَ بِهَا أَنْ تُؤَدَّى قَبْلَ خُرُوجِ النَّاسِ إِلَى الصَّلاةِ . صحيح البخاري   

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa’* moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-‘Iyd)” [Al-Bukhaariy]

  • swaa’ moja = kilo mbili na nusu hadi tatu au (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.

Kinachotolewa Ni Chakula Kinachotumika Na Watu Katika Nchi:

عن  أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ “ُكُنَّا نُعْطِيهَا فِي زَمَانِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ أو صَاعاً من الشعير, أو صاعاً من تَمر, أو صاعاً من زَبيب، أو صاعاً من أقِط    البخاري  

Abu Sa’iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Tulikuwa tukitoa zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) swaa’ moja ya chakula, au swaa’ ya shayiri au swaa’ ya tende au swaa’ ya zabibu au swaa’ ya aqit” (mtindi mkavu) (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama za hizo) [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 2- ‘IYDUL-FITWR  

Inaitwa ‘Iydul-Fitwr (‘Iyd ya kufuturu au kufutari) kutokana na Waislamu kumaliza funga ya Ramadhwaan. Hivyo haifai kufunga Swawm siku ya ‘Iyd, bali ni sikukuu ya Waislamu ya kusherehekea, kufurahi kwa kila njia zilizomo katika mipaka ya Dini.

a)  Apasayo Kufanya Muislamu Yaliyo Sunnah

Kuoga Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali

فقد صح في الموطأ وغيره أَنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ كَانَ يَغْتَسِلُ يَوْمَ الْفِطْرِ قَبْلَ أَنْ يَغْدُوَ إِلَى الْمُصَلَّى

Imethibitika katika Muwattwaa na vitabu vinginevyo kwamba ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akioga siku ya ‘Iydul-Fitwr kabla ya kwenda Muswallaa.

Kujipamba Na Kuvaa Nguo Nzuri

وعن جابر رضي الله عنه قال : كان للنبي صلى الله عليه وسلم جبة يلبسها للعيدين ويوم الجمعة . صحيح ابن خزيمة   

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume alikuwa ana jubbah akilivaa siku za ‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa” [Swahiyh Ibn Khuzaymah]

Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akivaa nguo zake nzuri kabisa siku ya ‘Iyd.

Kwa hiyo inapasa kujipamba kwa nguo nzuri, na manukato mazuri. Ama wanawake hawapasi kujipamba na kudhihirisha mapambo yao ikiwa ni mavazi au kujipaka vipodozi na pia hawapaswi kujitia manukato na kutoka nje. Wanaweza kudhihirisha yote hayo mbele ya Maharimu zao tu.

Kula Tende Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لا يَغْدُو يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ .. وَيَأْكُلُهُنَّ وِتْرًا . البخاري  

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki kwenda kuswali Swalah ya ‘Iyd ila baada ya kula tende… na akila kwa hesabu ya witr. [Al-Bukhaariy]

Hii ni kwa sababu haifai kufunga siku hii ya ‘Iyd. Asiyepata tende anaweza kula kitu chochote.

Ama katika ‘Iydul-Adhwhaa ni Sunnah kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na anaposhuka baada ya Swalah ni bora kitu cha kwanza kula ni ile nyama ya Udhwhiyah (mnyama aliyechinjwa) ikiwa itapatikana.

Kuleta Takbiyrah Kwa Sauti

Sunnah kuu katika ‘Iyd kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ((

((na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 185]

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta Takbirah mpaka anamaliza Swalah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah – Shaykh Al-Albaaniy]

 Matamshi Ya Takbiyrah

الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد

Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah, WAllaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamdu

Wakati wa Takbiyrah

Unaanza usiku wa ‘Iyd mpaka anapoingia Imaam kuswalisha Swalah ya ‘Iyd

Kupongezana

Ni vizuri kupongezana siku ya ‘Iyd baina ya Waislamu, kuzidisha mapenzi baina yao. Na ilivyo Sunnah ni kusema kama walivyokuwa wakiambiana Maswahaba wanapokutana siku ya ‘Iyd ni kusema:

‘Tuqubbila Minna wa Minka’ au ‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’.

 Kuelekea Katika Muswallaa Kwa kutembea Na Kurudi Kwa Njia Nyingine

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا كَانَ يَوْمُ عِيدٍ خَالَفَ الطَّرِيقَ . رواه البخاري   

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia siku ya ‘Iyd” [Al-Bukhaariy]

Hikmah yake ni kwamba njia hiyo itashuhudia siku ya Qiyaamah na ardhi itazungumza yote ya kheri na shari anayotembelea mja juu yake. Pia kudhihirsiha Uislamu katika njia mbili, pia kukutana na watu tofauti na kuwasaidia kwa njia yoyote.

Kuswali Swalah ya ‘Iyd Katika Muswallaa

Ni Sunnah bali, ni waajib kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamrisha watu wote watoke kwenda kuswali:

عَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رضي الله عنها قَالَتْ “أَمَرَنَا تَعْنِي النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نُخْرِجَ فِي الْعِيدَيْنِ الْعَوَاتِقَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ وَأَمَرَ الْحُيَّضَ أَنْ يَعْتَزِلْنَ مُصَلَّى الْمُسْلِمِينَ”  مسلم

Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Ametuamrisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tutoke katika ‘Iyd mbili vijana na vikongwe na kaamrisha wanawake wenye hedhi wajitenge katika Muswallaa” [Muslim]

b)  Yaliyo Bid’ah Katika ‘Iyd

Kuleta Takbiyrah Kwa Pamoja Katika Misikiti Na Muswallaa

Inavyopasa ni kila mtu kuleta Takbiyrah pekee.

Kutembelea Makaburi

Imekuwa ni ada ya baadhi ya watu kutembelea makuburi siku za ‘Iyd. Jambo hili halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala Maswahaba zake. Mtu anaweza uzuru makaburi siku yoyote na si kutenga siku ya ‘Iyd kwa jambo hilo na hadi kugeuka kuwa ni katika Sunnah za ‘Iyd hivi leo.

Maamkizi Ya Kuiga Makafiri

Kupelekeana kadi na zawadi kama wafanyavyo makafiri, haipasi kuwaiga kwani ni jambo tulilokatazwa katika dini na tuwe na fakhari na mila na desturí zetu.

c)  Yaliyo Maasi

Kunyoa Ndevu

Kunyoa ndevu hasa kwa makusudi ya kukusudia ‘Iyd kwa kudhani mtu anapendeza akifanya hivyo ilihali anavunja shari’ah na kupingana na Sunnah za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Wanawake Kutokutimiza Hijaab zao za kishari’ah na kudhihirisha mapambo yao mbele ya wasio Maharimu wao.

Sherehe Za Maasi

Kuchanganyika wanawake na wanaume (party) na kuwekwa muziki, vyakula na vinywaji vya haraam na kupeana mikono wanawake na wanaume.

((لأَنْ يُطْعَنَ فِي رَأْسِ أَحَدِكُمْ بِمِخْيَطٍ مِنْ حَدِيدٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَمَسَّ امْرَأَةً لا تَحِلُّ لَهُ))

Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Ni bora kwa mwanaume kupigwa sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah – Shaykh Al-Albaaniy]

Wanawake wanaruhusiwa kuimba Nashiyd siku za ‘Iyd wakiwa peke yao au mbele za Maharimu wao.

Kufanya Israaf ya chakula na mali badala ya kuwasaidia masikini na mafakiri

3- SWAWM YA SITATUSH SHAWWAAL   

Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhwaan na siku ya ‘Iyd ul Fitr. Ni Sunnah iliyo na fadhila kuu kwani thawabu zake ni sawa na thawabu za mtu kufunga mwake mzima kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه،

((Atakayefunga Ramadhwaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]

Hesabu ya kuwa mwaka mzima ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))

((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An’aam:160]

Na kauli ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((إن الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها الله له عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر حسنات , إلى سبعمائة ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها , كتبها الله عنده حسنة كاملة , فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة واحدة )) متفق عليه ،

 ((Allaah Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia nia kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya  ataandikiwa dhambi moja)) [Al-Bukhaariy ya Muslim]

Maulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhwaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhwaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.

Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu.

Tunawaombea Waislamu wote wajaaliwe kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhwaan kwa kheri na mafanikio, watakabaliwe Swawm zao, na madhambi kughufuriwa, waweze kutoa Zakaatul-Fitwr za kutakasa Swawm, Wawe na ‘Iyd ya furaha na uwezo wa kufunga Sitatush Shawwaal.

Taqabballa Allaahu Minna wa Minkum

Chanzo: Alhidaayah

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s