Maharamia nanyi mtakwenda tu

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein
                                         Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein

VIONGOZI wa CCM Zanzibar wanakosea sana. Huu utamaduni na hulka ya ulaghai, jeuri, chuki na ubinafsi waliouzoea katika kufikia malengo ya kisiasa, si kitu kingine chochote isipokuwa ni ushetani.

Kudhani kwamba Zanzibar haiwezi kuongozwa na mtu mwingine yeyote mbali na wanaoabudu Chama Cha Mapinduzi badala ya Mwenyezi Mungu, hakuna maana zaidi ya kuamini kuwa juu ya ardhi asiyekuwa CCM, basi hafai kuaminiwa kwa lolote.

Mtizamo huo si sahihi hata kidogo. Yote hayo si sahihi chembe. Hakika hayo wanayoyafikiria na kuyaamini, yote ni dalili za ushetani tu.

Kuamini kuwa binaadamu ni wao tu, ni ndoto, na kwa hakika hayo wayaaminio na wayatendayo yanatoa tafsiri moja kubwa: Viongozi hawa wa CCM si wacha Mungu wa kweli.

Hivi wanapojitapa na kushabikia ujinga kuwa “Serikali ya Zanzibar haichukuliwi kwa vikaratasi bali wakitaka nao wapindue” ni nini kama sio kuabudu ushetani, kiburi, ulaghai na utamaduni mbaya na usiofaa kwa watu wenye akili timamu?

Viongozi hawa lazima watambue Zanzibar si nchi ya watu fulani tu, na watu wenyewe wakawa ni wao tu wanaoamini katika mipango ya kuhujumu taratibu za kisheria na kikatiba kwa sababu ya maslahi binafsi.

Kwamba mbele yao ni wao na nyuma yao ni wao. Eti bila ya wao Zanzibar haiwezekani kuishi na kukua, Mapinduzi hayalindiki, na Muungano hauimarishiki.

Si kweli, nao wanajidanganya na kudanganyana.

Zanzibar ingawa ina wenyewe, bali ni nchi ya kila aliyepo juu yake. Wanapojihalalishia kuwa wao ndio wawe waamuzi wa kila jambo, na kwa wakati wautakao wao, wanakosea sana.

Kinachofanywa kupitia mikono yao ni uharamia mtupu. Ni uharamia tu kama uharamia mwingine wowote unaofanywa kwingine kokote juu ya ardhi ya Mwenyezi Mungu. Basi nao ni maharamia.

Ona wanavyofedheheka mchana. Anaitwa waziri serikalini anafadhili genge la askari waliojaa woga na kuwashikisha silaha wakizunguka mitaa na kwenye vituo vya uandikishaji wapigakura.

Ni waoga wakubwa maana wasingefunika nyuso wanapoendesha uharamia kwa wananchi wenzao wa Zanzibar. Wanaume shupavu wajifunike nyuso kuogopa nini? Hakuna anayejiamini akavimba kwa kutenda uharamia akijificha asitambuliwe.

Hakuna waziri anayejiheshimu akamkiuka rais aliyemteua na kuchafua siasa njema akapandikiza ujinga kwa askari wa serikali. Nani?

Askari wa serikali gani wanathubutu kushika bunduki ya Sub Machine Gun (SMG), majambia, marungu, nondo na misumari iliyochomekwa kwenye vipande vya mbao na kuvamia wananchi?

Askari gani anafunika uso wake huku amebeba silaha na kuvuruga vijana waliotulia msikitini wakisubiri saa ya kusali? Kwamba wamejiumba na kujitengeneza wenyewe sio? Haiwezekani.

Mimi nakubali askari hawa ni wahuni tu kama walivyo wale wanaowalisha, kuwapanga na kuwaelekeza waende kuhujumu wananchi majumbani, mitaani kwao na kwenye vituo vya uandikishaji wapigakura.

Askari gani anasukuma mwanamke kama anapambana na jabari? Anamvua nguo na kumbaka uwanjani mchana kweupe ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani?

Wanaume wanne waliotimia – tuseme wa miraba minne – wanatumia misuli yao kumshika mwari wa watu na kumuingilia mchana hadharani. Hawa unawaita nani kama sio maharamia wakuu?

Huwa ninasema usitende uovu, hakuna atakayekugusa. Hata simu hutapigiwa. Hutatumiwa salamu wala nini. Utabaki salama na kimya raha mustarehe. Ila ukiamua kuuvua ubinaadamu na kuuvaa unyama na hisia za kikatili, hutaachwa utulie.

Kwa nguvu zako unazoringia, wenye kazi zao watakushughulikia kwa utaratibu wa kawaida sana wa kushughulikia washenzi kama wewe. Ndio, u mshenzi tu usingeacha utu ukauvaa ujinga.

Waziri mwingine wa zamani eti naye anatamka mipango yao ya kutafuta ushindi wa kulazimisha iwe tu hata ikibidi kwa kuua wananchi. Uharamia mtupu. Una nini wewe kisichoonekana? Roho nyeusi kama ulivyo, huna tofauti na ibilisi aliyefudikizwa na mkubwa kuliko.

Wengine wamejaaliwa weupe, kumbe mtihani mtupu. Hawana wanalo isipokuwa kufikiria uovu tu dhidi ya wananchi. Kwao siasa ndio kila kitu, hata maisha yao wameyasabilia kwa siasa. Basi iwe siasa chafu? Fujo na ghamidha?

Ona wanavyofedheheka – ndani ya walewale wanaowaona ni watu wao, wapo wenye moyo wanakataa na kuamua kufichua siri zao. Siri za maharamia na wazandiki hadharani. Tena kwa kurikodiwa.

Haya leo mnanuka mitaani Zanzibar, katika jamhuri na ughaibuni kote. Mnatajwa kuwa ndio akhasi mmechafuka kuonesha mna nguvu na mnajua kuliko mwenye nguvu na anayejua. Mmepotea poo!

Katika harakati zao wazandiki wamefikia kuvamia kituo cha redio eti wanamtafuta mwandishi muulizaji sababu za uharamia. Kumbe mkidhani mtaachwa mfanye mtakavyo? Hapana.

Kama rais aliyepo anawavumilia hamvumiliki. Mwenyezi Mungu anawapuruzia, mtakula jeuri yenu kwa wakati anaoutaka Subhana.

Hamko peke yenu. Haiwezekani serikalini kote wajifanye hawaoni maovu wanayotendewa wananchi Zanzibar. Haiwezekani Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi hajui hayo.

Hawa walinzi wa amani nao, masikini roho zao. Wanatii maharamia. Ni kutii maharamia ndo maana unawasikia zama hizi wanasema risasi zilipigwa juu kwa bahati mbaya zikamuangukia mwananchi. Aibu.

Rais Dk. Ali Mohamed Shein anayajua yote. Kama hajaelezwa na watu wake, hasomi gazeti? Hasikilizi redio, haangalii televisheni? Basi hayo yote tuache, hakutani na watu? Basi rais rahisi.

Urais ni dhamana. Ni uongozi. Ni uadilifu. Ni upendo. Ni mapenzi kwa unaowaongoza. Urais ni suala la katiba si tambo na vitisho. Uongozi ni jambo la ibada vilevile. Lakini unaongoza vipi? Ni kama alivyoagiza mola muumba au unatuna?

Zanzibar inataka kuongozwa na waadilifu. Kama una uongozi halafu wananchi wanaumizwa ovyo na wahuni na haiwi kitu, hapo pana uongozi upi? Mtihani mtupu.

Uongozi Zanzibar haujatimia. Uongozi utimie viwango na mtu utakiwe sio ujitakishe kwa watu. Viongozi wa CCM wajue mwisho wa ubaya ni ubaya.

Hata mara moja kura hazitafutwi kwa bunduki nchi ikabaki salama. Kura ni hesabu, bali isipotimia, haita kwa kuumiza watu wazima na watoto mitaani.

Hata watendao uharamia hawatabaki salama. Watasokomezwa vilevile kama wenzao waliotangulia. Watakwenda tu.

Chanzo: Mawio

 

5 Replies to “Maharamia nanyi mtakwenda tu”

 1. Hawa ccm walionao niujinga tu usiokua namipaka.Naukichunguza kiundani haswa unakuta nishrik,maana huwezi kusema hakuna kama ccm namengine yenye kufanana na hayo.

 2. “And never think that Allah is unaware of what the wrongdoers do. He only delays them for a Day when eyes will stare [in horror]” 14:42

 3. “And they had planned their plan, but with Allah is [recorded] their plan, even if their plan had been [sufficient] to do away with the mountains.”14:46

 4. [It will be] on the Day the earth will be replaced by another earth, and the heavens [as well], and all creatures will come out before Allah , the One, the Prevailing.”14:49
  “And you will see the criminals that Day bound together in shackles”14:50
  “Their garments of liquid pitch and their faces covered by the Fire.”14:51
  “So that Allah will recompense every soul for what it earned. Indeed, Allah is swift in account.
  14:52

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s