JK amfananisha Magufuli na ‘tingatinga’

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa amewanyanyua mikono mgombea urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma jana.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa amewanyanyua mikono mgombea urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma jana.

Dar/Dodoma. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli ameelezewa na watu mbalimbali kuwa ni mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, lakini Rais Jakaya Kikwete amehitimisha yote kwa kumpachika jina la “tingatinga”.

Rais Kikwete alisema hayo baada ya Magufuli kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliopigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kuzoa kura 2,104, sawa na asilimia 87.08, ushindi ambao alisema unaakisi kumalizika kwa makundi yaliyoibuka kwenye mbio za kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Balozi Amina Salum Ali alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 253 (sawa na asilimia 10.4), wakati Dk Asha Rose Migiro alikuwa wa mwisho kwa kupata kura 59 (asilimia 2.4). Jumla ya kura zilizopigwa kwenye mkutano huo mkuu zilikuwa 2,422 na kura sita tu ndio ziliharibika.

“Kila mtu anaitwa jembe,” alisema Rais Kikwete alipokuwa akianza kutaja sifa za Magufuli ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na pia Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

“Lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumili ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza.”

Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia wakandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano.

“Tunaamini kuwa utawaongoza Watanzania vizuri,” alisema Kikwete akimgeukia mbunge huyo wa Chato.

“Tulikuwa na wagombea 338 lakini sasa tunaye mmoja na tuna kundi moja tu la CCM. Timu Magufuli imeshaondoka. Wengi walidhani CCM itafia hapa, lakini ushindi huu ni ishara kuwa CCM ni moja.

“Tunatakiwa kuacha kuteuwa watu kwa urafiki na kujuana ili tushinde kwa sababu imani huzaa imani. Sina shaka kuwa tutashinda lakini ushindi hauji hivi hivi lazima tuwe na mikakati mizuri, mipango thabiti na utekelezaji makini,” alisema.

Rais Kikwete ni mmoja kati ya watu wengi waliohojiwa na Mwananchi kuhusu mteule huyo wa CCM, ambaye hakuwa akitajwa kama kinara kwenye mbio za urais kabla ya kufikia hatua hiyo ya kujadiliwa na vikao vya juu.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10,  alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.

Iyombe alisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya.

 Chanzo: Mwananchi

 

 

Advertisements

One Reply to “JK amfananisha Magufuli na ‘tingatinga’”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s