Ukawa ngoma nzito, waahirisha kumtaja mgombea urais

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu makubaliano yaliyofikiwa baada ya kikao cha Wenyeviti na Makatibu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliokubaliana kumtangaza mgombea mmoja wa Urais kwa tiketi ya umoja huo Julai Kumi na nne. Picha: Mwananchi
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu makubaliano yaliyofikiwa baada ya kikao cha Wenyeviti na Makatibu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliokubaliana kumtangaza mgombea mmoja wa Urais kwa tiketi ya umoja huo Julai Kumi na nne. Picha: Mwananchi

Dar es Salaam. Mvutano mkali ulioibuka jana katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.

Kutokana na mvutano huo, viongozi wa vyama hivyo waliahirisha kikao hicho na kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa watamtangaza mgombea huyo Jumanne ijayo.

Kikao hicho kilichowahusisha wabunge wote na viongozi wakuu wa vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa, kilifanyika jana katika ukumbi wa Millenium, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alishindwa kuwaeleza wanahabari kilichowakwamisha kumtangaza mgombea, huku akisisitiza kuwa wanataka kuweka mambo sawa.

“Hatuwezi kuwaangusha Watanzania na kipindi hiki ndiyo chetu kwani tunaingia katika uongozi wa Serikali ili kulikomboa taifa,” alisema: “Kuna mambo ya kukubaliana na kuweka sawa, tutamtaja mgombea wetu Julai 14 (keshokutwa). Naomba niwaeleze Watanzania kuwa Ukawa haiwezi kuvunjika tunachokifanya ni kuwa makini katika maamuzi yetu.”

Alisema kikao cha Kamati ya Ukawa kilifikia muafaka na jana kuwasilisha mrejesho kwa wabunge ndipo ulipofikiwa muafaka wa kusubiri hadi keshokutwa, huku akisisitiza kuwa katika kugawana majimbo wamekubaliana kwa asilimia zaidi ya 90.

Alipobanwa aleleze ni mambo gani yaliyokwamisha kufikiwa kwa muafaka alisema: “Kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama vyetu ila hayawezi kuleta matatizo, tupo pamoja na tutatoa jibu la pamoja.”

Alisema Ukawa imetokana na maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, hivyo kiongozi atakayepitishwa na chama hicho lazima awe, mwadilifu, muwazi na mwajibikaji.

“Lazima tuwe na mgombea atakayesimamia mambo ya wananchi waliyotaka yawemo katika Katiba, mambo hayo ni yale yaliyowekwa katika rasimu ya Katiba ya Jaji (Joseph) Warioba,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kama katiba ya nchi ingekuwa na kifungu kinachoruhusu vyama kuungana, vyama vinavyounda Ukawa vingeungana lakini kutokana na sintofahamu hiyo katika Katiba, wanalazimika kutatua changamoto hiyo kwa umakini mkubwa.

Kuhusu majimbo alisema; “ni kama tumeshagawana yote isipokuwa ambayo yana wagombea wawili wawili, yaani kutoka vyama zaidi ya viwili. Tumekubaliana majimbo zaidi ya 170 mpaka sasa.”

Habari za ndani

Imeelezwa kuwa katika kikao hicho kilichoanza saa tisa alasiri mvutano ulikuwa kati ya viongozi wa juu wa CUF dhidi ya wabunge na viongozi wengine wa vyama vyote vinavyounda Ukawa, wakiwamo wa CUF.

Habari hizo zilieleza kuwa viongozi wa CUF wanashinikiza mgombea urais wa Ukawa awe Profesa Lipumba, huku wabunge wa Ukawa wakimtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa maelezo kuwa anakubalika zaidi.

“Unajua Lipumba anataka kugombea urais wakati akitambua wazi kuwa upande wa Zanzibar pia CUF inasimamisha mgombea urais. Wajumbe wa Ukawa wanataka Chadema isimamishe mgombea upande wa Bara na kuiachia CUF Zanzibar,” zilieleza taarifa hizo.

Ilielezwa kwamba viongozi wa juu wa CUF, wakiwamo kutoka Zanzibar wametoa baraka zote kwa Dk Slaa kugombea, lakini kikwazo kimebaki kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.

“Nakwambia wazi muafaka hautapatikana na kikao hiki kitaahirishwa hadi Julai 14 au 15 maana huko ndani hakuna maelewano, kikubwa ni urais tu huko katika majimbo hakuna shida,” zilieleza taarifa hizo.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Dk Slaa, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Profesa Lipumba, Katibu Mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

One Reply to “Ukawa ngoma nzito, waahirisha kumtaja mgombea urais”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s