Dk. Shein arudi nyuma akijiuliza

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein akionesha Fomu yake ya kugombea kwa Wanachama wake katika hafla ya kurejesha
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein akionesha fomu yake ya kugombea Urais wa Zanzibar kwa Wanachama wake, katika hafla ya kurejesha fomu hizo

NAKUWA mgumu kuamini Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, anaweza kuwa kiongozi “mapuuza” au msahaulifu kiasi kinachojitokeza.

Sababu ni mbili – ana kiwango kikubwa cha ufahamu wa mambo ya uongozi. Na anatambua kiapo alichoapa cha kutii katiba na kuongoza kwa usawa na haki pasina kumbagua mtu yeyote na kwa namna yoyote.

Anakumbuka alichoelezwa na Maalim Seif Shariff Hamad mara tu alipotangazwa mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2010. Nikukumbushe uliyesahau.

Akiwa mtulivu na maridhia, na akijitokeza mara ya kwanza hadharani tangu ilipozuka hofu kuu ya wizi wa ushindi wa umma, Maalim Seif alikosoa utendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Alisema hauridhishi – na hasa kwa kuwa tayari wananchi walishazoea kutoiamini Tume – na ambao kwa namna hali ilivyo, si rahisi matokeo yake kuaminika pasina ufafanuzi.

Hivyo basi, Maalim Seif alisema katika namna ya kumtanabahisha Dk. Shein, kwamba aitizame kwa jicho pevu tume kama atakuwa na msimamo wa kuiletea nchi uchaguzi ulio huru, wa haki na unaofanyika kwa uwazi (pasina usiri).

Na alhamdulillah, aliitika ushauri ule kwa tabasamu palepale ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani kilipokuwa kituo cha kupokelea na kutangazia matokeo ya kura ya urais.

Aliuambia umma amesikia kilio kile na urekebishaji wa kasoro za kiutendaji za Tume atachukulia kama moja ya mambo muhimu atakayoyashughulikia mapema akishaunda serikali.

Je, Dk. Shein anaweza kurudi akajiuliza kiungwana kabisa, ametimiza kiasi gani ahadi yake katika eneo hili? Na je, yuko tayari leo akikutana au (ikibidi) aitishe mkutano na waandishi wa habari kueleza anachokijua katika hili?

Wakati anatafakari, anadhani wananchi hawana kipimo cha kujua ukweli wa mambo kwamba hakuna kilichobadilika wanapoangalia mwenendo wa tume na watendaji wake kutokana na yanayoendelea mpaka sasa zikiwa zimebakia chini ya siku 200 kufikia siku ya uchaguzi mwingine?

Ni kweli kumejengwa mazingira wezeshi na rahisi kwa wananchi kupata haki ya kuandikishwa ili waingizwe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar na kuhakikishiwa kuja kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wawatakao?

Tangu Juni mosi ilipoanza uandikishaji wa marekebisho ya daftari la wapigakura, Tume haijasikia malalamiko ya wananchi askari waliobeba silaha za moto huku wakijifunika nyuso zao wamejaa kwenye vituo vya uandikishaji?

Hivi kwani uandikishaji wapigakura ni kazi ya kijeshi? Au ya kiraia – inayochukuliwa kama moja ya vielelezo vya utekelezaji wa utaratibu wa kujenga demokrasia – inayopaswa kuendeshwa na kusimamiwa kwa sheria tu siyo silaha?

Lazima askari wawepo vituoni kulinda amani na haki ya wanaostahili kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Zanzibar ya mwaka 1985, kuandikishwa ili wapate fursa ya kuchagua.

Lakini je, Tume inaporuhusu askari kwa wingi, tena wakiwa wamebeba silaha nje-nje, tena huku wakiwa wameficha nyuso zao, ina maana gani kama siyo kuruhusu viashiria vya kuivuruga kazi ya uandikishaji?

Isitoshe, Tume haioni mtindo wa watu kufikishwa vituoni kwa gari kubwa (malori) zilizodhibitiwa kwa utaratibu mahsusi, na watu kulalamika kuwa hao wanaofikishwa kwa staili hiyo ni wageni wasiostahili kuandikishwa vituo walipopelekwa?

Upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanasikika wakisema kila mtu ana haki ya kuandikishwa, na kwamba hakuna haki ya mtu au kundi la watu kuzuia haki ya watu wengine ya kuandikishwa.

Sawa kama utaratibu unafuatwa. Lakini ni kweli kuwapeleka watu kwa mzo namna inavyofanywa na wakionekana kabisa watu hao kuwa si wenyeji wa mitaa ya jimbo husika, si uvunjaji wa sheria?

Hivi ni sahihi kweli kauli kuwa watu hao waachiwe waandikishwe na kama mtu anadhani hawana haki kwa kuwa ni wageni, asubiri kuja kuwawekea pingamizi wakati utakapofika?

Kweli hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa hata kwa watu walioandaliwa makusudi kuandikishwa kwa mpango wa hila?

Na kwamba hayo yavumiliwe kwa kuwa utafika muda wa kuyapinga, na upingaji wenyewe ukawa wa kuwawekea pingamizi? Jamani, inaingia akilini watu wengi hivyo kuwawekea pingamizi? Imewahi kutokea lini na wapi?

Kama hivyo ndivyo inavyopasa kuwa, tuseme ni sahihi mtu anayemuona mwizi – kwa kumjua fulani yule ni mwizi – avunje nyumba na kutoka na vitu ndipo yule mtu amkamate na kumpeleka kituo cha polisi? Ndivyo inavyopasa kuwa?

Sasa kama hivyo ndivyo, tuseme na Polisi yetu inafanya kazi namna hiyo – kusubiri mtu avunje na kuiba ndipo wakamatwe? Na pale inapotangaza kuwa imepangua njama za majambazi kuiba au “magaidi waliotaka kushambulia kwa mabomu kanisa wamekufa katika majibizano ya risasi na askari wetu” ina maana Polisi imekosea?

Si nao wangesubiri mpaka jambazi avunje, na magaidi watekeleze mashambulizi kwa kulipua mabomu kanisa ndipo wawakamate? Mbona haifanywi hivi, isipokuwa raia wao wakiona tukio linataka kufanywa wajifiche ndani mpaka wabaini wizi au shambulio limefanywa?

Ujinga wa mwaka. Na hapa huipati tofauti ya chizi aliyenyakua taulo ya muogaji na kukimbia nayo; na muogaji naye kuamua kutimka kutoka bafuni akimkimbiza chizi ili arudishe taulo yake.

Ni nani chizi zaidi kati yao? Bila ya shaka ni muogaji. Si angebaki bafuni akaagiza taulo mpya au kanga ya kujisitiri.

Matukio ya kutisha yanatokea vituoni lakini wanaoyasimamia yatekelezeke wanachukuliwa ndio walinzi wa sheria na wale wanaojipanga kuyazuia – kuzuia uhalifu – waonekane ndio wahalifu?

Askari wa vikosi vya serikali, walewale wanaovalia soksi kuficha nyuso zao wanazunguka mitaa na silaha nzito mikononi huku wakipiga na kudhalilisha wananchi wakati huu wananchi wanapotakiwa kufukuzia vituoni ili waandikishwe kama wapigakura.

Hawa askari wahuni – hakuna namna nyingine ya kuwaita maana kama ni wa serikali wasingejivika vitambaa usoni kujificha – wametumwa na nani kupiga raia?

Je, mazingira haya ndiyo Dk. Shein anaweza kusimama kiririni – ikiwemo pale Baraza la Wawakilishi – akayatetea ni halali?

Kwamba rais yuko sahihi hasa kuwa haya yote ni sahihi na halali? Halafu kutokana na hayo yanayolindwa na serikali anayoiongoza, tuseme ndiyo sisi waandishi tuandike kwamba anaongoza kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar aliyoapa kuitii?

Hapana. Binafsi sipo tayari kuwa mkosefu wa maarifa kiasi cha kuyapamba maovu kwa kuyapa jina zuri kama wanavyofanya wengine. Kwa hilo, nisamehewe bure. Sikufundishwa hivyo na wala sijakulia kuona matukio ya kishetani halafu nikayapalilia kuwa “ndio utaratibu wa kisheria tuliojiwekea.”

Sasa hali ya mambo ndivyo ilivyo Zanzibar kwa miezi kadhaa. Hata kabla ya Juni mosi, wananchi wanashuhudia watu waliobebwa kwenye malori na mabasi wakipelekwa kambi za vikosi vya ulinzi vya serikali.

Tuseme hawaendi kusajiliwa ili wapate kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, umma uelezwe basi wanakokwenda. Na kufanya nini?

Maswali haya ni muhimu kwa sababu kama ni kusailiwa kwa ajili ya kuajiriwa shughuli za ulinzi si kungekuwa na tangazo la kuita vijana wanaotaka kazi hiyo?

Kwa kuwa hakuna tangazo kama hilo, na haiingii akilini kuwa Dk. Shein ameruhusu ajira za kibaguzi, maana aliapa kuongoza kwa kutii katiba na bila ya kubagua mtu kwa namna yoyote ile. Hakuna ajira mpya iliyotangazwa vikosini.

Dk. Shein arudi nyuma. Safari aliyoianza haifai kwa faida ya amani, umoja na maendeleo. Aone jukumu na dhamana alonayo kwa nchi. Afikirie ahadi ya kulinda serikali ya umoja wa kitaifa na ajizuie kushabikia ujinga na uhalifu.

Chanzo: Mawio

Advertisements

One Reply to “Dk. Shein arudi nyuma akijiuliza”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s