Risasi zarindima BVR, mkutano ZEC wavunjika

Mmoja wa majeruhi waliyopigwa risasi ,Ramadhani Hija Hassan akiwa katika kituo cha afya cha AL-Rahma kwa ajili ya kupatiwa matibabu .Alipigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Shehia ya Nganani Mjini Magharibi, Unguja jana
Mmoja wa majeruhi waliyopigwa risasi ,Ramadhani Hija Hassan akiwa katika kituo cha afya cha AL-Rahma kwa ajili ya kupatiwa matibabu .Alipigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Shehia ya Nganani Mjini Magharibi, Unguja jana

Zanzibar. Wakati watu watano wakijeruhiwa, wawili kwa kupigwa risasi, kwenye uandikishaji wa wapigakura eneo la Makunduchi, mkutano baina ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau umevunjika kutokana na mzozo wa mgwanyo wa majimbo.

Vurugu hizo zimetokea baada ya watu waliokuwa wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya kupinga kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu kuwapo kwa mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta wakivamiwa na kundi la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha za moto.

Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan (42) na Ramadhani Hija Hassan (29) wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali Seif Issa (38), Ali Hassa Hassan (70) kutoka Paje akiwa amepigwa kwa magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir (43).

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji ukiendelea.

“Ilikuja gari na watu waliojifunika nyuso zao wakatuambia tuondoke na sisi tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia kuandikishwa mamluki katika eneo letu. Baada ya kubishana pale wakaenda kuchukua gari nyingine wakaanza kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa risasi ya pajani.

“Watu waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na kuondoka kabla ya kufanya shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo la tukio la Nganani kwa kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku akilalamika kusikia maumivu.

Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa, mkazi wa Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao ni pamoja na walio na umri mdogo.

“Lilikuja kundi la watu mara mbili na kuondoka. Walikiwa wamefunika nyuso zao na waliporudi kwa mara ya mwisho walitushambulia kwa kutumia silaha za kienyeji na baadaye kufyatua risasi za moto na kujeruhi watu wawili,” alisema Mzee Ameir.

Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.

Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha hayo yamesababishwa na nini. “Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao yanatokana na nini lakini yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya risasi kwa kuwa risasi jeraha lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia lakini kitobo kikubwa inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa watakapopata nafuu.

“Wapo walioumia sana hao wataendelea kuwepo hospitali kwa sababu wametokwa damu nyingi sana na kutoka Makunduchi hadi Mjini ni mbali kwa hivyo wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo watakapopata nafuu,” aliongeza Dk Suleiman.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi alisema kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi kuwaingiza kwenye Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu kupigwa risasi na kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na hivyo hazijajeruhi mtu.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s