‘Bao la mkono’ la Nape latua Tume ya Uchaguzi

Wakizungumza kwenye mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili ya Uchaguzi jana, baadhi ya viongozi hao walitaka mkutano huo usitishwe hadi pale CCM itakapomuonya Nape
Wakizungumza kwenye mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili ya Uchaguzi jana, baadhi ya viongozi hao walitaka mkutano huo usitishwe hadi pale CCM itakapomuonya Nape

Dar es Salaam. Kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye bado inawaumiza vichwa wapinzani nchini baada ya viongozi hao jana kuitamkia wazi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuwa hakuna haja ya kujadili maadili wakati CCM tayari kimesema ‘kitafunga bao la mkono.’

Wakizungumza kwenye mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili ya Uchaguzi jana, baadhi ya viongozi hao walitaka mkutano huo usitishwe hadi pale CCM itakapomuonya Nape.

Wa kwanza kuibua mada kuhusu Nape, ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi ambaye alisema hakuna haja ya kuendelea na mkutano huo hadi NEC, Msajili wa Vyama vya Siasa na IGP wakemee kauli hiyo.

“Hivi tutayazungumziaje maadili, mbona CCM kimeshaonyesha kuwa hakitafuata maadili, kuna haja gani ya kuzungumzia wakati wameshasema watafunga hata kwa goli la mkono?” alisema Dk Makaidi.

Awali akiwa katika ziara ya Kinana wilayani ya Sengerema, Nape alikaririwa akisema kuwa ana uhakika CCM itashinda baada ya kuona mwitikio mkubwa wa Watanzania katika ziara hizo.

“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono… bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva aliwatoa wasiwasi wanasiasa hao akiwaambia kuwa Nec itafanya uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na hivyo kauli ya Nape haiwahusu.

“Maadili tunayoyatengeneza yataanza kutumika kuanzia Agosti 22, wakati wa kampeni, lakini iwapo kuna vurugu zinatokea baina ya vyama sisi wala Nec hatuhusiki,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa akichangia kipengele cha wahusika wa maadili aliitaka Nec kuliweka Jeshi la Polisi kupitia IGP kusaini na kuwa mhusika katika masuala ya maadili ya uchaguzi.

Hiki kipengele cha 1.3 kinawataja wahusika wa maadili kuwa ni vyama vya siasa, wagombea, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Nec pekee.

“Kutokana na uzoefu tulionao katka chaguzi zilizopita, Jeshi la polisi ni washiriki wakubwa katika masuala ya uchaguzi, kama jeshi hilo halitasaini maadili hayo basi kutakuwa na matatizo makubwa katika uchaguzi huo,” alisema.

Awali akifungua mkutano huo Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa kufuata maadili, sheria na kanuni za uchaguzi, na katika kipindi chote cha kuanza kwa kampeni hadi siku ya uchaguzi.

Chanzo: Mwananchi

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s