Upinzani ‘walianzisha’ tena bungeni

Mbunge wa  Ubungo (Chadema),John Mnyika
                                  Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika

Dodoma. Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika jana ulizua kizaazaa na kumlazimisha Spika Anne Makinda kuahirisha kikao baada ya kukosekana utulivu ndani ya Ukumbi wa Bunge.

Kikao hicho kiliahirishwa muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu wakati Bunge lilipotakiwa kukaa kama kamati kumalizia kiporo cha Muswada wa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 ambao mchakato wa kuupitisha haukukamilika juzi kutokana na muda kuisha.

Ilikuwa ni kama marudio ya hali ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati wabunge wa upinzani waliposimama na kuweka mazingira ambayo yalizuia shughuli za chombo hicho kuendelea wakati wa kujadili sakata la escrow.

Jana, sakata hilo lilitokea baada ya Spika Makinda kuweka sharti la kutoa mwongozo ulioombwa na Mnyika aliyetaka kujua sababu za uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwenye shughuli za jana licha ya wabunge wa pande zote mbili kuipinga kwa kuwa haina haraka.

Kutokana na majibu hayo, wabunge wa upinzani walisimama na kuanza kupiga kelele wakipinga kitendo hicho cha uongozi wa Bunge huku wakisema; “muda wa kuburuzana umekwisha.”

Hata Spika Makinda alipojaribu kuwatuliza walipiga kelele na kumfanya kiongozi huyo wa chombo cha kutunga sheria kutangaza kuahirisha shughuli za Bunge.

 Hali ilivyokuwa

Mwongozo wa Mnyika ulitokana na ratiba ya shughuli Bunge kuonyesha kuwa kulikuwa na miswada minne iliyotakiwa kujadiliwa.

Hiyo ilikuwa ni Muswada wa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 ambao ulifikia ngazi ya Bunge kukaa kama kamati kuupitisha, Muswada wa Sheria ya Petroli wa mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Uchimbaji.

“Mheshimiwa Spika, naomba mwongozo wako kwa kutumia kanuni ya 53 (1) na (6) ambazo zinasomwa pamoja na kanuni ya 86 katika vifungu vya 1,5,6, kwamba Bunge lako limekiuka kanuni kwa kuleta hoja juu ya hoja,” alisema Mnyika.

Alipopewa nafasi ya kufafanua hoja yake, Mnyika alisema: “Tarehe 29 Bunge lako lilipokea semina juu ya miswada hii mitatu ambayo leo imeingizwa tena bungeni na wabunge kwa kauli moja, bila ya kujali itikadi za vyama, tulipinga jambo hili lakini leo tunaona mmeleta tunaomba ufafanuzi,”

Alisema na kumtaka Spika atoe ufafanuzi hapohapo kwa kuwa jambo hilo lilikuwa ni muhimu.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s