Dk Shein anajijengea historia yake mwenyewe

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akikagua gwaride maalum la Kikosi cha Polisi akiongozwa na SP Ali Abdalla Kitole wakati wa Ufungaji wa Baraza la Wawakilishi la nane huko Chukwani jana Nje ya Mji wa Unguja
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akikagua gwaride maalum la Kikosi cha Polisi akiongozwa na SP Ali Abdalla Kitole wakati wa Ufungaji wa Baraza la Wawakilishi la nane huko Chukwani jana Nje ya Mji wa Unguja

Na Mwadini Ali

INAONEKANA viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamtii sana kiongozi wao mkuu upande wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Na matokeo yake, naye Dk. Shein, daktari bingwa wa tiba ya magonjwa makubwa ya mwanadamu, anawatii sana wasaidizi wake hao wa chama.

Nazungumzia utiifu unaowahusu tu wanachama wa CCM, chama kilekile ambacho ndicho kimempandisha chati ya kisiasa daktari huyu, hadi kufika kuwa mpangaji mkuu wa makao makuu ya mamlaka ya Zanzibar, Ikulu yaliyopo Mnazimmoja.

Utiifu uliopo kati ya wanachama hao wa CCM na Dk. Shein kumbe hauna maana yoyote kwa mustakbali wa Zanzibar, na wala kwa watu wake – Wazanzibari, kutoka Unguja na Pemba.

Sasa hii ni bahati mbaya aliyoipata Dk. Shein katika miaka yake mitano ya uongozi inayomalizika ndani ya siku 120 zijazo. Bahati hii mbaya imetokea kwa sababu huyu Dk. Shein ndiye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM).

Kama si kutimiza tu matakwa ya kikatiba, urais anaoushikilia Dk. Shein usingekuwa na mahusiano yoyote na chama alichopitia kuongoza Zanzibar. Labda hapo ndo angeutumia vizuri wadhifa huu akawa mtiifu zaidi kwa wananchi badala ya kujiweka mtiifu zaidi kwa chama chake na kusahau kabisa maslahi ya wananchi.

Ndo ninaposema kumbe uliopo ni utiifu uliokuja vibaya kwa sababu kadiri ninavopima na kutathmini yanayotokea ndani ya Zanzibar, nchi ndogo kieneo iliyo sehemu ya jamhuri kubwa la Muungano, nazidi kuthibitisha kuwa hauzingatii chembe ya mahitaji halisi ya wananchi wa Zanzibar.

Chukulia suala moja muhimu ambalo alilitolea ahadi mara baada ya kushikana mikono, katika ishara ya kuridhiana, na Maalim Seif Shariff Hamad, ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani.

Ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwezi Novemba mwaka 2010, Dk. Shein baada ya kutangazwa mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanywa Oktoba 31, alitoa ahadi mbele ya ulimwengu kuwa atayashughulikia matatizo yaliyobainishwa kuihusu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar – Zanzibar Electoral Commission (ZEC).

Malalamiko yanayohusu utendaji wa Tume ya Uchaguzi yalitolewa kwake na Maalim Seif, mshindani wake katika kuwania urais, akiwakilisha Chama cha Wananchi (CUF). Maalim Seif ambaye tangu pale alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, aliyajua khasa matatizo ya tume kwa kuwa alikuwa akishughulikia mwenendo mzima wa ratiba ya uchaguzi mpaka matokeo ya mwisho yalipokuwa yakitangazwa.

Malalamiko yote yaliyokuwa yakitolewa na viongozi na wanachama wa chama hicho, na khasa yale yaliyohitaji hatua kubwa zaidi katika kuyashughulikia, yalimfikia yeye; ndipo basi alipolazimika kuyafikisha kwa Tume. Lakini pia yalimfika malalamiko kwa sababu mwenyewe alikuwa ndiye mgombea wa urais, alikuwa analazimika kufuatilia yanayokutwa na wasaidizi wake kama shida zinazotokana na utendaji wa Tume.

Basi Maalim Seif, mara tu lilipotoka tangazo la Mwenyekiti wa Tume wakati ule, Khatibu Mwinchande, la kumpa ushindi Dk. Shein, aliridhia na akaamua matatizo aliyoyabaini kutokea wakati wa uchaguzi, ayafikishe kwa kiongozi mpya kwa ajili ya kuyafanyia kazi.

Akamwambia “Dk. Shein nakuomba sana uyashughulikie matatizo makubwa yanayoikabili tume yetu ya uchaguzi. Yanasababisha manung’uniko mengi na ni lazima yaondolewe ili tufike wakati nchi yetu iendeshe uchaguzi ulio huru, wa haki na kwa njia za uwazi, ndipo matokeo yake yatakapokuwa yanaaminika.”

Dk. Shein aliposhika nafasi ya kuzungumza, akiwa ameshasikia kilio cha matatizo ya kiutendaji ya Tume ya Uchaguzi, alitoa ahadi palepale ya kuwa atayafanyia kazi ipasavyo na kwamba hiyo itakuwa moja ya kazi zake za kwanza akishateua serikali.”

Matatizo ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar si mapya. Yamekuwa yakijirudia kila wakati wa uchaguzi. Kwa kuangalia mjumuiko wa matatizo yanayokabili asasi hii ya kiserikali, ni rahisi kusema yamekuwa yakidhoofisha kuaminika kwa matokeo yenyewe ya uchaguzi yakiwemo yale ya urais. Na ni kwa bahati mbaya sana, katiba imefunga fursa ya kuyahoji matokeo kwenye chombo chochote, mara yakishatangazwa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ina makamishna saba, ikiongozwa na mwenyekiti ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, 1984, huteuliwa na Rais. Sifa ya mteuliwa ni kuwa mtu aliyekuwa au mwenye sifa za kuwa jaji katika Mahkama Kuu au Mahkama ya Rufaa katika nchi yoyote iliyo mwanachama wa Jumuiya ya Madola, au mtu anayeheshimika katika jamii.

Ibara ya 119 ya Katiba ya Zanzibar ndiyo inayotoa mamlaka ya kutambuliwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Uteuzi wa mwenyekiti unatajwa kifungu cha pili. Sasa Dk. Shein alimteua Jecha Salim Jecha, akijua hana sifa ya kuwa jaji. Yeye si mwanasheria kitaaluma.

Kwa hivyo, inachukuliwa kuwa alimteua Jecha, katibu mkuu wa zamani serikalini, kwa sifa ya kuwa “mtu anayeheshimika katika jamii.”

Alichokifanya Dk. Shein katika kumteua Jecha kuongoza Tume, ni kutii zaidi wasaidizi wake katika CCM. Jecha anajulikana alivyo mwanachama wa CCM. Bila ya shaka yoyote, hakustahili kuteuliwa kushika nafasi hiyo. Na msimamo huu unazingatia khasa umuhimu wa nafasi yenyewe kushikwa na mtu mwenye uwezo, uzoefu na ujasiri wa kutenda kwa kutegemea misingi ya Katiba na siyo ushabiki wa chama kama inavyoonekana kutokea chini ya Jecha.

Aliahidi kutenda kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria. Ona anavyoshindwa kuiongoza Tume katika kurahisisha upatikanaji wa haki za wananchi wakati huu tume ikiwa inaandikisha wapigakura vituoni. Lakini, vituo vinavamiwa na watu waliobeba silaha za moto huku wamejivika vitambaa usoni kuficha kutambuliwa.

Hivi kama uandikishaji wapigakura unahusisha watu waliobeba bunduki huku wakijificha wasitambuliwe kwa sura au kwa majina yao, tena wakipiga na kunyanyasa watu waliofika vituoni kujiandikisha, kusudi tu kubeba wengine wasiokuwa wenyeji wa maeneo husika, tuseme masuala ya uchaguzi yachukuliwe kuwa ni jambo la kijeshi?

Wala Jecha hajasikika akilalamika. Amebakia kimya mambo yakiharibika. Anayawachia kwa sababu moja tu kubwa – hayamshughulishi maana hayadhuru utashi wake wa kusimamia uongozi kwa misingi ya Katiba. Kwa kweli Jecha anakosa ujasiri wa kukemea kwa kuwa anamtii zaidi Rais aliyemteua, rais ambaye na mwenyewe anatii zaidi chama alichopitia kuwa rais.

Jecha amelemaa dhamira na akili kama anavyoonekana aliyemteua. Kwao la muhimu ni maslahi ya CCM wala si maslahi ya Wazanzibari. Kwa hivyo basi, kwa yanayoendelea vituoni, tayari wananchi wanaambiwa mapema kuwa wasije kutarajia Jecha kusimamia Tume kutangaza matokeo yatakayowaudhi viongozi wa CCM.

Hivi Jecha akiulizwa ni kwanini khasa Tume haijatangaza mpaka leo hii, miezi mitatu tu kabla ya siku ya uchaguzi, Oktoba 25, na miezi miwili tu kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea, majimbo yatakayoshindaniwa katika uchaguzi huo, atakuwa na jibu gani?

Tume tangu Juni mosi ilipoingia imetuma waandikishaji kuandikisha wapigakura majimboni, lakini haijaeleza kwa umma huyo mtu anayeandikishwa atakuwa mpigakura wa jimbo gani. Haoni anaiongoza tume kibubusabubusa, kama vile yeye na wenzake si watu wenye akili timamu?

Au kwamba yeye na wenzake wanazo akili timamu lakini wanachokikosa ni dhamira njema ya kutumia dhamana waliyopewa kujenga historia ya utendaji uliotukuka? Mkosefu wa dhamira, haipati nia njema kwenye hilo atendalo.

Dk. Shein alijua kwamba kwa kumteua Jecha kuongoza Tume ya Uchaguzi hakutabadilika chochote kutoka yale malalamiko aliyokabidhiwa na Maalim Seif, mwanasiasa aliyemridhia awe mmoja wa wasaidizi wake wakuu serikalini – Makamu wa Kwanza wa Rais.

Rais huyu alijua watendaji wa Tume, kwa kuwa wanaongozwa na mteule wake Jecha Salim Jecha, asiyekuwa na dhamira ya utendaji adilifu, isipokuwa kumpembejea yeye na kukibeba chama chao, wataendesha mambo kwa utaratibu uleule waliouzoea miaka yote – utaratibu wa kutenda huku wakihakikisha ni CCM tu kushinda si zaidi ya hapo.

Halafu hapo bado Wazanzibari na walimwengu wadanganywe kuwa Zanzibar itakuwa na uchaguzi ulio huru, wa haki na uliofanywa kwa njia za uwazi? Jaguju. Kama ndo hivyo, nini kimebakia? Kwanza Dk. Shein hakubadilisha chochote, lakini kubwa ameigandisha nchi isitoke tanurini kwa moto ilipo. Alhamdulillah ameijenga historia yake yeye mwenyewe.

Chanzo: An nuur

 

Advertisements

One Reply to “Dk Shein anajijengea historia yake mwenyewe”

  1. Hotuba ya Dr. Shein ya January 2011 ilitosha kufahamisha Watu yeye angefanya nini Usoni. Waliotarajia yeye angefanya vyenginevyo walikuwa na upeo mdogo wa kuona mambo

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s