Chadema ni ‘amsha amsha’

Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Chadema, Mabere Marando akikata utepe kuzindua Bendi ya Wanawake na Operesheni Amsha Wanawake Tanzania katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Dar es Salaam jana. Bendi hiyo itatumika kuhamasisha katika mikutano ya Ukawa.
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Chadema, Mabere Marando akikata utepe kuzindua Bendi ya Wanawake na Operesheni Amsha Wanawake Tanzania katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Dar es Salaam jana. Bendi hiyo itatumika kuhamasisha katika mikutano ya Ukawa.

Dar/Hai/Hanang’. Chadema imefanya mikutano mikubwa ya kuamsha wapigakura katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Dar es Salaam na Tanga huku mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akisema mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete waliotangaza nia ya kugombea urais ‘wanaivua nguo’ Serikali waliyomo kwa kueleza maovu ya ndani.

Alisema mawaziri hao hawana sauti moja, kila mmoja anazungumza lake kuikosoa Serikali kwa kuahidi kufanya mambo mazuri tofauti na yale yanayofanywa na Serikali ya sasa ya Kikwete.

Hadi sasa makada 38 wa CCM wamechukua fomu za kuomba kuwania urais, miongoni mwao wakiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri 10 na naibu mawaziri wawili.

Katika kutangaza sifa zao baadhi yao wamekuwa wakijigamba watatatua kero za ufisadi, migogoro ya ardhi, kudorora kwa uchumi na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mbowe alisema Chadema haiwezi kuiga mfumo huo kwa sababu wana utaratibu wao wa kutangaza nia na kuchukua fomu.

Alisema ratiba yao ya kuchukua fomu za urais ilishatolewa na itaanzia Julai 20 hadi Julai 25, mwaka huu.

“Mawaziri wa Kikwete hawana sera, wamesahau kuwa nao ni sehemu ya serikali hiyo iyo wanayoikosoa. Chadema tuna utaratibu wetu wa kutangaza nia na kuchukua fomu, nafasi ziko wazi,” alisema Mbowe.

Alipoulizwa wamefikia wapi kuhusu mgombea atakayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Mbowe alisema bado wanafanya mashauriano, muda wowote wakimaliza mgombea wa Ukawa atatangazwa.

“Hii ni vita, hatuwezi kumweka wazi mgombea wetu kwa sababu bado ni mapema. Ukawa bado tunafanya consultations (mashauriano), tukimaliza Watanzania watamjua mgombea wa Ukawa,” alifafanua kiongozi huyo.

Mbowe alipuuza madai kuwa Ukawa inavunjika, akisema haiwezi kuvunjika kama watu wanavyodhani hasa baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua fomu ya kuwania urais ndani ya chama chake.

Alisisitiza kuwa Ukawa haijazuia chama chochote kuchagua mgombea urais kama walivyofanya CUF bali chama chochote kitasimamisha mgombea wake kisha wagombea wote kushindanishwa na kumpata mmoja wa Ukawa.

“Jambo hili tuliliweka wazi tangu awali, kusimamisha mgombea wa chama siyo hatua ya mwisho, ni sehemu ya mchakato wa kumpata mgombea wa Ukawa,” alisema Mbowe.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s