Ikiwa Muungano unavunjika, tutaingia vitani?

KWA UFUPI Nataka ifahamike kwamba, muungano wowote ule ni jambo la hiyari na muhimu, lakini miungano mingi sana duniani imelindwa kwa mitutu ya bunduki, mara tu baada ya kuunganishwa kwa hiyari, hiyari hufuatiwa na “ulinzi wa mtutu”.
KWA UFUPI
Nataka ifahamike kwamba, muungano wowote ule ni jambo la hiyari na muhimu, lakini miungano mingi sana duniani imelindwa kwa mitutu ya bunduki, mara tu baada ya kuunganishwa kwa hiyari, hiyari hufuatiwa na “ulinzi wa mtutu”.

Na Julius Mtatiro

Leo tunamalizia sehemu ya tatu na ya mwisho ya mada hii fupi kwa kuangalia namna bora ya kuulinda Muungano ili usivunjike, na athari zake ikitokea utavunjika ghafla.

Nataka ifahamike kwamba, muungano wowote ule ni jambo la hiyari na muhimu, lakini miungano mingi sana duniani imelindwa kwa mitutu ya bunduki, mara tu baada ya kuunganishwa kwa hiyari, hiyari hufuatiwa na “ulinzi wa mtutu”.

Siku Nyerere na Karume walipochanganya mchanga tuliambiwa ni tendo muhimu la kihistoria, lakini baadaye kila aliyejaribu kuhoji muundo wa muungano, aidha aliishia jela, alifukuzwa CCM au yalimkuta makubwa, nashukuru kuwa leo hii watu tuna uhuru wa kuujadili muungano wetu bila kuingiliwa.

Ikiwa muungano wetu utavunjika kwa hiyari ya pande zote mbili hakutakuwa na hatari zozote zile zitakazotukabili, lakini ukivunjika bila upande mmoja wenye nguvu ya majeshi na uchumi mkubwa kuridhia tutakuwa matatizoni.

Haya nayasema hapa kwa sababu yalitokea hata wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika na katika Darubini ya Jumapili iliyopita nilisimulia kwa kifupi jambo alilonieleza Profesa Lipumba katika simulizi za kumbukumbu zake juu ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Mfano mwingine ni ule uliowahi kutolewa na rubani mmoja ambaye alileta ndege ya Kenya au ya Uganda na ikabaki mikononi mwa Tanzania. “Vunjiko” baya huhamasisha uhasama na matatizo lakini “vunjiko” la busara huleta neema, makubaliano na utulivu maalumu.

Kwa sababu natambua kuwa hatujiandai kufanya “vunjiko” la muungano na kwamba hivi sasa tuna jukumu la “kuimarisha” muungano, naamini hiyo siyo sababu ya kutufanya tusijadili nini kinaweza kutokea ikiwa muungano utavunjia ghafla.

Kujiepusha na vunjiko la ghafla la Muungano

Jaji Warioba na wazee wenzake walitumia busara kubwa wakati wanatuletea rasimu ya kwanza na ya pili ya Katiba. Wazee hawa waliweka wazi hali halisi inayolikabili taifa na huko linakokwenda, wakatuchorea mstari ambao tulipaswa kujiunga nao, mstari mpya wa kuwa na serikali tatu. Hoja ya serikali tatu si mpya, ilijadiliwa na kupitishwa na Chama cha Mapinduzi chenyewe mwanzoni mwa miaka ya 1990 na ikajadiliwa katika Bunge la Tanzania kwa msukumo mkubwa wa wabunge wa “G55” na baadaye Bunge likatoa maazimio kwa Serikali kuanza mchakato wa kwenda kwenye serikali tatu, nadhani baadaye Mwalimu Nyerere aliingilia kati na kupinga.

Mwalimu kama binadamu naamini alikuwa na uelewa wake na misimamo yake, lakini taifa halikupaswa kwa wakati huo kufuata ushauri wa mtu mmoja na kupuuza ushauri wa Bunge lililo na watu wengi na wanaotizama mbali zaidi ukiunganisha mawazo yao kuliko kutegemea mtu mmoja. Kitendo cha Mwalimu Nyerere kuingilia kati wakati ule na kufanikiwa kuzima hoja ya serikali tatu kilikuwa na maana Tanzania bado haijajijenga kitaasisi na inaongozwa kwa busara za watu au mtu, jambo ambalo ni hatari kwa taifa linalokua, kwamba maisha ya mamilioni ya Watanzania na fikra zao za mbele zinawekwa chini ya mtu mmoja na siyo taasisi kama Bunge au Serikali.

Mimi ni mfuasi mzuri wa falsafa za Nyerere na nakubaliana naye katika masuala mengi huku nikihoji na kupinga baadhi ya masuala muhimu. Ndiyo maana hata baada ya Nyerere kuondoka, Tume ya Jaji Warioba ambayo ilijaa watu waliofanya kazi na Nyerere muda mwingi, ilikuja na pendekezo la kuanzisha serikali tatu kwa utaratibu maalum wa kikatiba na bila kuleta mivutano. Ndiyo kusema kuwa mawazo ya kitaasisi juu ya muungano yanayonakishiwa na nguvu ya uono wa Watanzania wengi yaliendelea kuwa palepale hata baada ya baba wa taifa hili kututoka.

Kujaribu kuzima mawazo haya ni kurudi kulekule kwenye mielekeo ya kuongoza nchi kwa busara za mtu mmoja badala ya kuchukua mawazo na busara za wengi na kwa hakika, hali hiyo itatupeleka shimoni. Naloliona mimi ni kwamba, ikiwa nchi yetu haitaamua kuunda serikali tatu kikatiba na kwa kufuata taratibu, tutazidi kukaribia zaidi kwenye kuvunja muungano kuliko kuutengeneza. Siyo kweli kwamba kwa zama hizi za sasa CCM itaendelea kuwa na “control” kubwa Zanzibar na kwa makada wa chama hicho ndani ya Zanzibar.

Chanzo: Mwananchi

 

 

Advertisements

One Reply to “Ikiwa Muungano unavunjika, tutaingia vitani?”

  1. Ni wazi kuwa wakati ukuta na wakati ndio hutoa maamuzi. Kwa kipindi cha miaka ya sitini inawezeka kuwa serikali mbili zilikidhi kuongoza nchi kwa sasa ni serikali tatu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s