Waziri Mmarekani amuuliza JK utitiri wa wagombea urais

Rais Jakaya Kikwete akiagana na Makamu wa Rais wa zamani wa Sudani ya Kusini (kushoto),  Riek Machar Teny Dhurgon baada ya kufanya naye mazungumzo mafupi walipokutana jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini, juzi wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa  Marais na Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU), . Kulia ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete. Picha: Ikulu
Rais Jakaya Kikwete akiagana na Makamu wa Rais wa zamani wa Sudani ya Kusini (kushoto), Riek Machar Teny Dhurgon baada ya kufanya naye mazungumzo mafupi walipokutana jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini, juzi wakati wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Marais na Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU), . Kulia ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete. Picha: Ikulu

Dar/Mikoani. Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Waziri huyo aliuliza swali hilo usiku wa kuamkia Jumatatu (Juni 14, 2015) mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati anazungumza na Rais Kikwete kutokana na wanachama wa CCM 35 kujitokeza kuchukua fomu za kuwania urais.

Viongozi hao walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika, kwa siku mbili, kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Convention jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kumalizika jana.

Makada hao wa CCM wameibua upinzani mkali kwenye mbio za urais na hadi sasa hakuna dalili za mtu yeyote kuwa ana nafasi kubwa ya kupitishwa, hali ambayo imesababisha vyombo vya habari kubashiri kuwa mteule wa CCM anajulikana kwa viongozi wa juu wa chama hicho tawala.

Wakati nchi ikijiandaa kupata kiongozi mpya atakayeongoza Serikali ya Awamu ya Tano, mbio za urais ndani ya CCM zimevutia idadi kubwa ya wanachama ambayo haijawahi kutokea kabla na baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 baada ya watu 35 kuchukua fomu hadi sasa.

Mwaka 1995, wanaCCM waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Ali Hassan Mwinyi walikuwa 15 na mwaka 2005 waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Benjamin Mkapa walikuwa 11.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa mwanzoni tu mwa mazungumzo baina ya viongozi hao, Linda alimuuliza Rais Kikwete, “Je, unaye mgombea yeyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea”.

Baada ya swali hilo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete alijibu, “Sina mgombea ninayempendelea. Wagombea wote ni wa kwangu, ni wa chama changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali”.

Kuhusu utiriri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.

“Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya karibuni.

“Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”

Rais Kikwete alisema hana tatizo na wingi wa wagombea kwa sababu haiwezekani kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki yao.

Vile vile, alisema wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na pia ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka ndani ya chama na ni uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio.

Uchaguzi mkuu wa Marekani utafanyika mwakani na kwa mujibu wa taratibu zao, mchakato huanza mwaka mmoja kabla na wagombea hupatikana Juni ya mwaka wa uchaguzi.

Hadi sasa, makada wanne wa chama cha Democrats, ambacho kimeshika hatamu, wamejitokeza kuwania urais, wakati katika chama cha Republican, ambacho kina nafasi kubwa ya kushika madaraka mwakani baada ya kukaa nje kwa miaka 10, kuna makada 12 waliojitokeza.

CCM iteue kwa staili ya Papa

Katika hatua nyingine, mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina ameitaka Kamati Kuu ya CCM kutumia mfumo wa Vatican wa kujifungia na kuomba siku saba kabla ya kumpata Papa wakati itakapokutana kuteua mgombea urais wa chama hicho baadaye mwezi huu.

Katika mchakato wa kumchagua Papa, Makardinali kutoka sehemu mbalimbali duniani, hukutana kwenye mji wa Vatican na kujifungia katika mkutano wao (Conclave) wakiomba ili apatikane Papa na baada ya kukamilisha mchakato huo, moshi mweupe huonekana juu ya jumba la mkutano kuashiria kukubalika kwake kwa Mwenyezi Mungu.

“Mimi siwanii tena (ubunge), lakini ninachosema, tuache ushabiki… ninaondoka, lakini nina ushauri kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Kwanza ninawapongeza waliojitokeza kuwania urais lakini siyo yule msanii wa darasa la saba.

“Tuombe Mungu atupe Rais mzuri, anayependa watu, anayependa maendeleo ya watu, lakini na Kamati Kuu muanze kuomba Mungu kama anavyotafutwa Papa. Makardinali wanajifungia siku saba, wanaomba, wanaomba na ninyi ombeni. Sasa na sisi tusishabikie, tuache vikao vitaamua,” alisema Ntukamazina wakati akichangia mjadala wa bajeti bungeni.

Membe aibukia kwa Msuya

Jana wagombea wa CCM waliendelea na safari ya kutafuta wadhamini huku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliibukia kwa nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Cleopa Msuya.

Membe alifika nyumbani kwa Msuya eneo la Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufanya naye mazungumzo akitokea mkoani Tanga ambako aliahidi kuwa akibahatika kuingia Ikulu, kwanza atashughulika na bandari ya Tanga.

Katika mazungumzo yao, Msuya alisema anamuunga mkono Membe katika harakati zake za kugombea urais kwa kuwa anakidhi vigezo vilivyotajwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.

Msuya alisema ana matumaini CCM itamteua Membe kwa kuwa ni mgombea pekee ambaye hajawahi kukumbwa na kashfa na amekidhi sifa zinazohitajika.

Msuya alisema chama hicho hakipaswi kumchagua mgombea mwenye madoadoa ya ufisadi na uchafu kwa kuwa mgombea wa aina hiyo hatawatendea haki Watanzania.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa ngazi za madiwani, wabunge na rais, chama kinapaswa kuwatanguliza watu wenye sifa na vigezo ili kupata viongozi bora watakaowatumikia wananchi.

“Kama kweli Taifa linawachukia mafisadi na wenye kila aina ya madoadoa, chama hakipaswi kuwapitisha viongozi wa aina hiyo kwa kuwa

wataendeleza ufisadi huku Watanzania wakiendelea kuteseka,” alisema Msuya

“Kama tunachukia ufisadi na matendo machafu haya yanayoendelea kufanywa na baadhi ya watu katika Serikali yetu basi mgombea mwenye madoadoa hataweza kuwatendea haki Watanzania kwani wananchi wanahitaji mtu safi na asiyekuwa na aina yoyote ya uchafu,” alisema Msuya.

Pinda atikisa kwao

Mkoani Katavi; Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameanza mbio za kusaka wadhamini jimboni kwake Katavi ambako alipokewa kwa maandamano na kuchangiwa Sh1 milioni za kumsaidia kuzunguka katika mikoa mingine kutafuta wadhamini.

Pinda maarufu kama “Mtoto wa Mkulima” alipokewa kwa mabango yaliyoandikwa “Pinda siyo fisadi… ni mtoto wa mkulima… karibu nyumbani… wewe ndiye rais ajaye”, na alisindikizwa kwa maandamano yaliyowafanya askari kuwa na wakati mgumu kudhibiti ulinzi.

Baada ya kupata wadhamini 9,141 katika tarafa mbalimbali za mkoa wa Katavi, Pinda aliwashukuru na kueleza kuwa tukio hilo ni la kihistoria na kuwaomba wananchi waendelee kumwombea ili aweze kupata ridhaa ya chama chake na hatimaye kuwa rais.

Wasira na uchapakazi

Mkoani Njombe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira amesema uchapakazi na uaminifu wake ndio uliofanya kila Rais aliyepita ahitaji kufanya naye kazi.

Wasira, ambaye pia ni mbunge wa Bunda alisema hayo jana wakati akitafuta wadhamini katika mkoani Njombe. Alisema asingekuwa mwaminifu, angekuwa ameshawekwa pembeni kama ambavyo baadhi ya mawaziri wamefanywa.

“Nimekuwa sehemu ya uongozi wa Taifa letu kwa miaka kadhaa, nimeanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akaja Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, kwa hiyo ni walimu wangu wanne, uzoefu nilioupata kutoka kwao ni shule tosha kwangu ya kuliongoza Taifa hili,” alisema Wasira.

Bilohe na siri ya urais

Kada wa CCM anayewania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais, Edephonce Bilohe amesema hatishiki wala kuwaogopa wagombea wanaonunua watu kwa nguvu ya fedha kwa kuwa uongozi ni tunu kutoka kwa Mungu.

“Natambua kwamba nagombea nafasi hii kubwa zaidi nchini nikishindana na wasomi na matajiri, lakini kamwe sitishwi na hawa wagombea wanaojidai kuhonga viongozi na watu wengine ili wawaunge mkono,” alisema Bilohe.

“Tangu nikiwa mdogo tulikuwa tunaambiwa kwamba CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, ndiyo maana mimi nikiwa mkulima katika Kijiji cha Muzye na Mtala niliamua kwa moyo wangu wote kugombea urais ili niwawakilishe maskini wenzangu ambao ndio wengi katika jamii na sina shaka wataniunga mkono katika harakati zangu za kuingia Ikulu kuongoza Taifa,” alisema.

Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema: “Ni aibu nchi ya wastaarabu kama Tanzania, inayoongozwa na viongozi wasomi bado tunashuhudia mapigano ya wakulima na wafugaji wakigombea maeneo ya kulima na kuchungia mifugo.

“Nchi yetu ina ardhi kubwa isiyokaliwa na watu na haijawahi kutumika tangu dunia iumbwe, iweje sasa watu wauane kwa ajili ya ardhi? Hili nitalikomesha.”

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s