Mama Samia anapotetea ufisadi uchaguzini

Waziri Samia Suluhu Hassan
                                                  Waziri Samia Suluhu Hassan

 

Na Jabir Idrissa

UTHIBITISHO umekuja hadharani. Ndani ya Bunge tukufu la jamhuri, kiongozi mwandamizi wa CCM anataka CUF na UKAWA waweke mezani ushahidi kuwa mamia ya wanawake, wanaume na kundi la vijana, hawaandikishwi kuwa wapigakura.

 

Anataka wabunge wa UKAWA – Umoja wa Katiba ya Wananchi – wamkabidhi Spika Anne Makinda, picha za mnato na filamu zinazoonesha magari ya vikosi vya majeshi yamebeba vijana wakubwa na watoto wasiotimia umri wa kuchagua, yakiwapeleka kambini kuandikishwa, wakikabidhiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZAN-ID).

 

Bi Samia Suluhu Hassan, huyu waziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, anataka UKAWA wakabidhi picha zinazoonesha maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar – Zanzibar Electoral Commission (ZEC) wakiandikisha watoto hao.

 

Kwake yeye, Bi Samia, ukikabidhiwa ushahidi huo kwa Spika, ndipo Wazanzibari, Watanzania na Wadunia waamini tuhuma zinazotolewa na UKAWA bungeni, na CUF hadharani na wananchi mitaani. Vinginevyo waongo na wazandiki.

 

Hoja ya Bi Samia bungeni, ina maana moja kubwa: Haamini kuwepo mamia kwa mamia ya wanawake – wakubwa kwa wadogo – wanakosa kitambulisho cha uzanzibari na kura. Kwake, hakuna kitu kama hicho. Kwa hivyo, tuhuma zinazoelezwa, ni uzushi.

 

Bi Samia ni mwanamke mtu mzima, mbunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Muyuni, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini, Unguja, Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Alianza ubunge 2005, baada ya kutumikia uwaziri ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia 2000 alikoteuliwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, kupitia nafasi kumi za uteuzi unaofanywa na Rais wa Zanzibar, kwa mujibu wa Ibara ya 66 ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Inafafanuliwa na Kif. 41 cha Sheria Na.11 ya 2010.

 

Aliteuliwa akitokea mashirika ya kiraia alikojenga jina kwa utetezi jasiri wa haki za wanawake wa Zanzibar. Naam, akizitetea kwa nguvu pamoja na kinamama wenzake kama vile Mama Kibao.

 

Sina shaka ujasiri wake katika kupigania haki za wanawake, ndio ulimvuta Amani Abeid Karume aliposhika urais katika uchaguzi mchafu, na labda kwa ushawishi wa wakubwa wa CCM, kumteua aingie serikalini kusaidia pamoja na mengine, wanawake wenzake.

 

Aliongoza wizara ya Uwekezaji, Biashara, Viwanda na Masoko lakini mpaka anaondoka, na hadi leo hii, wanawake wengi Zanzibar ni masikini wa kutupwa. Kundi hili bado ndilo linalohemea maisha bora, chejio na mitaji ya kuanzisha/kuimarisha vijibiashara.

 

Hawajavuka mstari wa umasikini, pamoja na kulima mwani baharini kutoka Makunduchi, Kusini Unguja, mpaka Tumbatu, Kaskazini Unguja. Mwani umefifia badala ya kumkomboa mwanamke, kutokana na serikali kushindwa kutokomeza mfumo mbaya wa mauzo.

 

Wakubwa wa CCM wamempandisha bungeni. Akaingia Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano Tanzania (SMT) tangu 2005, akiwa waziri katika ofisi ya Makamo wa Rais wa masuala ya Muungano.

 

Hili eneo ni mwamba mkubwa usiomithilika. Ni tofauti na walivyo Waskochi kwa dola ya Uingereza. Hawezi kuuvunja ili kuisaidia Zanzibar. Mfumo uliobaki na serikali mbili usioisaidia kwa lolote Zanzibar, ikiwemo wananchi wa jimbo analowakilisha, Muyuni. Baadhi ya wanawake na wanaume wa jimboni kwake hawana kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, kwa hivyo hawawezi kusafiri kuingia Dar es Salaam kutafuta kazi wala kutibiwa baada ya maradhi yanayowasibu yakiwemo uvimbe kwa makumi kinamama, kushindikana kutibiwa hospitali kuu ya Mnazimmoja.

 

Kwa kukosa kitambulisho, hawapati tiketi ya kusafiria si usiku kwa Flying Horse, wala mchana kwa Azam Marine. Sharti uwe nacho ndipo upate tiketi. Tangazo lipo ukutani bandarini na kwa kila kampuni ya usafirishaji abiria Zanzibar.

 

Mama Samia hajali kitu. Kwake si tatizo. Anasema bungeni tuhuma ni uongo mpaka UKAWA wampe ushahidi Spika Makinda. Mle ndani, wabunge wa CCM wanamuunga mkono asemapo hayo – ndo tafsiri ya kimya chao.

 

Wamo Yahya Kassim Issa (Chwaka), Abdalla Sharia Ame (Dimani), Sylvester Mabumba (Dole), Waride Bakari Jabu (Kiembesamaki), Masauni Yussuf Masauni (Kikwajuni), Dk. Juma Abdalla Sadalla (Rahaleo) ambaye ni naibu waziri wa Afrika Mashariki, na Kwahani kwa Waziri wa Ulinzi Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi.

 

Majimbo yote hayo na wabunge wake, yanashikwa na CCM kama ilivyo Fuoni (Said Zubeir Mussa) ambako utaratibu umeandaliwa wa kulikata jimbo ili kuongeza ulaji kwao, pamoja na yale ya Magogoni, Mtoni na Nungwi yanayoshikwa na CUF, wananchi wake wananyimwa kitambulisho ili wasiandikishwe kwa sababu wakipewa haki yao, watapigia wagombea wa UKAWA.

 

Majimbo mengine mengi Unguja, likiwemo la Kitope kwa Balozi Seif Ali Iddi, na Pemba iliko ngome kuu isiyomenyeka ya CUF, kuna mamia kwa mamia ya wananchi wananyimwa ZAN-ID ili tu wasipate fursa ya kuandikishwa na kuingia kwenye daftari la wapigakura.

 

Viongozi wa CCM, wakiwemo hao waliopo mkutano unaohutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wao Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na ambao Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Iddi, amekimbizwa dakika za mwisho asiende kuhutubia kwa kukosekana watu wa kumsikiliza (picha inaonesha) – ilihitaji kumzuia ili kulinda ‘heshima yake kiuongozi’ – wanafurahia mwenendo na kuridhia mfumo wa kunyonga haki ya wananchi kushiriki uchaguzi.

 

Nini maana yake? Yale ninayoyatolea sauti hapa kwamba CCM inafanya maandalizi ya kuuvuruga uchaguzi ili tu ibaki madarakani kwa sababu, viongozi wenyewe wanasema hadharani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haipatikani kwa vijikaratasi. Wakitaka nao, wakilengwa wapinzani hasa CUF, wapindue kama 12 Januari 1964.

 

Wapinzani watapindua kwa njia ipi wakati mapanga, mashoka, majambia na bunduki zinamilikiwa na kuhodhiwa na dola inayoshikwa na CCM ambako CUF hawana chao pamoja na kuwa sehemu ya serikali iliopo.

 

Kwa mfumo ulivyofanywa wa kihafidhina, ari na moyo wa maridhiano vikizuiwa kutambaa hadi kwa wakuu wa idara, hawapiki wala hawapakui.

 

Kumbukeni, ilipata kusemwa na kiongozi mkubwa wa CCM katika kampeni za uchaguzi wa 2005, kuwa serikali ikichukuliwa kwa njia ya kura, “Tutashusha na kuyanoa yale mapanga na mashoka, bado tunayo, ili tuwapindue (CUF).”

 

Ukisikia CCM wanasema na kuimba “Mapinduziiiiiiii,” na wakiitikia “Daimaaa,” ujuwe hiyo – mapanga na mashoka tuyanoe tupindue – ndiyo maana halisi. Angalieni wanavyotekeleza, hawataki kusikia tuhuma za kunyimwa haki watu wasiingie kwenye daftari la kudumu la wapigakura (DKWK).

 

Habari iliyopo mjini ni kwamba mwenendo huu ni moja ya masuala makubwa aliyoyaeleza Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wa CUF, Makamo wa Kwanza wa Rais na mgombea ajae wa UKAWA kuwania urais.

 

Ni kutoa indhari kuwa mfumo unaolindwa na CCM unalenga kuzuia haki ya ushindi halali, badala yake, uje ushindi wa kishindo, unaoumiza matumaini ya Wazanzibari. Tatizo unaweza kuja na damu.

Ends.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s