Wasira: Hii ndiyo Tanzania ninayoitaka mimi

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira akiwahutubia wananchi kwenye Ukumbi wa Benki Kuu Tanzania (BoT) mjini Mwanza alipotangaza nia ya  kuwania urais kupitia CCM.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira akiwahutubia wananchi kwenye Ukumbi wa Benki Kuu Tanzania (BoT) mjini Mwanza alipotangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM.

Mwanza/Dar. Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ametangaza nia ya kuwania urais akisema iwapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera yake, atahakikisha utendaji wa Serikali yake unakuwa wa kitaasisi.

Alitangaza nia hiyo katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza jana Wasira alisema: “Baada ya kutafakari kwa makini nimeona uamuzi wa kugombea nafasi hii ya juu kabisa kwa nchi yetu ni sahihi na wakati muafaka, kwa kuwa nina nia ya kupeleka nchi hii katika ngazi ya juu kabisa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.”

Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya ITV na Star TV, Wasira alisema: “Leo nakuja hapa Mwanza kuvunja ukimya na kumaliza minong’ono kwa kutangaza rasmi kwamba nimekata shauri ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Wasira aliyekuwa ameongozana na mkewe na baadhi ya viongozi wa CCM, alisema angependa kuwaeleza Watanzania ni kwa nini amechukua uamuzi huo kwa kuwa jambo hilo si dogo.

 “Kwanza ni haki yangu. Raia wote wana haki ya kugombea, ni haki ya kikatiba. Lakini ninayo sababu nyingine ambayo ni kubwa zaidi, naifahamu vizuri Tanzania kwa muda mrefu tangu miaka ya 1970 nimeshirikishwa katika uongozi wa Taifa hili nikiwa na miaka 25,” alisema Wasira akibebwa na historia ya utendaji ya muda mrefu.

Wasira alitamba kuwa iwapo atateuliwa na CCM na kushinda urais, Serikali yake itasimamia uadilifu na kupambana na rushwa na amedhamiria kupandisha viwango vya maendeleo. Aliwaonya Watanzania kutothubutu kuukabidhi urais kwa mla rushwa, kwani kuna siku atauza Ikulu.

“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea.”

Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mara kwa mara, Wasira alisema kiongozi huyo aliwahi kusema kuwa rais wa Tanzania ni lazima achukie rushwa na anatakiwa aonekane kwa vitendo akiichukia… “Siku hizi kila kiongozi anakemea rushwa kama fasheni hata wala rushwa wanaikemea kwa sababu bila kufanya hivyo wanaona mambo yao hayatawanyookea.”

Kauli hiyo ya Wasira iliwafanya wafuasi wa chama hicho kusimama na kumshangilia huku wakiimba ‘Wasira sema usiogope.’

Alisema: “Mwalimu Nyerere aliwahi kuniuliza ninataka nini kati ya utajiri na kuongoza watu, alisema nikitaka utajiri nichague kuwa mfanyabiashara kwani nitanunua kwa bei rahisi na kuuza aghali.”

Alisema Nyerere alimweleza kuwa hawezi kuwa tajiri kwa kazi ya kutumikia watu kwa mshahara na kwamba mfanyabiashara ndiye anaweza kutajirika.

“Kwa hiyo nimewatumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali tangu nikiwa na umri wa miaka 25 lakini sijawahi kuhusishwa na kashfa za rushwa, nyie ni mashahidi sijawahi kuhusishwa na kashfa za Epa wala Tegeta Escrow,” alisema.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s