Wanamtusi Maalim Seif waliyemjenga wenyewe

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

Na Jabir Idrissa

WAKUU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawachoki kumshambulia Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, licha ya kuwa pia ndiye Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar.

Wala hawajali mashambulizi yao yanayofikia kumtusi na kumdhalilisha, kama binaadamu na kama kiongozi katika nchi, yameshindwa kumdhoofisha kisiasa.

Kinyume chake, wamezidi kumjenga na matokeo yake, ni hali inayojionesha ya kuimarika kwa CUF, chama alichokiasisi tangu 1992.

CUF imekua isivyo kawaida. Mafanikio yake yanaelezeka kirahisi hata kwa anayeichukia.

  • Kimefanikiwa kueneza itikadi yake ya utajirisho nchi nzima na ughaibuni.
  • Ni sehemu ya Serikali ikiwa na Makamo wa Rais na mawaziri saba.
  • Kimefuta kile wapinzani wake walichokiaminisha kuwa kina nguvu tu Pemba; kina wawakilishi na wabunge Unguja.
  • Kina taarifa nyingi za mipango ya kukihujumu.
  • Kimekuwa kimbilio kuu la wana-CCM.
  • Kimepokea mawaziri watatu wa zamani kutoka CCM.
  • Kimefanikiwa kukusanya raslimali nyingi kwa maandalizi ya uchaguzi ujao.
  • Ndio tumaini la maendeleo na maisha kwa Wazanzibari wakubwa na vijana.

Chama kimekuwa na nguvu kubwa kiasi cha kulazimisha wakuu wa CCM kukosa utulivu, kwa kuona kinapokwa madaraka.

Ile hali iliyokuwepo miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi 1992, ya baadhi ya wana-CUF kuhofia kuvaa hadharani sare za chama, sasa imehamia CCM.

Hali ni mbaya kwa CCM kwa sababu baada ya kushuhudia umma wa vijana ukiitenga CCM na kuchagua CUF, tena kwa fakhari wakikabidhiwa kadi na Maalim Seif, sasa mikutano ya CCM inadharauliwa na wananchi.

Kwa kuwa CCM haiaminiki tena, wengi hawajali kukosa hotuba za viongozi wake. Kule kuamini kuwa watakachosikia ni matusi zaidi, kumechangia kuwatenga na kutoona haja ya kuhudhuria mikutano ya chama hicho.

Wiki iliyopita, wakazi wa Magogoni na maeneo jirani, walisogelea mkutano wa hadhara uliotangazwa kwa siku mbili na kuahidiwa mhutubiaji mkuu angekuwa Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.

Masikini wee, hakufika mkutanoni, na hakuna sababu iliyotajwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, ya kutofika kwa kiongozi huyo.

“Mnamo saa 11.15 (saa 11 na robo) nilipita nikashuhudia watu wachache wanamsikiliza Spika wa Baraza la Wawakilishi,” amesema msomaji wa safu hii aliyenipigia simu Ijumaa wiki iliyopita.

Msomaji anasema baadaye alimpigia simu ndugu yake anayeishi karibu na uwanja wa Kwa Mabata, jimbo la Magogoni, ngome ya CUF, na kumuuliza mkutano ulivyomalizika.

“Ameniambia Balozi Seif hakufika mkutanoni. Anadhani maofisa wa usalama walimzuia kutoka kwa sababu mkutano ulikuwa na watu wachache sana,” anasema.

Nimethibitishiwa na vyanzo ndani ya CCM tukio kama hilo la Balozi kutofika kwenye mkutano wa CCM aliotarajiwa kuhutubia, inakuwa mazoea.

“Usishangae, mara nyingi dakika za mwisho Balozi anazuiwa kwenda mkutanoni kwani kumekosekana watu wa kumsikiliza. Ndiyo hali halisi, chama kina hali ngumu kwa kweli,” anasema.

Wananchi waliokuwa wamesimama kwa mbali uwanjani wakisikiliza, wengi wakionekana kama si wapenzi wa CCM, walianza kuondoka, walipomsikia Vuai akiporomosha kauli za uchochezi.

Vuai ambaye Machi mwaka huu alinukuliwa akitamba CCM itahakikisha Maalim Seif anabakia Makamo wa Rais na siyo Rais wa Zanzibar, alirudia kauli hiyo, safari hii akija na mapya yanayoonesha namna CCM walivyopanga kung’ang’ania madaraka, wakipuuza msingi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amenukuliwa na gazeti la Mwananchi, akisema, “… tunasema hata siku moja hawezi kuwa rais, haiwezekani na haiwezekani, kama anasema iko siku atakuwa rais, labda Mtambwe kwa sababu ana nia chafu na hawapendi Wazanzibari.

Mtambwe ndio kijiji cha nyumbani kwao Maalim Seif, ndani ya Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

“CCM imejidhatiti na kuhakikisha katika uchaguzi tunaendelea kushinda na kuchukua majimbo yote ya Unguja, baada ya kufanyika mabadiliko makubwa ya mipaka ya majimbo ya uchaguzi.”

“Hakuna jimbo la Magogoni wala Mtoni litakalotoka CCM na kuchukuliwa na CUF mwaka huu, tumejidhatiti.”

Vuai anasema serikali haitamvumilia mtu yeyote anayeazimia kufanya fujo. Akadai wao wanazijua mbinu za Maalim Seif za kutaka kuleta vurugu.

Wakati huo, Spika Pandu Ameir Kificho na Mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi, Yussuf Mohamed Yussuf, mbunge mstaafu Mwembemakumbi, walishampakazia Maalim Seif wakimtaja kama kiongozi mchochezi.

Yussuf alinukuliwa akimtaja Maalim Seif kama adui mkubwa wa Zanzibar na Wazanzibari, ndo maana “amekuwa akizorotesha misingi ya Mapinduzi na Muungano.”

Kificho aliye nadra kuhutubia mikutano ya hadhara, alisema Maalim Seif anatoa kauli zinazohatarisha amani wakati ni mmoja wa viongozi wakuu serikalini.

Aliipigia chapuo Katiba Inayopendekezwa ambayo aliisimamia ipitishwe licha ya kukosa maslahi yaliyotarajiwa na Wazanzibari.

Lakini akigusia Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema misingi yake ikitetereka, itavuruga mshikamano wakati “Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara wanafikia laki tano (500,000) ambao muungano ukivunjika Zanzibar itashindwa pa kuwaweka.”

Hakugusia chochote kuhusu mbinu za CCM kuwakusanya kama dagaa Watanzania wa Bara na kuwapeleka Zanzibar unapokaribia uchaguzi ili waibebe CCM kwa kura za hila.

Bali hajasema lini waliogoma kuondoka Zanzibar baada ya uchaguzi, watarudi Tanganyika. Na ajue Zanzibar kama nchi ya visiwa ina haki, kulingana na sheria za kimataifa, ya kulindwa isivurugwe silka zake.

CCM inaumia sasa kwa mbinu zake kufichuliwa. Isipotengeneza hofu mitaani, CCM haina maringo na haichaguliki. Uonapo viongozi wake wanazidisha mashambulizi kwa Maalim Seif, ni kwa vile tu anazianika njama zao.

Analaumu kuitumia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Idara inayotoa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, kutafuta ushindi wa nguvu. Ni kujiandaa na anguko la kihistoria.

Nguvu wanazoongeza za propaganda zinasema dhahiri kuwa arobaini ya CCM imefika. Hakuna Donge, hakuna Makunduchi, hakuna Kiembesamaki wala Kikwajuni. Anguko tu.

Tena anguko mbele ya matumizi ya vikosi vya ulinzi na usalama wa taifa. Wakati haukubali tena hila, vitisho, ulaghai na uongo.

CCM inatumia yote hayo, huku CUF imempokea Juma Hamad Omar, waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii wakati wa uongozi wa Ali Hassan Mwinyi, na Mohamed Hashim Ismail, naibu waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar.

Hamad amejisogeza kwenye uteuzi wa kugombea ubunge jimboni Wawi, ambako Hamad Rashid Mohamed ametema kiti akitangaza kugombea urais kupitia Alliance for Democratic Change (ADC) alichokiasisi baada ya kufukuzwa 2013.

Hashim ambaye pia aliongoza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), mfano wa TRA, amejisogeza kwenye uteuzi wa kugombea uwakilishi kwao Dimani.

CUF tayari inaye Mansour Yussuf Himid, shujaa aliyeapa kuipigania Zanzibar yenye mamlaka kamili tangu akiwa waziri wakati wa Amani Karume na Dk. Shein. Wameichagua haki.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s