Uchaguzi Mkuu, CCM sasa rasmi

Mke wa Rais, Salma Kikwete akimsalimia mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya CCM, Stephen Wasira mjini Dodoma jana. Wajumbe wengini ni Raphael Chegeni (wa pili kushoto) na Profesa Mark Mwandosya. Picha: Mwananchi
Mke wa Rais, Salma Kikwete akimsalimia mjumbe mwenzake wa Halmashauri Kuu ya CCM, Stephen Wasira mjini Dodoma jana. Wajumbe wengini ni Raphael Chegeni (wa pili kushoto) na Profesa Mark Mwandosya. Picha: Mwananchi
  • Wagombea urais kuchukua fomu Juni 3 na Julai 2
  • Ubunge na udiwani ni Julai 15 na kurejesha Julai 19
  • Mwingulu ajiuzulu unaibu katibu mkuu kuwania urais

Dodoma. Mbio za kuwania urais na nafasi nyingine kupitia CCM zimetangazwa rasmi baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoa ratiba ikibainisha kuwa mgombea urais chama hicho tawala atajulikana Julai 12, siku mbili baada ya yule wa Zanzibar kufahamika.

“Sasa ni ‘ruksa’ kwa wanaotafuta uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama katika nafasi za urais, ubunge, udiwani na uwakilishi kuchukua fomu kwa tarehe zilizopangwa,” Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana mjini hapa. Wanaotaka kuwania urais wataanza kuchukua fomu kuanzia Juni 3 hadi Julai 2.

Nape alisema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, utafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12. Alisema mgombea urais wa Zanzibar, atapitishwa na NEC Julai 10.

Mara baada ya kupitishwa kwa ratiba ya mchakato huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba alijizulu wadhifa huo ili kupata fursa ya kuwania urais.

Naibu Waziri huyo wa Fedha, alimwandikia mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuomba kuachia ngazi, naye akampa nafasi kueleza nia hiyo mbele ya kikao.

Akizungumza mkutanoni hapo, Mwigulu alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa hawezi kuwa refa na mchezaji.

Kutokana na uamuzi huo, Rais Kikwete alimteua aliyekuwa msaidizi wake kisiasa, Rajab Luhavi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu na kuchukua nafasi ya Mwigulu.

Uchukuaji fomu urais

Akizungumzia utaratibu wa uchukuaji fomu alisema kwa wanaowania kuteuliwa kugombea urais wataanza kuchukua fomu hizo Juni 3, mwaka huu na mwisho wa kuzirejesha ni saa 10.00 jioni ya Julai 2.

Alisema muda huo wa Juni 3 hadi Julai 2, pia utatumika kwa wagombea urais kutafuta wadhamini 450 katika mikoa 15, kati ya hiyo mitatu ikiwa ya Zanzibar, kwa maana ya Pemba na Unguja.

Utaratibu wa zamani kwa wagombea uliwataka kuwa na wadhamini 250 katika mikoa 10, miwili iwe ya Zanzibar. Pemba mmoja na mwingine Unguja.

Alisema hatua hiyo ya wadhamini 450 imetokana na kuongezeka kwa idadi ya wanachama na mikoa na kwamba idadi hiyo haitakiwi kupungua wala kuzidi.

Mikoa ya Bara imeongezeka kutoka 20 hadi 25 na Zanzibar imebaki mitano, Unguja mitatu na Pemba miwili.

“Safari hii ukija na wadhamini zaidi ya 450 unarudi nao nyumbani kwako, sisi hatuwataki hao wengine,” alisema.

Akizungumzia masharti ya uchukuaji fomu, alisema chama kimepiga marufuku mbwembwe na shamrashamra katika uchukuaji na urudishaji wa fomu.

Nape alisema masharti mengine ni wajumbe wa NEC kutotakiwa kuwadhamini wagombea, kwa sababu wao ni waamuzi katika vikao vya juu… “Pia mwanachama haruhusiwi kumdhamini mgombea zaidi ya mmoja.”

Vikao vya mchujo

Kuhusu vikao vya uchujaji wa wagombea urais, Nape alisema Kamati ya Usalama na Maadili itafanya kikao chake Julai 8, kuangalia utaratibu wa kanuni kama haukuvunjwa na kitafuatiwa na Kamati Kuu Julai 9 na kisha NEC Julai 10.

Urais Zanzibar

Nape alisema tarehe za uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa Zanzibar, zinafanana na zile za wagombea wa urais wa Muungano.

Alisema Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar, itafanya kikao chake Julai 4, ikifuatiwa na Kamati Maalumu Julai 5.

Alisema kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika Julai 9, kitapitia majina ya wagombea watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo.

 “Watatakiwa watafute wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu ya Zanzibar, lakini angalau mkoa mmoja uwe Pemba au Unguja,” alisema.

Ubunge, uwakilishi na udiwani

Nape alisema wagombea wa nafasi hizo watachukua fomu Julai 15 na kuzirejesha Julai 19, saa 10.00 jioni… “Kampeni zitaanza Julai 20 na kumalizika Julai 31 mwaka huu.”

Alisema Agosti Mosi mwaka huu, itakuwa ni siku ya kupiga kura za maoni kwa wagombea wa ngazi zote.

Gharama za uchaguzi

Nape alisema gharama za kuchukua fomu zipo kikanuni na hazijabadilishwa. Alisema fomu ya kuwania urais ni Sh1milioni, ubunge ni Sh100,000 na udiwani ni Sh50,000.

“Sisi hatufanyi biashara. Gharama zipo kwenye kanuni,” alisema.

Akizungumzia jinsi ya kuzuia rafu katika uchaguzi, alisema chama kimeweka mikakati ya kudhibiti kadi feki kwa kutaka kila mwanachama kuwa na kadi nyingine (kadi ya benki, mpigakura au kitambulisho cha kazi) kuthibitisha uhalali wake.

“Daftari la wanachama tutalifunga Julai 15 ili tuweze kufanya uhakiki wa wanachama,” alisema.

Sadifa asusa

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM) Taifa, Sadifa Juma Khamis jana aliondoka kabla ya muda wa kikao cha NEC kumalizika, akieleza kukasirishwa na mabadiliko kuhusu uteuzi wa viti maalumu kundi la vijana kuhamishiwa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (UWT).

“Itakuwaje nafasi za vijana wachaguliwe na watu wenye umri zaidi ya miaka 40. Naondoka zangu nakwenda Zanzibar,” alisema Sadifa na kuondoka katika viwanja vya White House ulipofanyika mkutano wa NEC.

Akielezea uamuzi huo, Nape alisema NEC imeamua kulipeleka jukumu la uteuzi wa mwisho wa wabunge UWT. Hata hivyo, alisema kura za mwisho tu ndizo zitakazopigwa na UWT kwa kundi hilo.

Alisema NEC imeongeza viti maalumu viwili kutoka Baraza lake la Wazee.

Uchaguzi

Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu Tanzania la CCM leo linafanya mkutano mkuu ambao utachagua viongozi wa ngazi ya Taifa.

Katibu Mtendaji Mkuu wa shirikisho hilo, Christopher Ngubiagi alisema mkutano huo utakaofanyika katika ukumbi wa Kilimani na utafunguliwa na Rais Kikwete.

Dk Shein afiwa, aondoka kikaoni

Wakati mkutano ukiendelea, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein alilazimika kuondoka Dodoma kutokana na msiba wa dada yake, Fatma Mohamed Shein (72) uliotokea jana.

Fatma aliaga dunia saa 4.30 asubuhi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar alipokuwa amelazwa kwa muda kutokana na maradhi ya saratani.

Msemaji wa familia ya marehemu, Said Mohamed alisema mipango ya mazishi itawekwa bayana leo baada ya kuwasili Rais Shein. Fatma aliwahi kupelekwa India kwa matibabu na kurejeshwa katika Mnazi Mmoja alikolazwa mara mbili.

Mohamed alisema mazishi yatafanyika katika makazi ya familia Kidongo Chekundu, Mjini Magharibi. Fatma ameacha mtoto mmoja, Saih Mohamed Ali

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s