Utawala unapogeuzwa na kuwa wa “sisi kwa sisi”

Rais wa Angola, José Eduardo dos Santos akiwa na mke wake wa tatu Ana Paula dos Santos. Nyuma yao ni Isabel dos Santos (anayepiga makofi) akiwa na mume wake Sindika Dokolo Mjini Luanda
Rais wa Angola, José Eduardo dos Santos akiwa na mke wake wa tatu Ana Paula dos Santos. Nyuma yao ni Isabel dos Santos (anayepiga makofi) akiwa na mume wake Sindika Dokolo Mjini Luanda

Na Ahmed Rajab

KUNA mizaha na mizaha. Si mizaha yote huwa ya aina moja. Mingine huchekesha; mingine huliza. Mfano wa mzaha wa aina hii ya pili niliuona Jumanne iliyopita nilipokuwa nikisoma gazeti moja la Angola kwenye intaneti.

Kichwa cha maneno cha makala moja kilichoandikwa kwa hati za kukoza kilinadi hivi: “Presidente recebe prémio de boa governação.” (Rais amepokea zawadi kwa utawala bora.)

Kichwa hicho cha maneno kilinivutia mno kwani ilinipitikia, ingawa sijui kwa nini, kwamba anayezungumzwa ni Rais wa Kiafrika. Lakini ni yupi? Kwa vile hakijamtambulisha huyo Rais mhusika nikataka kuendelea kuyasoma makala ili nijuwe ni Rais gani huyo aliyebahatika kwa kutunukiwa tuzo hiyo inayotolewa Dubai na taasisi moja iitwayo MeAfrica.Kumbe makala yakinicheza shere.

Ilikuwa wazi kwamba niliutumia muda wangu kusoma kichekesho — jambo la kuchekesha lakini lisilochekesha. Ni mzaha wa karaha, wa kutia haya.

Nilipoendelea kulisoma gazeti hilo liitwalo Jornal do Angola ndipo nilipotanabahi kwamba Rais mwenye bahati yake ni Rais José Eduardo do Santos. Na hicho ndicho kichekesho kwani huyu ni Rais aliye madarakani Angola kwa jumla sasa ya miaka 36 na wala haonyeshi dalili ya mtu mwenye kufikiria kung’atuka.

Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos na Mkewe Ana Paula katika Mji Mkuu Luanda
Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos na Mkewe Ana Paula katika Mji Mkuu Luanda

Do Santos, ambaye mitaani watu humwita kwa jina la utani la “Zedu,” ni kiongozi anayeongoza nchi kwa msingi wa “sisi kwa sisi.” Amekwishaigeuza Angola nzima iwe kama ni yake peke yake, yeye na familia yake na wenzake.

Do Santos ameoa mara tatu, ana watoto sita na mmoja amemzaa nje ya ndoa.

Inakisiwa kwamba thamani ya utajiri wake binafsi Do Santos imepindukia dola bilioni 20. Ndipo tunapojiuliza inawezekanaje Rais mwenye kazi ya kuendesha serikali ya nchi yenye wakazi masikini kama Angola akaweza kujikusanyia mali yote hiyo? Anazigawa vipi saa zake 24 za kila siku? Saa ngapi anazitumia kuendesha nchi na ngapi kujikusanyia mali?

Anapoamka asubuhi na kutwa nzima akili yake inakuwa wapi? Katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo na shida za wananchi wenzake au inakuwa katika kutafuta njia za kujilimbikia mali zaidi? Rais wa sampuli hiyo anaweza kweli kuongoza serikali yenye utawala bora?

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea salamu za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano kutoka kwa Rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos uliowasilishwa kwake na Waziri wa Serikali za mitaa(local Governments) Mhe.Bornito De Sousa ikulu jijini Dar es Salaam
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea salamu za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano kutoka kwa Rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos uliowasilishwa kwake na Waziri wa Serikali za mitaa(local Governments) Mhe.Bornito De Sousa ikulu jijini Dar es Salaam

Utawala wa Do Santos hauna sifa zozote za kuufanya ustahili kuitwa “utawala bora.” Kwa hakika, Do Santos asingalithubutu kuifanya nchi hiyo iwe hivi ilivyo lau angekuwa na utawala bora. Ukiupima na kuutathmini utawala wa Do Santos utaona kwamba utawala huo, kwa kila hali na kila kipimo, ni utawala mbovu.

Una mengi yenye kufanana na tawala za nchi kadhaa za Kiafrika, ukiwemo wa Tanzania. Zote hizo hazina mfumo thabiti wa kidemokrasia. Taasisi zake za kuusimamia utawala bora ni hafifu. Mahakama zake si huru, wananchi wananyimwa haki zao za kidemokrasia na hata za kibinadamu, vyombo vya habari vinaminywa na kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia.

Nchini Angola, hivi karibuni kwa mfano, wanaharakati wa lile lijiitalo Vuguvugu la Kimapinduzi walizuiwa na polisi wasifanye maandamano ya kudai hali bora za maisha katika manispaa ya Rangei. Wakitaka wapatiwe maji safi, umeme na manispaa yao iwe inasafishwa.

Haya ni madai ya kimsingi ambayo serikali ya Angola imeyapuuza na imetumia nguvu dhidi ya wenye kuyadai. Huo ni mfano mwingine wa utawala mbovu, tena ulio muovu.

Mfano mwingine ni namna majeshi ya Angola yanavyowakandamiza waumini wa dini tofauti. Kwanza ilikuwa Waislamu ambao kwa muda wa miaka kadhaa wamekuwa wakinyimwa haki yao ya kuabudu bila ya pingamizi. Hivi karibuni imekuwa zamu ya Wakristo wa madhehebu ya Seventh Day Adventist.

Mwezi uliopita serikali iliyapiga marufuku makundi tisa ya Wakristo katika mkoa wa Huambo na kwa mujibu wa wapinzani waumini wanaofika 1,000 waliuliwa na polisi. Serikali imezikanusha shutuma hizo. Lakini waliozitoa shutuma hizo wanasema wanao ushahidi wa kuyathibitisha madai yao.

Ukandamizaji wote huo unafanywa na utawala wa Do Santos. Kwa hivyo, yeye hawezi kuwa mfano wa mtu mwenye kuongoza “utawala bora.” Kadhalika, licha ya mapatao makubwa yanayopatikana kutokana na mauzo ya mafuta, almasi, chuma cha pua, dhahabu pamoja na madini mingine serikali ya Angola imeshindwa kuwatumikia ipasavyo wananchi wake.

Angola bado ni nchi ambayo thuluthi mbili ya wakazi wake hawawezi kupata maji safi na zaidi ya nusu ya wakazi wake ni mafukara.  Hali za wengi wa wakazi wa Angola ni duni ijapokuwa kwa mujibu wa takwimu rasmi uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukikua tangu baada ya kumalizika vita baina ya majeshi ya serikali na majeshi ya chama kikuu cha upinzani, Unita.

Utajiri mkubwa wa Angola umeiwezesha serikali ya huko kuanzisha Mfuko wa Utajiri wa Angola, Fundo Soberano de Angola (FSDEA) au kwa Kiingereza “Angola Sovereign Wealth”, Oktoba 2012. Mfuko huo ulianzishwa ukiwa na akiba ya rasilmali ipatayo dola za Marekani bilioni 5. Mwenyekiti wa Mfuko huo ni Jose Filomeno de Sousa dos Santos, mtoto mkubwa wa Rais Do Santos.

images (1)

Hayo yana maana kwamba akian Do Santos, baba na mwana, ndio wenye kuuhodhi utajiri wa taifa la Angola. Tukimuacha huyo mwanawe Rais wa kiume kuna na binti yake aitwaye Isabel tuliyewahi kumtaja zamani. Isabel ni mtoto wa Do Santos aliyezaa na mkewe wa mwanzo aliyezaliwa Urussi, Tatiana Kukanova. Walikutana Azerbaijan alipokuwa Do Santos anasoma huko.

Isabel amezishika biashara utadhani ana mikono ya pweza.  Anamiliki kampuni mbalimbali kwao Angola, São Tomé and Príncipe (ambako ndiko wazazi wa Rais Do Santos walikozaliwa), Ureno, Brazil, Gabon na kwingineko.

Inasemekana kwamba Isabel do Santos ni mwanamke wa kwanza wa Kiafrika aliye bilionea. Inakisiwa kwamba thamani ya utajiri wake inafikia dola bilioni tatu. Ni bilionea mwenye kuichezea rasilmali ya Angola bila ya pingamizi. Hamna shaka yoyote kwamba Isabel asingaliupata utajiri wote huo ingalikuwa yeye si binti wa Rais wa nchi yake.

Azma ya Mfuko wa Utajiri wa Angola ni kuyaweka kando mapato yanayopatikana kutokana na mauzo ya mapipa 100,000 ya mafuta kwa siku na kuzitumia fedha hizo kugharimia miradi mbalimbali ya miundombinu.

Waziri Mkuu, Mizengio Pinda akisalimiana na Rais wa Angola Jose Edwardo dos Santos katika kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleoo ya Nchi za Kusini mwa Afika
Waziri Mkuu, Mizengio Pinda akisalimiana na Rais wa Angola Jose Edwardo dos Santos katika kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleoo ya Nchi za Kusini mwa Afika

Utawala huo wenye uvundo wa ufisadi unawakera wengi nchini Angola hata miongoni mwa wakereketwa wa chama kinachotawala cha MPLA. Wanauona utawala huo kuwa ni uliofurutu ada kwa namna unavyoidekeza familia ya Rais na unavyoupepea utawala mbovu wa Do Santos.

Na si Do Santos na familia yake peke yao wanaonufaika na mfumo wa utawala mbovu wa Angola. Kuna majemedari wa jeshi, vigogo vya chama kinachotawala cha MPLA pamoja na marafiki wa Do Santos na wanawawe ambao pia wanauchota bila ya hofu utajiri wa umma wa Angola.

Kwa vile Do Santos ameanza kuzeeka kuna wanaosema kwamba kazi kubwa anayoifanya siku hizi ni kumjenga mwanawe wa kiume ili baadaye akirithi kiti chake cha urais.

Ajabu ya maajabu ni ya mtu kama huyu kuambiwa kwamba ati anaongoza utawala bora na kufika hadi hata ya kutunukiwa tuzo. Haya yamenifanya niyakumbuke maneno aliyowahi kunambia rafiki yangu mmoja kwamba: “wanapotaka kukutumia watakupamba kwa kila aina ya sifa ili wakutumie.” Watakwita “nguzo ya amani” au mwenyekiti wa jopo hili au jopo lile la kimataifa.

Haya tuliyashuhudia katika enzi ya vita baridi kwa kina Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire na bado yanaendelea. Mobutu na wengine waliovumiliwa, walitumiwa na baadaye wakabwagwa walipoonekana kuwa hawana tena thamani.

Siku hizi kundi jipya la viongozi wa aina hiyo limeibuliwa kwa jina la “walinzi wa demokrasia na utawala bora” licha ya kuwa wanafahamika wazi kuwa ni wakandamizaji, kwa viwango tofauti, wa demokrasia na haki za binadamu. Kama wao wenyewe hawakandamizi basi huwafungia macho washirika wao walio nchini mwao pamoja na walio nje ya mipaka ya nchi zao.

Mara ngapi tunawasikia marais wetu wakiyatetea majeshi yao au polisi wao wanapokuwa wanawakandamiza wananchi. Yanapotokea hayo wakuu wa dunia hii huwanyamazia kimya marais wetu na hata huwaunga mkono madhali maslahi yao hayamo hatarini.

Huu ndio unafiki wa kimataifa unaoisumbua dunia ya leo. Mizimwi inayotula tunaijuwa wenyewe lakini hutokea vidudu mtu vya kimataifa vikatupangia ni nani kati ya waovu wetu wenye utawala bora.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

CHANZO: RAIA MWEMA

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s