Maalim Seif: Sijachoka, nitagombea tena Urais Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi walioongozwa na Mhariri Mtendaji, Frank Sanga (wa tatu kulia) walipomfanyia mahojiano maalumu kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi walioongozwa na Mhariri Mtendaji, Frank Sanga (wa tatu kulia) walipomfanyia mahojiano maalumu kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
  • Asema anajiandaa kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu

Salma Said

Siasa za Zanzibar ni baina ya vyama viwili pekee  vya siasa. Chama tawala CCM na chama kikuu cha upinzani CUF. Vyama hivyo viwili vimekuwa katika ushindani mkubwa tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi nchini na kuingia katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Katika vipindi vinne vya uchaguzi, CUF imekuwa ikimsimamisha Maalim Seif Sharif Hamad kuwania urais, Zanzibar, huku  washindani wao CCM, wakifanya mabadiliko ya wagombea wake.

Kama ilivyo ada, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif ametangaza nia yake ya kugombea tena nafasi ya urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao na kusisitiza kwamba suala la yeye kuingia madakarani atakaposhinda halina mjadala.

Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na kamati maalumu ya (CUF) Zoni ya Mjini iliyokwenda kumdhamini kugombea nafasi hiyo huko nyumbani kwake Mbweni, Maalim Seif alisema anatarajia kugombea tena nafasi hiyo ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar kama alivyowaahidi mwaka 1988.

Maalim Seif akionesha fedha alizokabidhiwa na wafuasi wa chama hicho shilingi milioni mbili na nusu
Maalim Seif akionesha fedha alizokabidhiwa na wafuasi wa chama hicho shilingi milioni mbili na nusu

“Nimekuwa nikiulizwa na waandishi wa habari kwamba  vipi nitagombea tena urais. Naam, natangaza rasmi kuwa, ndiyo nitagombea tena. Mimi siyo kama CCM wanaoogopana,” anasema Maalim Seif.

Anasema tangu mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, CUF kimekuwa kikiibuka mshindi katika chaguzi zote, lakini hakikupata kutangazwa hata mara moja kuwa ndicho kilichoshinda. mwaka huu hili halitatokea tena.

Maalim Seif anasema CUF hakijapata kufanya maandalizi makubwa na yenye ufanisi katika chaguzi zote zilizofanyika kama kilivyofanya kwenye uchaguzi huu na kujigamba kuwa hakuna sababu ya chama hicho  kushindwa.

“Tumejiandaa vya kutosha, watake wasitake tutachukua nchi, mara hii Tume ya Uchaguzi ikitutangaza au isitutangaze sisi tunachukua serikali Insha Allah,” anasisitiza Maalim Seif.

Anasema tayari wagombea wa chama hicho wamejipanga katika kuwania nafasi mbalimbali za ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Wenyewe mmeona jinsi tulivyojiandaa kuchukua serikali na si mmeona tulivyojitayarisha na hatutaki mchezo matayarisho yetu tuliyoyafanya mara hii ni makubwa kwa sababu suala la kuwa Maalim Seif atafuatwa na ataombwa akubali matokeo safari hii nasema haliwezekani,” aliongeza Maalim Seif.

 

Vipaumbele

Akielezea mambo ambayo atayapa kipaumbele katika uongozi wake, Maalim Seif anasema CUF kitakapoingia Ikulu ya Zanzibar kazi kubwa itakayofanyika ni kutengeneza misingi ya utawala bora, misingi ya kuwa na uchumi ulio imara na kuwaunganisha Wazanzibari ambao wamekuwa wakibaguliwa chini ya uongozi uliopo sasa.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, anasema wananchi wa Zanzibar wameshaamua kukikubali chama cha CUF baada ya kuona ndiyo tegemeo lao la kuikomboa Zanzibar kiuchumi, kuwarahisishia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii pamoja na kulinda hadhi na heshima ya Zanzibar.

Anasema jambo lingine ambalo Wazanzibari wategemee chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF, ni kuimarika kwa huduma za kijamii, zikiwamo huduma za afya, maji na elimu bora ambayo itamuwezesha kijana aliyehitimu Zanzibar kumudu ushindani na kijana kutoka nchi yoyote ile.

 

Msimamo  wake kuhusu Muungano

 

Akizungumzia Muungano, Maalim Seif anasema mfumo uliopo una kasoro nyingi ambazo zimekuwa zikiwaumiza wananchi wa Zanzibar na kuleza kuwa akiwa Rais watapata fursa ya kuulizwa iwapo wanataka Muungano huo na uwe wa aina gani, ili kuwapo usawa kati ya pande zote mbili.

Maalim Seif anasema baadhi ya viongozi wa upande wa Tanzania Bara kwa kauli zao wanazozitoa, hawana nia njema kwa Zanzibar na ni wazi nia yao ni kuona Zanzibar inafutika kabisa katika ramani ya dunia.

 “Wanaonekana nia yao ni kuimeza Zanzibar, lakini dua zenu zimesaidia, imekuwa kama tembo aliyemeza chura na amemkaa kooni, lazima atamtema tu,” anasema Maalim Seif.

 

Wachambuzi wanamzungumziaje?

 

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka anasema, Maalim Seif hakupaswa kushawishiwa kugombea urais wa Zanzibar kwa sababu tangu uchaguzi wa mwaka 1995 anagombea nafasi hiyo na hajawahi kufanikiwa kuipata, hivyo anatakiwa kutambua kwamba ana kasoro na ndiyo maana hakubaliki.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka

Anasema Maalim Seif anatakiwa kupumzika na kumwandaa mtu mwingine kuwania nafasi hiyo ya urais badala ya kung’ang’ania yeye kila uchaguzi unapofika.

Akitofautiana na kauli ya Shaka, Enzi Talib Aboud afisa wa serikali aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ukurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, anasema licha ya umri mkubwa wa Maalim Seif , bado ana uwezo wa kufikiri na kubuni mambo makubwa katika taifa.

Enzi Talib Aboud
Enzi Talib Aboud

Enzi Talib anamuelezea Maalim Seif kuwa ni mtu mwenye sifa ya uhodari na ana subira kwani ni viongozi wachache ambao wamepata tabu katika maisha yao lakini hawajaweza kurudi nyuma wala kukata tamaa.

“Maalim Seif ana subira sana ingekuwa mtu mwingine angeshakata tamaa, lakini yeye angalia mambo aliyofanyiwa na bado yupo sawa halipizi kisasi na ni kiongozi jasiri, kumbuka siasa za Zanzibar zinahitaji mtu jasiri asiye na woga,” anasema Talib.

Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) Kassim Suleiman akielezea uamuzi wa Maalim Seif kuchukua fomu anasema siyo vibaya kujaribu kwa mara nyingine kwa kuwa ni haki yake kidemokrasia.

“Jambo muhimu mtu anayetaka kuwania Urais ni kuwa  na uwezo wa kiafya na hiyo haimzuii Maalim Seif.”

Lakini akasisitiza iwapo kama kuna watu wengine ambao wanataka kupimana nguvu na Maalim Seif wajitokeze.

 Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s