Mawaziri wawili CUF watupwa kura za maoni

Haji Faki Shaali
Haji Faki Shaali

Zanzibar. Mawaziri wawili wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF na wabunge wengine wakongwe wa chama hicho wamepigwa mwereka kwenye kura za maoni za kutafuta wagombea wa nafasi za uwakilishi na ubunge kwa majimbo 50 ya Zanzibar.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF, Omary Ali Shehe alisema matokeo hayo ni ya awali.

Walioangushwa ni waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Haji Faki Shaali ambaye ameangushwa katika Jimbo la Mkanyageni, sambamba na mbunge wa jimbo hilo, Mohamed Habib Mnyaa na Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame katika nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Nungwi.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali, kura hizo zimewatupa waandishi wa habari waliokuwa wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali akiwamo mtangazaji mkongwe wa BBC, Ally Saleh ‘Alberto’ ambaye ameangushwa na mbunge wa sasa wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ibrahim Mohamed Sanya.

Wengine ni Talib Ussi Hamad wa Mwananchi aliyepata kura 31 katika nafasi ya ubunge Jimbo la Magogoni na kutanguliwa na Juma Kombo Hamad aliyepata kura 106 huku mbunge anayemaliza muda wake Kombo Khamis Kombo akiambulia kura 61.

Mwandishi wa Majira, Mwajuma Juma alishika nafasi ya pili, baada ya kupata kura 11 akiwania nafasi ya uwakilishi jimbo la Amani, ambapo Khamis Rashid Abeid aliibuka kidedea kwa kura 22, huku mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Maua Mohamed Mussa akishika mkia katika nafasi aliyokuwa akiwania ya ubunge wa viti maalumu, Wilaya ya Mjini.

Mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Najma Khalfan Juma alipata pigo mara mbili baada ya kuanguka katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Ziwani na nafasi ya ubunge viti maalumu kupitia Wilaya ya Chakechake, Pemba.

Kwa upande wa uwakilishi wa viti maalumu Wilaya ya Mjini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amepenya kwenye tundu la sindano kwa ushindi wa kura moja, baada ya kupata kura 91, akifuatiwa na Nunuu Salim Rashid aliyepata kura 90 na mtoto wa mbunge wa Mji Mkongwe, Rahma Ibrahim Sanya aliyepata kura 30 huku kura nne zikiharibika.

Mbunge wa Mtambile, Mohamed Abdallah Salim naye ameanguka katika kura za maoni sambamba na mwakilishi anayemaliza muda wake, Mohamed Haji Khalid huku Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Dk Alley Soud Nassor akijitoa kabla ya uchaguzi na nafasi hiyo ya uwakilishi kunyakuliwa na Abdallah Bakar Hassan.

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi wa CUF kutoka Jimbo la Chonga, Abdallah Juma Abdallah ameanguka katika kura hizo pamoja na mbunge wa jimbo hilo, Haroub Mohamed Khamis huku Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), Omar Ali Shehe akishinda kwa kura tisa baada ya kumwangusha Mhasibu wa Kampuni ya simu ya Zantel, Ali Bakari aliyepata kura 97.

Kwa upande wa ubunge Jimbo la Chakechake, Yusuph Kaiza Makame ameibuka kidedea kwa kura 84 baada ya kumuangusha Fatma Omar Juma aliyepata kura 83, huku Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Duni Haji akishinda kwa kupigiwa kura za ndiyo baada ya mpinzani wake Ali Juma Khamis kujitoa dakika za mwisho na kupata kura 60 kati ya 61 katika nafasi ya uwakilishi jimbo la Bububu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui amepita katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Mtoni, lakini mbunge, Faki Haji Makame ameanguka.

Katika Jimbo la Mtambwe, Mbunge wake, Khalifa Mohamed Issa ameangushwa katika kura za maoni pamoja na Mwakilishi wake Salim Abdallah Hamad huku Mbunge wa Ole Rajab Mbarouk Mohamed naye akianguka lakini Mwakilishi wa jimbo hilo, Hamad Masoud akiibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza.

Mbunge wa Micheweni, Rashid Ali Abdallah pamoja na Mwakilishi wake, Subeti Khamis Faki wamefanikiwa kuzitetea nafasi zao na kuibuka washindi katika kura za maoni, wakati Mbunge wa Konde Khatib Said Haji akiibuka na ushindi, upande wa Mwakilishi, Suleiman Hamad Khamis aliangushwa.

Mwakilishi wa Jimbo la Wete, Asaa Othman Hamad naye ameangushwa katika kura za maoni, wakati Mbunge, Mwadini Abbas Jecha akitetea nafasi yake, huku Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakari akishinda kwa hekaheka nafasi ya uwakilishi lakini Mbunge wa jimbo hilo, Kombo Khamis Kombo akianguka kwenye kura za maoni kwa kura 61 na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Kombo Hamad aliyepata 106.

Wagombea uwakilishi, Ismail Jussa Ladhu na Mansour Yusuph Himid walipitishwa wakiwa ni wagombea pekee katika majimbo ya Mji Mkongwe na Kiembesamaki, mtawalia, huku kamishna wa zamani wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Mohamed Hashim Ismail naye akiibuka na ushindi wa nafasi ya uwakilishi Jimbo la Dimani huku Khalid Said Suleiman ‘Gwiji’ akishinda katika nafasi ya ubunge wa jimbo hilo.

Waziri wa zamani wa Utalii na Maliasili katika Serikali ya awamu ya Pili, Juma Hamad Omar alipita kuwania ubunge wa Jimbo la Wawi kuziba nafasi ya Hamad Rashid Mohamed huku Mwakilishi wa jimbo hilo Saleh Nassor Juma akianguka kwenye nafasi hiyo.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s