Maalim Seif adhaminiwa tena kugombea Urais Zanzibar

Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, cheti cha heshima kutokana na uongozi wake
Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, cheti cha heshima kutokana na uongozi wake

Salma Said,

ZANZIBAR: Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad jana ametangaza nia yake ya kugombea tena nafasi ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao na kusisitiza kwamba suala la yeye kuingia madakarani atakaposhinda halina mjadala.

Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na kamati maalum ya (CUF) Zoni ya Mjini iliyokwenda kumdhamini kugombea nafasi hiyo huko nyumbani kwake Mbweni, Maalim Seif amesema anatarajia kugombea tena nafasi hiyo ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar kama alivyowaahidi mwaka 1988.

“Nimekuwa nikiulizwa sana na waandishi wa habari vipi nitagombea tena urais, Naam ndio nitagombea na leo ndio nasema kwamba nitagombea tena katika kinyanganyiro hiki mimi sio kama CCM kama nitaogopa kutangaza nia wao wanaogopana” alisema Maalim Seif.

Alisema tokea mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi chama hicho kimekuwa kikiibuka mshindi katika chaguzi zote, lakini hakikupata kutangazwa hata mara moja kuwa ndicho kilichoshinda, jambo ambalo halitatokea kwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi fedha taslim Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, ili aweze kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar wakati utakapofika
Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi fedha taslim Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, ili aweze kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar wakati utakapofika

Maalim Seif alisema CUF hakijapata kufanya maandalizi makubwa na yenye ufanisi katika chaguzi zote zilizofanyika, kama kiliyofanya kwa ajili ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu na hakuna sababu chama hicho kisichukue uongozi wa nchi.

Tumejiandaa, watake wasitake tutachukua nchi, iwapo wananchi wa Zanzibar watatuchagua katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu”, alisema Maalim Seif.

“Waheshimiwa mara hii tume ya uchaguzi ikitutangaza au usitutangaze sisi tunachukua serikali inshaalah, na sisi CUF tokea uchaguzi wa mwanzo wa 1995 tunashinda lakini tume ya uchaguzi haitutangazi na mie mara zote nakubali lakini mara hii nasema hilo halitatokea tena” alisisitiza Maalim Seif.

Aidha aliwaambia wanachama wake kwamba katika kuhakikisha chama hicho kimejiandaa vizuri kwa kwenda Ikulu katika uchaguzi huu kumekuwepo na matayarisho mbali mbali ambayo yameanza kuonekana ikiwemo wagombea wa chama hicho kujipanga katika kuwania nafasi mbali mbali za ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Wenyewe mmeona jinsi tulivyojiandaa kuchukua serikali na si mmeona tulivyojitayarisha na hatutaki mchezo matayarisho yetu tuloyafanya mara hii ni makubwa kwa sababu suala la kuwa Maalim Seif ataendewa ataombwa akubali matokeo mara hii nasema haliwezekani” aliongeza Maalim Seif.

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akionyesha fedha alizokabidhiwa kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akionyesha fedha alizokabidhiwa kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais

Hata hivyo hakusema watafanya nini iwapo tume ya uchaguzi itamtangaza mgombea kutoka chama cha mapinduzi lakini alisema matayarisho na mipango yote ya yeye kushinda na kuchukua serikali yamekamilika na kuwataka wafuasi wake wajitayarishe kwenye ushindi na kuona mafanikio makubwa ambayo yatafanyika baada ya kukabidhiwa madaraka hayo.

Alieleza kuwa kila siku zikienda mbele Wazanzibari wanazidi kubaini kuwa CUF ndicho chenye nia njema na Zanzibar na Wazanzibari wote, na hawatarudi nyuma hadi kitakapoingia Ikulu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Wananchi wakishaamua ndio wameamua, na Wazanzibari kwa kweli wana haki ya kukipa takala CCM, kwa vile kimeshinda kutimiza matarajio yao”, alieleza Katibu Mkuu wa CUF.

Akielezea mambo ambayo atayapa kipaumbe Maalim Seif alisema CUF kitapaoingia Ikulu ya Zanzibar kazi kubwa itakayofanyika ni kutandika misingi ya Utawala Bora, misingi ya kuwa na uchumi ulio imara na kuwaunganisha Wazanzibari ambao wamekuwa wakibaguliwa chini ya uongozi uliopo sasa.

Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema wananchi wa Zanzibar wameshaamua kukikubali chama cha CUF baada ya kuona ndio tegemeo lao la kuikomboa Zanzibar kiuchumi, kuwarahisishia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii pamoja na kulinda hadhi na heshima ya Zanzibar.

Alisema jambo jengine ambalo Wazanzibari wategemee chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF, ni kuimarika kwa huduma za kijamii, zikiwemo huduma za afya, maji na elimu bora ambayo itamuwezesha kijana aliyehitimu Zanzibar kumudu ushindani na kijana kutoka nchi yoyote ile.

Akizungumzia Muungano, Maalim Seif alisema wananchi wa Zanzibar watapata fursa ya kuulizwa iwapo wanataka Muungano huo na uwe wa aina gani, ili kuwepo usawa kati ya pande mbili za Muungano huku akisema mfumo uliopo una kasoro nyingi ambazo zimekuwa zikiwaumiza wananchi na kuulalamikia.

Maalim Seif alisema kinachojitokeza sasa kwa baadhi ya viongozi wa upande wa Tanzania Bara kwa kauli zao wanazozitoa hawana nia njema kwa Zanzibar na ni wazi nia yao ni kuona Zanzibar inafutika kabisa katika ramani ya dunia.

“Wanaonekana nia yao ni kuimeza Zanzibar, lakini dua zenu zimesaidia, imekuwa kama tembo aliyemeza chura na amemkaa kooni, lazima atamtema tu”, alisema Maalim Seif.

Awali akisoma risala katika hafla hiyo, Salum Abdallah Salum ilisema, 2015 ni mwaka ambao nchi itashuhudia mafanikio makubwa chini ya uongozi wa CUF huku akiwatoa khofu wazanzibari kwamba wategemee mambo mazuri katika maisha yao na matumaini kwa vizazi vyao na kuwataka wakiunge mkono chama hicho hadi kupatikana kwa Mamlaka kamili.

Kamati hiyo ya CUF Zoni ya Mjini imemdhamini Maalim Seif kwa fedha taslim shilingi milioni mbili na laki tano, ili iweze kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar wakati utakapofika.

Maalim Seif ameishukuru kamati hiyo kwa uamuzi wa busara waliochukua, hali inayoonyesha kuwa wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuwa na imani naye kutokana na mwelekeo wake wa kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kwa Zanzibar na kuwaahidi fedha hizo atazitumia kwa umakini na kwa haja iliyokusudiwa.

“Naahidi fedha hizi nitazitumia wakati ukifika nitatoa milioni moja na nusu kwa ajili ya kuchukua fomu katika chama changu iwapo watanipitisha na kisha nitakifunga kibweta changu vizuri nasubiri tume ya uchaguzi ikishatangaza kutoa fomu natoa zilizobaki kwenda kupeleka tume inshallah” aliwaambia waliompa fedha hizo.

Baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF waliojitokeza katika hafla ya kumkabidhi fedha Maalim Seif iliyofanyika nyumbani kwake Mbweni.  Picha: Salmin Said - OMKR
Baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF waliojitokeza katika hafla ya kumkabidhi fedha Maalim Seif iliyofanyika nyumbani kwake Mbweni.
Picha: Salmin Said – OMKR
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s