Mzee Moyo: Walionifukuza ni watoto wasiojua kitu

Mzee Hassan Nassor Moyo aliyefukuzwa uanachama hivi karibuni na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mzee Hassan Nassor Moyo aliyefukuzwa uanachama hivi karibuni na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Salma Said, Zanzibar

Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Mjini Magharibi imetangaza kumfukuza uanachama kada na mmoja wa waasisi wa chama hicho, Nassor Hassan Moyo. Moyo, ambaye pia ni mwasisi wa Muungano mwenye kadi namba 000007 ya chama hicho, sasa anaitwa msaliti ndani ya chama alichokitumikia kwa miaka mingi.

Amefukuzwa kwa makosa mawili; kutetea sera za serikali tatu na kutetea mamlaka kamili ya Zanzibar,  mambo ambayo kwa jumla ni kinyume na msimamo wa CCM.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziza Ramadhani Mapuri, alinukuliwa akisema Mzee Moyo amefukuzwa kutokana na mwenendo wake usiozingatia maadili ya chama chake.

10660187_1458652554426235_3103696690392008294_n-430x320

Mwenyewe anasemaje?

Moyo, ambaye ni mmoja wa vinara wa  Mapinduzi ya Zanzibar walio bado hai, anasema:

 “Sijashtushwa wala kushangazwa na uamuzi wao, maana wenye kufanya hivyo ni watoto wadogo na hawajui wanachokifanya.

Anasema wakati huu ambao Zanzibar inahitaji mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiuongozi, kunahitajika watu wenye misimamo madhubuti, huku akiwanasihi  kutokuwa na  hofu kwani mabadiliko hayawezi kuzuilika.

“Mimi siwezi kurudi nyuma asilani kwa sababu ninachokitetea ni maslahi ya Zanzibar. Kwa hivyo, nitaendelea kukitetea na kukiamini kile nilichosimamia,” anaeleza.

Anasema uamuzi uliotolewa na CCM wa kumvua uanachama anauchukulia kama ni wa kitoto, kwani  yeye hakuzaliwa  CCM na wala hakuna wa kumzuia asiwe na maoni tofauti.

 “Hatuwezi kuwa na maoni na mtazamo wa aina moja, kila mmoja ana mtazamo wake na mimi huu ndiyo mtazamo wangu, kwa hivyo siwezi kubadilika. Waache  wanifukuze lakini mimi siogopi kwani sikuogopa wakati wa Mzee Karume nilipokuwa nikisema…eeeeh nitaogopa sasa hivi?” anahoji Mzee Moyo na kuendelea kusema:

 “Basi na tukubaliane kutokukubaliana haidhuru lakini hawawezi kunifunga mdomo nitaendelea kutetea Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili na kamwe sitorudi nyuma

“Mimi hata mara moja sikuwahi kusema au kutamka kwamba nilikuwa mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, na hata mara moja sikuwahi kusema au kutamka kuwa mimi ni mjumbe wa kamati ya watu 14. Ninachosema mimi ni mmoja wa waanzilishi wa Baraza la Mapinduzi na serikali yake ya mwaka 1964”.

Kamati ya Maridhiano ambayo Mzee Moyo ndio mwenyekiti wake
Kamati ya Maridhiano ambayo Mzee Moyo ndio mwenyekiti wake

 Tuhuma zake

Miongoni mwa makosa yalioorodheshwa na chama hicho yanayomhusu Mzee Moyo ni pamoja na lile la kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Februari 9 mwaka 2014 katika uwanja wa Tibirinzi uliopo Pemba.

Inaelezwa kuwa alipopanda jukwaani, alisema anamuamini Maalim Seif Sharif na kumkubali Mwenyekiti wa CUF.

Kosa lake jingine alilifanya Aprili 6 2014 katika kongamano lililoandaliwa na CUF. Siku hiyo Mzee Moyo anadaiwa alisema Muungano haukuletwa na ufalme na mkataba wa Muungano haujulikani ulipo.

Anadaiwa pia kutamka kuwa wajumbe wote waliokuwapo katika lililokuwa Bunge la Katiba walipaswa kutetea Zanzibar na Tanganyika na akaonya kuwa wakileta Katiba mbaya wananchi wataikataa.

Kosa jingine la Mzee Moyo kwa mujibu wa CCM, lilifanyika Aprili 30 2014, aliposimama jukwaani katika mkutano ulioandaliwa na CUF na kusema Serikali tatu ndiyo msimamo wa Zanzibar.

Kutokana na tuhuma hizi na nyinginezo, CCM wanasema Mzee Moyo alikiuka taratibu za Chama cha Mapinduzi.

Kwa mujibu wa taratibu hizo za kikatiba, mwanachama anatakiwa kuhudhuria na kutoa maoni yake katika mikutano ya chama.

hassan-nassor-moyo

Nassor Moyo ni nani?

Alizaliwa mwaka 1933. Alipata elimu yake ya msingi kuanzia mwaka 1940 hadi 47 katika shule ya Mnazi Mmoja iliyopo kisiwani Unguja.

Mwaka 1955 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha wafanyakazi huku yeye akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza.

Mwaka 1960, alikwenda nchini Urusi kwa mafunzo ya uongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa mwaka mmoja, kabla ya kuteuliwa na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) kugombea ubunge wa jimbo la Mwangapwani bila ya mafanikio.

Nyadhifa Serikalini

Mzee Moyo aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi kuanzia mwaka 1964 hadi 1985.

Aidha kutoka mwaka 1964 hadi 1985, alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mfano alikuwa waziri mdogo wa kazi (1964); Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Aprili – Septemba 1964); Waziri wa Kilimo Zanzibar (1964 hadi 1967); Waziri wa nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1972-1977); Waziri wa mambo ya Nchi (1977-1980 ) na Waziri wa Kilimo Zanzibar ( 1980-1985).

Uzoefu wake kisiasa

Alijiunga na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) mwaka 1957 na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya chama na Katibu Mipango kuanzia 1972-1977.

Mwaka 1977, aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya watu 20 waliounda Chama Cha Mapinduzi. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM 1977-1992 na baadaye mwaka 1987 hadi 199, aliteuliwa kuwa Katibu wa Mkoa wa Dodoma. Alistaafu rasmi shughuli za kichama na kiserikali mwaka 1996.

One Reply to “Mzee Moyo: Walionifukuza ni watoto wasiojua kitu”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s