Kweli CCM wanamuogopa Maalim Seif

Maalim Seif Sharif Hamad
                                                           Maalim Seif Sharif Hamad

Na Jabir Idrissa

 CHAMA cha CCM kimepwaya sana. Hata wanaoishi nacho wanajua mvuto wake katika zama hizi, sio ule uliozoeleka miaka ya 1990. Hakivutii tena, kwa waliomo ndani na hata wanaofikiria kujiunga.

Ni kwa sababu hiyo, katika miaka hii 23 ya siasa za ushindani, zilizoruhusu vyama vya mageuzi kusajiliwa, kwa sehemu kubwa kimeishi kwa kutegemea kudura ya Mungu.

Lakini, Jeshi la Polisi Tanzania, linalowasaidia na kuwalinda, halitumwi na Mungu. Mabaya yanayofanywa kuvikandamiza vyama vingine, si maamuru ya Mungu, hata kidogo; ni utashi wa wakuu wenyewe wa jeshi.

Kwamba Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamza Omar Makame ametumwa na Mwenyezi Mungu kuzuia wananchi walioko nje ya jimbo la Kitope, kwenda jimboni kusikiliza maneno matamu ya Maalim Seif Shariff Hamad na wasaidizi wake CUF, si kweli.

Kamishna huyu aliyeapa kufanya kazi kwa haki na kuzingatia sheria alipokwenda kumsalimia Maalim Seif katika wadhifa wake wa makamo wa kwanza wa rais, amebadilika.

Si yule wa 2013 alipoteuliwa. Sasa anaruhusu askari wafurushe wananchi kwa mabomu ya machozi, kwa kuwa tu wanamfuata wanayemuamini anawakonga moyo.

Angalia tofauti: wakuu wa polisi wanahimiza wananchi wafuate sheria bila shuruti. Wao wanavunja haki za wananchi kwa kutoa shuruti.

Hawataki vyama vifike kwa wananchi kutafuta wanachama, na wanazuia watu kusikiliza sera za vyama, jambo lililo haki kikatiba. Unashirikije siasa bila kusikiliza wanasiasa?

Kamishna Hamza anajua kutoa amri kuwa watu wasifike sijui mji wa pili au wa watu, au mkoa mwingine kusikiliza sera ni amri batili kisheria.

Hivi ukomo wa mwananchi kwenda kufuata siasa upo kifungu gani katika Sheria Na. 11 ya Usajili wa Vyama vya Siasa ya 1992?

Kama ni kweli Inspekta Jenerali Ernest Mangu anaamini wanachotakiwa Polisi baada ya kupewa taarifa ya mkutano wa chama, ni kutoa ulinzi, tuone basi anadhibiti wasaidizi wake walioporomosha mabomu ya machozi kuvuruga watu wasiende mkutanoni Kitope.

Kwani Kitope ni jimbo la Mungu au la wananchi wenye haki ya kushiriki siasa kwa kusikiliza kila mwanasiasa, kila kiongozi na kila chama, na kuachiwa wenyewe kuchagua wapendacho?

Wakubwa watumikia CCM hawaoni wanajisumbua tu kuzuia watu leo – ukweli banda linafungwa farasi keshatoka.

Hata wanapomtoa mzee Hassan Nassor Moyo kwenye chama chao, wanajiudhi bure. Mzee Moyo ana moyo uliotokana na moyo wake wa kuwatia moyo Wazanzibari kwa kutaraji mamlaka kamili. Inataka moyo vilevile kuamini haya.

Mzee Moyo hana cha kukosa. Hataraji cheo wala pesa kupitia CCM. Amedhamiria tu kuacha alama kwa anayoyaamini. Na kwa hili amefanikiwa sihaba.

Zipo siri za namna CCM ilivyofanikiwa kutangazwa mshindi katika uchaguzi mara zote nne tangu ule wa kwanza wa mwaka 1995 baada ya mfumo huo kurudishwa. Inahusu Zanzibar na hata Tanganyika.

Kule kuwa ni chama kinachoshika dola, kunakisaidia kujipanga na kujihakikishia kufanikiwa kwa malengo yake, likiwemo la kuendelea kushika madaraka bila ya kujali njia zinazotumika.

Kwa hivyo, kupumua kwake kunategemea ulegevu wa dola inayoonekana haijali kujidhalilisha; inakubali pasina shida kujipakatisha kwa wakuu wa CCM na kuwatii kwa kila jambo.

Utaratibu huu unaendana kabisa na kauli aliyopata kuitoa Frederick Sumaye mwaka 1997, akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliposema, “wewe ukitaka biashara zako ziende bila shida, egemea tu CCM.”

Watu wengi, wakiwemo wafanyabiashara na mafisadi wa ardhi, waliitumia kauli hiyo kujilimbikizia mali kwa njia mbalimbali.

Walipora viwanja na maeneo ya wazi; wakamilikishwa kwa kusaidiwa na watumishi wa manispaa, miji na majiji walioona wangejisumbua tu kukataa milungula.

Hata wangeikataa, isingewasaidia kwani wangebakia na unyonge na hata kuhatarisha kazi kwa vile wangeweza kufanyiziwa na wakubwa serikalini ambao mara zote huonesha utii kwa wakuu wa CCM.

Ni suala la mtumishi kuchagua – ama maslahi yangu binafsi nisigombane nao, au kuheshimu utaratibu wa kazi nikosane nao.

Siku zote ukitenda ambalo litakuwa limechangia uhai hata kidogo tu wa CCM, inayokabiliwa na hatari ya kukosa utawala, bila ya kujali umelitendaje – maana mengi yanatendwa kijinai – utalindwa.

Anayoyafanya bwanamkubwa wa Tumbatu ya kuchochea chuki na kuhujumu wasiopenda CCM, si tatizo kwa kuwa yanakisaidia chama chao kupumua.

Yeye na wakubwa zake wanaamini ni sawa tu maana muhimu ni kukipatia ushindi chama. Eti kuvuruga watu kunakipatia ushindi chama cha siasa. Unakwepaje kusema kina viongozi waliochoka?

Nimesimuliwa jimboni Makunduchi, ngome inayomeng’enywa ya CCM, wanashutumiana. CUF inazoa umma wa vijana na wanawake, wapigakura wakuu nchini. Wajumbe wa Wilaya wameketi na kugombana “mbona tunazidiwa kete n’kafu (na CUF).”

Anatajwa maalim Haroun Ali Suleiman, mwakilishi na waziri katika serikali. Ameahidi wananchi hajatimiza ahadi. Hajatoa msaada wa skuli ya kompyuta na Kiingereza ya klabu ya Jamhuri ya Kijini.

CCM Kusini wamemjia juu kukaa nyuma huku madume ya Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu na Jihad Hassan wakichangia. Ushahidi wa siasa kuwa vitendo sio maneno!

Udhaifu huu wa mwakilishi unatumika kuthibitisha ilivyo shida chama kupiga kampeni kuomba kura za Oktoba hasa wakati tayari wanachama wanaingia CUF.

Jimbo la Makunduchi lililokuwa haligusiki, sasa ni huria. Na hicho ndio kinasukuma mabwana na mabibi wakubwa wa CCM – mwakilishi, mbunge na wajumbe wa kamati ya siasa wilaya – kuamini maeneo ya jimbo yataishia Jozani ili iwe rahisi kulitwaa.

Wanasemezana jimbo la Muyuni halitakuwepo. Badala yake, maeneo ya Jambiani, Paje na Bwejuu, ambako CCM imedhoofishwa sana kiudhibiti, yatajumuishwa kwenye jimbo la Koani.

Itakuwa ajabu kubwa hilo likiwa. Jimbo la Koani litakuwa ndio lenye urefu zaidi kwa Zanzibar. Na je, Wilaya ya Kusini itaishia wapi? Kwa sababu Koani ni jimbo ndani ya Wilaya ya Kati wakati Jambiani, Paje na Bwejuu ni vijiji ndani ya Wilaya ya Kusini.

Ndio kama yanayosemwa Kiembesamaki litafutwa. Fuoni yatakuwa mawili kwa kukata maeneo ya Dimani kutengeneza jimbo jipya. Eti Dole litagawiwa kuleta jimbo jipya. Mahangaiko yasiyo sababu ya msingi.

Mbele ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wala hawatajiuliza maswali haya maana kwao, la muhimu ni kutekeleza tu watakalo CCM. Baadaye watajua utetezi utakavyokuwa mbele ya malalamiko ya upinzani kupitia vyombo vya habari. Labda mahakamani ikipelekwa kesi kupinga.

Hii “tufanye tu muhimu CCM ishinde” ni kujisumbua. Tatizo lililopo ni kwamba chama hiki hakina tena mvuto kwa Watanzania, kwa Wazanzibari ndio usiseme.

CCM hakipendi tena watu, watu hawategemewi tena kwa ushindi, bali mabavu na ghilba. Sasa, wajitahidi kushinda nyoyo za Wazanzibari sio kutengeneza visingizio na vitisho.

Vinginevyo, nakosea wapi kusema hakika wanamuogopa Maalim Seif.

Chanzo: Mawio

Advertisements

2 Replies to “  Kweli CCM wanamuogopa Maalim Seif”

  1. Reblogged this on Haki Sawa kwa Wote and commented:
    Kama ni kweli Inspekta Jenerali Ernest Mangu anaamini wanachotakiwa Polisi baada ya kupewa taarifa ya mkutano wa chama, ni kutoa ulinzi, tuone basi anadhibiti wasaidizi wake walioporomosha mabomu ya machozi kuvuruga watu wasiende mkutanoni Kitope.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s