Mansoor afunguka

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha Mansour Yussuf Himid kwa wanachama wa Kiembesamaki na kuwaomba wamuunge Mkono.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha Mansour Yussuf Himid kwa wanachama wa Kiembesamaki na kuwaomba wamuunge mkono.

Na Jabir Idrissa

TAMKO la Mansour Yussuf Himid, kuwa atagombea uwakilishi jimbo la Kiembesamaki, limechangamsha siasa za jimbo hili kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa ushindani wa kivyama urudishwe nchini mwaka 1992.

Na lazima niseme mapema, hatua yake hiyo inajenga daraja imara kati yake na wanajimbo katika safari ya kulijengea miundombinu kwa ajili ya miradi ya kiuchumi ya wananchi, huduma za kijamii na ajira kwa vijana.

Mansour, mwanasiasa kijana aliyekula mtukutu akisema atapigania mamlaka kamili ya Zanzibar kwa nguvu zote, akiwa ubavuni kwa Maalim Seif Shariff Hamad, amejitoa kwa watu wa Kiembesamaki.

Anataka awatumikie kikwelikweli na katika zama mpya kwa kuwa sasa ameingia itikadi mpya ya chama kingine, mbali na ile aloisimamia chini ya CCM.

Aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki (CCM) Mansour Yussuf Himid, akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika jimboni humo.
Aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki (CCM) Mansour Yussuf Himid, akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika jimboni humo.

Mansour anajua wakati ule akiwa mwakilishi wa jimbo hili linaloishi watu mchanganyiko, wakiwemo mafukara; wenye kipato cha kawaida; wafanyabiashara wakiwemo wenye utajiri wa kiasi chake; wasomi wakiwemo wataalamu na viongozi serikalini, mambo hayakuwa mazuri hasa.

Ukweli huu unathibitishwa na kauli aliyoitoa mwishoni mwa wiki, katika mkutano wa hadhara ndani ya jimbo, aliposema “nawaomba radhi kwa matendo mliyokuwa mkitendewa, yakiwemo kupigwa na kudhalilishwa wakati mimi nikiwa katika serikali.”

Ni kauli inayoonesha Mansour anajutia makosa ya kiuongozi yaliyotendwa na serikali kwa Wazanzibari, wakiwemo wanajimbo, wakati akiwa kiongozi mkubwa.

Mansour alifukuzwa CCM Agosti 2013 kwa tuhuma za kusaliti sera za chama hicho kuhusu Muungano. Ingawa ilikuwepo fursa ya kukata rufaa, aliikataa akisema, “sina sababu, kama hawanitaki katika chama chao, nami nasema basi.”

Anajua watu wa Kiembesamaki, kama walivyofanyiwa wa majimbo mengine nchini, nao walipigwa vipigo kishetani, wakadhalilishwa na kunyanyaswa. Anajuta na kuazimia kushiriki kujenga upya nchi.

Wafuasi na wapenzi wa CUF wakifuatilia mkutano huo wa kumtambulisha Mansour.
Wafuasi na wapenzi wa CUF wakifuatilia mkutano huo wa kumtambulisha Mansour.

Hayo anayasahau na kuahidi matumaini. Anataka wananchi wamuunge mkono anaposaka uwakilishi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), alichojiunga karibuni, baada ya kuridhika ndio chama chenye dhamira ya kweli ya kuipatia Zanzibar mamlaka kamili ili kuendeleza Wazanzibari.

Ona anavofunguka kwa kuutambua na kuuthamini ukweli – kwamba amejiunga CUF na kujiandaa kutoa mchango muhimu wa kuleta mabadiliko, yeye akijitangaza waziwazi kuwa mfuasi imara wa Maalim Seif.

Ameamua kumsifia Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, tangu alipofukuzwa CCM. Anaamini ndiye mwanasiasa pekee muaminifu na mwenye ujasiri wa kuisimamia Zanzibar ipate mamlaka kamili.

Safari yake CUF ilijaa mtihani kwani alisakamwa na CCM, akafukuzwa, kitendo kilichoshtua waliokuwa wakimuamini na kutaraji mchango wake katika kubadilisha hali zao.

Mwenyewe anasema ilikuwa safari ngumu. Wazee na vijana jimboni waliamini amekwisha kisiasa. Wakati anatafakari, wakashtukia anakamatwa na kufunguliwa kesi ya jinai ya kumiliki silaha isivyo halali.

Mpaka leo haijaanza kusikilizwa wakati akiwa nje kwa dhamana.

Anairejea hali ilivyokuwa jimboni baada ya kufukuzwa CCM. “Mlilia sana, niliwaambieni tulieni wakati bado. Mlinifariji nilipoamua kujiunga CUF. Mlikuwa na wasiwasi kwamba baada ya mimi kwenda jela sitagombea uwakilishi.

Mliona nilikuwa taabani (kisiasa). Nawapa pole mliopata misukosuko kama yangu, wazee na vijana wenzangu, sasa nimekuja rasmi kwenu kusema nitagombea na naomba tushirikiane kwa hili.”

Kwa sababu hakuwa jeuri, anajiamini ipo fursa ya kupata ushindi bila nguvu kubwa. “Katika harakati zangu hizi nitaomba kura hata katika matawi ya CCM, haya matawi nimeyajenga mwenyewe. Sitoogopa matawi ya CCM, nitakwenda na kuingia humohumo, hizi ndio siasa za CUF za leo, CCM na CUF wote watu wangu,” anasema.

man4

Mansour alichukua fomu katika tawi la CUF Kiembesamaki, na kuirudisha baada ya kuijaza kabla ya Machi 10. Alijitoa kuridhia kufukuzwa CCM, leo anajitoa kwa mara nyingine akitaka wanajimbo walewale wamuunge mkono kugombea uwakilishi kupitia CUF.

Wananchi jimboni Kiembesamaki wana kila sababu kumuamini. Wamuone yuleyule aliyewatii na amebakia muaminifu hata wakimchagua kupitia CUF.

Wanampa dhamana ileile, lakini ni katika mtizamo mpya wa kusaidia watu chini ya siasa za maridhiano ambazo CCM wanazifitini bali CUF wanaziamini ndio ufumbuzi wa uchumi duni Zanzibar.

Wale ambao hawajaelewa mantiki ya mwelekeo mpya wa siasa za ndani ya jimbo lao, wasizubae wala kumshangaa.

Wamchukulie kuwa amepata akili ya kuiona njia sahihi ambayo inampa fursa ya kusema hadharani analoliamini kuwa ndio linaifaa Zanzibar na linawafaa Wazanzibari, wakiwemo wa Kiembesamaki.

Mansour amechagua siasa zinazozingatia ukweli wa mambo na yeye kujitoa kuueleza hivyo bila ya woga wala chuki – alivyoamua kuanzisha msamiati wa ‘Tuachiwe tupumue’ wakati kukianza mjadala mzito kuhusu mustakbali wa Zanzibar chini ya Muungano.

Wakati ule bado alikuwa CCM na hali inaonesha dhahiri kuwa uamuzi wake huo ndio uliochochea kuibuka viongozi wanaompinga ambao hatimaye walipanga njama kumchonganisha na chama hicho.

Ni hapo wabaya wake hao wakafanikiwa kuwezesha kumtungia tuhuma na zilipofikishwa mbele ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa, inayokaa chini ya mwenyekiti wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein, zikamtengenezea mlango wa kutokea.

Anasema hajutii kufukuzwa CCM, chama ambacho kina mchango wa nguvu za marehemu baba yake – Yussuf Himid, aliyekuwa mmoja wa waasisi wa mapinduzi ya Januari 1964 chini ya Afro-Shirazi Party (ASP).

Sijuti, wala siwezi kumnunia mtu yeyote; nitaendelea kuwaheshimu (waliomfukuza) kwa vile ni chama chao,” anasema katika mkutano wa hadhara alioutumia kutangaza kugombea uwakilishi.

Mansour ana historia muhimu katika kutandikwa kwa siasa za maridhiano Zanzibar. Ndiye – wakati akiwa Waziri wa Maji, Ardhi, Nishati na Mazingira – aliyekuwa msiri mkuu wa Amani Abeid Karume alipoanzisha majadiliano na Maalim Seif ya kufuta siasa chafu.

Miaka sita baadaye, anasema leo, “mnakumbuka niliwaambia umuhimu wa maridhiano katika kujenga jamii iliyotulia. Ingawa wawakilishi wenzangu wengi ndani ya CCM walipinga tukiwa Baraza la Wawakilishi, sikutetereka, niliamini lengo siyo kumtengenezea Maalim Seif nafasi ya uongozi au CUF kutoa mawaziri saba kuingia katika serikali.”

Maalim Seif hana njaa, mawaziri hawana njaa, tunataka kuleta utulivu, hizi siasa za ufisadi zinamuumiza Maalim, ana dhamira ya kuondoa chuki na kujenga historia mpya chini ya serikali imara, yenye vyombo vinavyolinda misingi ya uadilifu na kuhimiza utamaduni wa uwajibikaji,” anasema Mansour.

Anasema wakati muafaka utakapofika, atampitisha Maalim Seif majimboni ikiwemo Kiembesamaki ili kumuombea kura kwa le ngo la kuunda serikali itakayotumikia watu kwa umakini.

Amemtaja Maalim Seif kuwa ndiye kiongozi mwenye utashi wa kweli wa kusimamisha uongozi mwema katika serikali, kwani ndio chimbuko la kupatikana maendeleo yanayolenga kuinua hali za wananchi.

Hapana shaka uchaguzi wa Oktoba utakuwa na ushindani mpya huku imani kubwa ya wananchi wakiielekeza kwa shujaa huyu wa maridhiano.

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s